Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuguswa na mahangaiko ya mamilioni ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; ukame na majanga asilia; watu wanaoendelea
kutumbukia katika umaskini kutokana na vita pamoja na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa! Jumuiya ya Ulaya pamoja nachangamoto zake, kamwe isiwageuzie kisogo wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi, kwa kutambua kwamba, hata wao ni sehemu ya matatizo yanayozikumba nchi maskini zaidi duniani kutokana na ukoloni! Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kushikamana kwa dhati katika kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotishia maisha, usalama na maendeleo ya wengi!
kutumbukia katika umaskini kutokana na vita pamoja na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa! Jumuiya ya Ulaya pamoja nachangamoto zake, kamwe isiwageuzie kisogo wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi, kwa kutambua kwamba, hata wao ni sehemu ya matatizo yanayozikumba nchi maskini zaidi duniani kutokana na ukoloni! Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kushikamana kwa dhati katika kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotishia maisha, usalama na maendeleo ya wengi!
Haya ni kati ya mambo msingi yaliyojiri katika mahojiano maalum kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Bwana Eugenio Scalfari, mwandishi wa Gazeti la Repubblica linalochapishwa kila siku nchini Italia. Kiini cha mahojiano haya ni “Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana”. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya upendo miongoni mwa binadamu. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele unaopaswa kumwilishwa kwa maskini, wagonjwa na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Kristo Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha haki na amani; mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki na amani duniani. Yesu Kristo ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake. Hii ndiyo imani ambayo Kanisa linaona fahari kuiungama na kuifundisha kwa watu, ingawa Bwana Eugenio Scalfari anakiri kwa kusema kwamba, si mwamini ingawa anamsikiliza Baba Mtakatifu kwa moyo wake wote!
Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kuna mpasuko mkubwa kati ya viongozi wa G20 kuhusiana na masuala tete na changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa. Hakuna uhusiano mwema kati ya Marekani na Russia, bado wanaendelea kushutumiana kwa sababu mbali mbali, hali inayowafanya viongozi wa mataifa haya kusigana hata kwa mambo ambayo ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Bado kuna pengo kubwa la mahusiano kati ya Korea ya Kaskazini, China na Marekani. Kuna watu wanao muunga mkono Rais Bashar Al Assad na msimamo wake wa kisiasa huko Siria; Rais Puttin wa Russia anaendelea kutengwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya! Zote hizi ni changamoto zinazohofisha mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa pamoja na maamuzi yake juu ya mustakabali wa utekelezaji wa maamuzi mbali mbali yanayofanywa kwenye mikutano na vikao kama hivi!
Changamoto kubwa anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; ongezeko la umaskini wa hali na kipato duniani kutokana na vita, majanga asilia pamoja na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Hata katika nchi zilizoendelea kuna umaskini unao endelea kuongezeka kila kukicha kiasi cha kuwajengea watu hofu ya kuvamiwa na wahamiaji pamoja na wakimbizi. Ulaya imesahau kwamba, ilikuwa ni chanzo cha uvamizi kwa nchi maskini na matokeo yake ukoloni ukaingia na kuota mizizi. Huu ni mfumo uliokuwa na mazuri yake, lakini pia umesababisha madhara makubwa kwa uchumi na maendeleo na mafungamano ya kijamii. Bara la Ulaya likabahatika kupata utajiri mkubwa, lakini leo hii linataka kuwageuzia kisogo wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Kuna hatari kubwa ikiwa kama maamuzi yanayotolewa na Jumuiya ya Kimataifa hayatekelezwi kwa ufasaha kwa kujikita katika utaifa usiokuwa na mshikamano wala udugu na wale wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia.
Bwana Eugenio Scalfari katika mahojiano maalum na Baba Mtakatifu amegusia pia changamoto zilizowakumba wana falsafa kama akina Baruch Spinoza na Blaise Pascal kiasi hata cha kutengwa na Kanisa, kama ilivyokuwa hata kwa Shirika la Yesu. Mwanafalsafa Blaise Pascal alionesha moyo wa toba na wongofu wa ndani; akayaacha malimwengu na kuambata ufukara, mfano bora wa kuigwa kwa kutangazwa kuwa Mwenyeheri. Hapa, Baba Mtakatifu anakaza kusema, ili mwamini aweze kutangazwa kuwa Mwenyeheri, sheria, taratibu na kanuni zote zinapaswa kufuatwa na hatimaye, Khalifa wa Mtakatifu Petro, kutoa maamuzi yake.
Kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuendeleza safari ya Kanisa iliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kweli zile cheche za mageuzi zilizoletwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ndani ya Kanisa ziweze kumwilishwa katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Kwa hakika Kanisa, halina budi kufanya hija ya kumwelekea Kristo Yesu, huku likiwasaidia watu kukutana ili kwa pamoja waweze kusonga mbele kumwendea Kristo Yesu.
Hii ndiyo dhana ya Sinodi inayopewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa halina budi kuwaambata wote kwa kujiaminisha chini ya ulinzi, tunza, uongozi na karama za Roho Mtakatifu. Ni wajibu wa Maaskofu kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, ili wote kwa pamoja waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Bwana Eugenio Scalfari katika mahojiano maalum na Baba Mtakatifu Francisko anakiri kuguswa sana na unyenyekevu pamoja na mtindo wa maisha wa Baba Mtakatifu Francisko, kiongozi ambaye anaendelea kuwa kweli ni sauti ya wanyonge, maskini, wakimbizi na wahamiaji! Ni kiongozi anateseka kuona viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wakishikamana kwa ajili ya kulinda na kutetea masilahi yao binafsi badala ya kusimama kidete kulinda na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni