______
MWANZO
Zab. 119:137, 124
Ee Bwana, wewe ndiwe mwenye haki, na hukumu zako ni za adili. Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako.
________
SOMO I
Eze. 33:7-9
Basi wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu. Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 95:1-2, 6-9 (K) 7-8
(K) Ingekuwa heri leo tusikie sauti yake!
Tusifanye migumu mioyo yetu.
Njoni tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele yake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)
Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)
Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba;
Kama siku ile ya Masa jangwani,
Hapo waliponijaribu baba zetu;
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)
________
SOMO 2
Rum. 13:8-10
Msiwiwe na mtu chochote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sharia. Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani, na ikiwapo amri nyingine yoyote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya, basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
________
SHANGILIO
Yn. 14:23
Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu;
Na baba yangu atampenda; Nasi tutakuja kwake.
Aleluya.
________
INJILI
Mt. 18:15-20
Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo. La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru. Amin, nawaambieni, yoyote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yoyote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.
Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lolote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.
Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni