0
PAROKO wa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Kalmeli jimboni Morogoro Padri Vivian Menezes, amewaasa mapadri nchini kushika njia ya utakatifu na kuthamini masakramenti ya Kanisa ikiwa ni pamoja na kuadhimisha misa takatifu ili kuokoa waamini wenye kiu ya kukutana na Mwenyezi Mungu. 
Padri Menezes amesema kuwa kazi kubwa ambayo amepewa padri na Mwenyezi Mungu ni kuokoa roho za watu kupitia kiti cha maungamo, hivyo mapadri wana jukumu la kuwasaidia na kuwahudumia waamini kiroho, kwa furaha hata kama wapo katika hali ya uchovu, ili waweze kupata tuzo mbinguni mara baada ya kutekeleza vyema wajibu wao ndani ya Kanisa kupitia waamini wao.
Padri Menezes amesema hayo katika mahojiano maalum na gazeti hili, kufuatia kumbukumbu yake ya kutimiza miaka 15 ya upadri, akielezea furaha yake katika safari hiyo ndefu ya utume.
Amesema kuwa maisha ya padri bila kuzingatia muda wa sala hawezi kufurahia wito wake, kiasi kwamba inakuwa rahisi kupotea katika vishawishi vya dunia, mojawapo  ikiwa ni kukata tamaa mapema kwa changamoto zinazoweza kujitokeza, daima mapadri humaliza changamoto zao kwa sala pekee.
Padri Menezes ameeleza kuwa mapadri wanaalikwa kuishi maisha ya ufukara na usafi kamili hasa kuepuka kutumia pesa za waamini nje ya matarajio kwa kufanya maendeleo binafsi ambayo yanaleta kasoro katika utumishi na viapo vyao.
Kazi mojawapo ya padri katika parokia ni kuhakikisha anaweka mikakati ya kuwashirikisha waamini kuchangia maendeleo ya Kanisa kwa kujenga makanisa ili kusogeza karibu huduma za kiroho kwao badala ya kujiwekea miradi yao binafsi na kutumia vibaya pesa za waamini.
“Padri haoni uchovu katika kazi yake. Kazi ya upadri inahitaji zaidi uaminifu. Usiweke mkono wako katika sadaka za waamini na kuiba michango yao kwa maendeleo binafsi. Ukiwa padri jisikie fahari kuona maendeleo ya mahali unakofanyika kazi,” amesema padri Menezes.
Mbali na hayo ametaja baadhi ya mambo ambayo muda mwingine yamekuwa kikwazo kwa mapadri kutoka kwa waamini, mojawapo akieleza kuwa ni masengenyo dhidi ya mapadri zinapojitokeza kasoro ndogondogo, ambapo kazi ya waamini si kuwakosoa mapadri ila kuwaombea.
“Wapendwa waamini tushirikiane na mapadri, tusiwakwaze kwa makusudi, kama padre mmoja ana kasoro fulani tumuombee kwanza, mwendee kwa upole na kumueleza. Padri amepakwa mafuta ya krisma katika vitanga vya mikono yake. Mikono hiyo ni Yesu mwenyewe, usiangalie tabia zake, wala sura yake  angalia Kristo aliyejaa moyoni mwake, kwa sababu amewekwa kando padri huyu hata kama ana tabia mbaya kiasi gani,” amesema padri Menezes.
Hata hivyo kiongozi huyo wa kiroho amewashauri mapadri na jumuiya zao, kupendana katika jumuiya zao na kama kuna kasoro za mmojawapo katika shirika warekebishane kwa upendo hasa kuonyana kwa upole.
Padri Menezes alipata daraja takatifu la upadri Desemba 28 mwaka 2002 ambapo wakati wote wa utume ndani ya Kanisa amefanikiwa kuzikabili changamoto mbalimbali ambazo zimeimarisha wito wake ikiwa ni pamoja na kusimamia ahadi zake na kushirikiana na waamini kiroho kuboresha maendeleo ya Kanisa

Chapisha Maoni

 
Top