Ekaristi
Takatifu mlo wa kipasaka unabaki kuwa ni mlo wa kipasaka lakini unaunganishwa
na Kristo mfufuka. Hivyo maumbo haya ya kawaida katika jamii ya mwanadamu yaani
mkate na divai yanainuliwa katika hali ya juu kabisa na kupata hadhi ya juu.
Hakika tunapaswa kujongea na kupokea katika hali ya uchaji mkuu, ni Yesu
mfufuka, Yesu mzima ambaye amejitoa na amekufa kwa ajili yetu. Wanafunzi wake
waliandaa mlo huo mahsusi kabisa kwa ajili ya Pasaka wakimuuliza Bwana wetu
Yesu Kristo: “Ni wapi utakapo tuende tukuandalie ule Pasaka?”.
Hakika
mlo huu wa kipasaka ni Yesu mfufuka kwani Yeye mwenyewe alisema kama
tulivyosikia katika somo la Injili “huu ni mwili wangu .... hii ni damu yangu”.
Hata baada ya ufufuko wake alidhihirisha muunganiko wa Kristo mfufuka na Kristo
kabla ya ufufuko, aliwaonesha madonda yake mikononi na miguuni na pia pia ubavu
uliotobolewa. Hapa walipata hakika ya Yeye aliyejitoa na kuteswa kwa ajili yetu
na pia hapa mlo huu wa Kipasaka unapata maana kubwa na nzito, kuwa chakula cha
wokovu wetu.
Maneno
ya Kristo Yesu wakati wa Karamu ya Mwisho yaligeuza maumbo haya ya kawaida ya
mkate na divai na kupokea hadhi ya juu kabisa. Mkate unageuka kuwa mwili wake
mtakatifu sana na Divai inageuka kuwa Damu yake iliyo azizi. Chakula hiki cha
kawaida cha kidunia kinageuka kuwa karamu ya mbinguni. Si mkate kama mkate wa
kawaida, ingawa tunaonja mkate katika ulimi wetu; si divai kama divai ya
kawaida ingawa tunaonja divai katika ulimi wetu. Ni mwili na damu ya Kristo. Ni
Kristo mzima katika maumbo ya Mkate na Divai.
Hili
ni Fumbo la imani! Kwa macho yetu hatuoni, kwa ulimi wetu hatuonji lakini kama
isemavyo mojawapo ya tungo za kale juu ya Ekaristi “hakuna hata! Ni mkate
lakini mwiliwe twakiri sote”. Hivyo kupokea elimu hiyo kubwa ya kimbingu
inahitaji msaada wa kimungu, yaani neema, na fadhila ya imani. Imani hii kuu
itatuweka katika hadhi ya kuitukuza tunu hii kubwa kabisa tuliyopewa wanadamu
iliyo ishara ya upendo na kifungo cha umoja.
Somo
la pili katika Sherehe ya leo linatuangazia juu ya nguvu ya chakula hiki cha
kimbingu ambacho kinatutakasa na dhambi zetu. Dhambi ilimtenga mwanadamu na
muumba wake. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inamtakasa mwanadamu na dhambi
zake. Neno la Mungu linatuambia kuwa sadaka ya Kristo Msalabani “itawasafisha
dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai”. Ni sadaka ya
utakakaso ambayo inamuunganisha Mungu na wanadamu, inaunganisha mbingu na
dunia. Kifo cha Kristo msalabani kinaifuta ile dhambi ya kale na kutufanya sasa
kuwa na uwezo wa kupokea ahadi ya urithi wa milele. Tunafanywa kuwa warithi
pamoja na Mwana kwa sababu tunafana naye. Kwa kula mwili wake na kuinywa damu
yake tunageuzwa nafsi zetu na kuwa kama Yeye, tukimtukuza na kumtii Mungu Baba
yetu wa mbinguni.
Somo
la kwanza linaiunganisha Sadaka hii ya Ekaristi Takatifu na matendo yetu
wanadamu. Huu ni muktadha wa maisha ya kimaadili, yaani tunaelekezwa katika
utendaji wetu kurandana kadiri ya amri na maagizo ya Mungu: “Wakasema, ‘Hayo
yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii”. Chakula hiki ni agano
tunaloliweka na Mungu la kutenda kadiri ya amri na maagizo yako. Tuulapo mwili
wake Kristo na kuinywa Damu yake tunapokea uzima wa kimungu, Kristo mwenyewe
anakuwa ndiye kanuni katika utendaji wetu kama Wakristo. Ushiriki wa chakula
hiki unaambatana na wajibu wa kimaadili, wajibu wa kutenda katika ulimengu huu
kadiri ya mwanga wa Injili. Hivi Kristo tunayempokea anakuwa si kanuni tu
lakini pia kielelezo cha maisha yetu ya kikristo.
