0

Kardinali Christoph Schonborn, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema,  Mtandao wa Wabunge Wakatoliki Kimataifa ulianzishwa kunako mwaka 2010, ili kuwawezesha wabunge kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao katika masuala ya kisiasa kama waamini wa Kanisa Katoliki. Papa Mstaafu Benedikto XVI na sasa Baba Mtakatifu Francisko, daima wamewatia shime, ili kuweza kukabiliana na changamoto katika mabunge ya nchi zao kwa kujikita katika imani na Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Tangu mwanzo kabisa wa kuundwa kwa mtandao huu, anasema Kardinali Christoph Schonborn, wamejitahidi kupembua kwa kina na mapana: dhuluma na nyanyaso za Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kuonesha upendo na mshikamano unaofumbatwa katika huduma makini kwa Wakristo wanaoteswa, wanaonyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mwaka huu, kuna wajumbe wengi kutoka Kenya, Uganda, Zimbabwe na Malawi. Mikutano ya namna hii, imekuwa ni nafasi ya kuweza pia kubadilishana: mawazo, uzoefu na mang’amuzi katika medani ya kisiasa kitaifa na kimataifa.
Kardinali Christoph Schonborn anakaza kusema, ni fursa pia ya kujenga umoja, urafiki na udugu; kwa kuimarishana katika imani, matumaini na mapendo. Ni fursa ya kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kusali Rozari kwa pamoja, ambayo kimsingi ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi. Ni wakati muafaka pia wa kushiriki kikamilifu katika maisha ya Kisakramenti. Wajumbe hawa, wanasaidiwa na mabingwa waliobobea katika nyanja mbali mbali za maisha, ili waweze kutekeleza vyema utume wao.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top