0

Na Angela Kibwana, Morogoro
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude amewaonya baadhi ya wazazi wenye tabia ya kuwaacha watoto kutazama luninga kwa muda mrefu wakiwa peke yao hasa picha zisizofaa kwani zimekuwa chanzo cha uvunjifu wa maadili. 
Askofu Mkude amesema kuwa wazazi wanapaswa kuweka ratiba maalum kwa watoto wao hasa kupanga muda maalum wa kuweka vipindi vyenye tija ndani ya familia zao, hususani  kuelimisha kuliko kuwaacha watoto kutazama picha zinazopotosha maadili na kuathiri ukuaji wao.
Askofu Mkude amesema hayo katika mazungumzo maalumu mara baada ya misa takatifu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Patris jimboni humo, akiwaonya wazazi kuwa makini na athari zitokanazo na utandawazi na matumizi mabaya ya luninga.
Amebainisha kuwa wazazi wanapaswa kuwasadikisha na kuwafundisha watoto kwamba si kila kitu kinachoonekana katika luninga kinafaa, hivyo ni wajibu wao kutowapa uhuru watoto kwa mambo yasiyofaa.
Askofu Mkude ameeleza kuwa ili kuwasaidia watoto na matumizi ya muda mrefu katika luninga, ni vyema kila familia ikaweka ratiba maalumu ya kutazama luninga kwani kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kufuatilia maendeleo ya mtoto shuleni pamoja na kupata muda wa kuwafundisha kusali.
“Mkiwaruhusu muda wote kutazama luninga peke yao wakati ninyi mnaenda kulala mnategemea nini? Mbona mnaweka muda wa chakula mnashindwaje kusimamia hili, wasadikisheni watoto kwamba si kila kitu katika luninga kinafaa, lazima wawe na uchaguzi, lazima kuwafundisha nidhamu ya kuchagua wangali wadogo,” amesema Askofu Mkude.
Wakati huo huo, kiongozi huyo wa kiroho jimboni Morogoro amewaasa wazazi kuunda dhamira ya kila mtoto aweze kujitambua nafasi yake katika familia kuwa yeye ni nani, ambapo watoto wanapaswa kuelimishwa faida za ukweli na uwazi kadiri wanavyoendelea kukua kiroho na kimwili.
“Kuwaacha watoto kujisimamia wenyewe ni makosa katika sheria za Kanisa, nawashauri wazazi undeni dhamira ya ndani kwa watoto wenu wajijue tangu wadogo, wapeni mwongozo wa maadili, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, lakini pia anaweza kujikuza vibaya asiposimamiwa ipasavyo, lazima asimamiwe kimaadili na kufundishwa kusema ukweli, mema wayaendeleze mabaya waelekezwe,” amesema Askofu Mkude.

Chapisha Maoni

 
Top