Uwepo
huu wa daima wa Ekaristi takatifu siyo wa mapambo, si jambo ambalo linakosa
maana. Kristo anajiweka kwetu kama mlo ili tuushiriki mlo huo na kuneemeshwa
kwa chakula hiko cha mbinguni. Ekaristi Takatifu inatupatia wajibu wa
kuunganika na Kristo na kuwa ishara ya Upendo wake kwa watu wote. Tunakuwa kile
tunachokipokea. Kama vile chakula cha kawaida kinavyokuwa cha faida kwa miili
yetu kwa kutupatia nguvu na kukua kwa mwili, ndiyo chakula hiki cha kiroho
kinakuwa nguvu na kutukuza katika maisha ya kiroho. Tunaunganika na Kristo na
kufanywa kuwa yeye, yaani, tunayapokea maisha yake na kuyafanya kuwa ni maisha
yetu. Yeye anakuwa ndiye chanzo cha utendaji wetu wa kikristo, kwa kumpokea
tunafanywa kuwa vyombo vya kuisambaza habari njema ya Kristo kwa wanadamu wote.
Mwenyeheri
Mama Maria Crocifissa Curcio, ambaye alikuwa na ibada kubwa sana katika
Ekaristi Takatifu aliwaambia masista wenzake maneno haya: “Ndugu zangu nawasihi
na tena nawaambieni, upendo huu mnaouchota kila siku katika Ekaristi Takatifu
uenezeni ulimwenguni kote”.Katika desturi ya tangu kale ya sherehe hii waamini
hufanya maandamano ya Ekaristi takatifu wakiwa na lengo la kushuhudia imani yao
katika mazingira ya kawaida ya wanadamu. Kwa shangwe kubwa huku wakiimba nyimbo
nzuri na tenzi za rohoni wanambeba Kristo na katika ujasiri huo wanazunguka
mitaani kwa lengo la kumfikisha huyu aliye Mwanga wa Ulimwengu katika maisha ya
kawaida ya mwanadamu.
Tukio
hili si la kuishia tu katika shangwe za siku moja bali linapaswa kuwa ukumbusho
na kichocheo cha kumpeleka Kristo tumpokeaye kila mara katika mioyo yetu wakati
wa ibada ya Misa takatifu katika maisha yetu ya kawaida/ kumpeleka huko
majumbani mwetu, katika sehemu zetu za kazi, katika mazungumzo yetu ya kindugu
na kirafiki na mahali pengine popote. Na ndiyo maana Mwenyeheri Mama Teresa wa
Calcutta alisema kuwa yeye huabudu Ekaristi Takatifu kwa muda wa masaa 24,
yaani masaa machache mbele ya Ekaristi Takatifu Kanisani na muda mwingine
mwingi anapokuwa na wenzake na hasa anapokuwa anahudumia maskini. Yeye aliiona
sura ya Kristo katika kila mwanadamu ambaye kwa hakika ameumbwa kwa sura na
mfano wa Mungu.
Hili
linatupeleka kuunganisha fumbo hili ya Ekaristi Takatifu na Amri ya
Mapendo. Mtakatifu Augustino anatuambia maneno yafuatayo juu ya Ekaristi
Takatifu, “Ni ishara ya Umoja na kifungo cha Upendo. Sakramenti ya Ekaristi ni
Sakramenti ya Upendo. Bwana wetu Yesu Kristo anatoa fundisho la namna ambayo
upendo huo unapaswa kuwa; ni upendo wa kujitoa katika ukamilifu wote,
kujisadaka katika uhuru wako mithili ya mtumwa. Namna yake ya utumwa ni tofauti
na utumwa ulivyozoeleka. Anajitoa katika hali ya utumwa kwa uhuru wote na
Mapendo makubwa.
Anatambua
wazi kwamba Yeye ni Bwana na mwalimu wao, ni mkuu wao na kwa desturi hakupaswa
kuwaosha miguu walio chini yake. Hapa anatupatia shule kubwa sana ya namna
ambavyo tunapaswa kujitoa kuwahudumia wengine katika hali ya Upendo mkamilifu.
Siyo kuangalia nguvu zangu, mamlaka yangu, uwezo wangu n.k. bali ni kumwangalia
mwanadamu mwenzangu aliye mbele yangu na anayehitaji huduma yangu, anayekuwa na
hakika ya kupatiwa huduma hiyo kutoka kwangu.
“Tuishi
Ekaristi tunayounganishwa nayo katika Fumbo la imani, tugeuze matendo yetu yote
yawe sawa na Ekaristi, yaani mwili na damu ya Kristo; katika Ekaristi
tunampokea Kristo, na tuishi kama Kristo Bwana”. Sherehe ya leo itufanye tuwe
mashahidi wa Ekaristi katika maisha yetu ya kila siku. Leo tuupokee utume huu,
utume wa kuwa Ekaristi inayozunguka katika maisha ya kawaida ya mwanadamu,
Ekaristi ambayo inawagusa wote wenye shida: wahitaji, maskini, wajane, yatima
na wengine wote wenye mahangaiko wanaohitaji kuuonja upendo wa kimungu ambao
umeubeba moyoni mwako. Na mwisho leo pia tuwe tayari kumwona Kristo katika
nyuso ya kila mmoja wetu tunayekutana naye na kumuabudu na kumtukuza daima kwa
heshima na hadhi stahiki.
Mimi
ni Padre Joseph Mosha.
Chanzo cha habari ni
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni