0
Kabla ya kuandika makala hii niliwauliza baadhi ya watu kama kuna vikwazo vinavyowakabili katika maisha ambavyo wameshindwa kuvivuka.
Wengi walikiri kuwa wana vikwazo vinavyowasumbua na kadri miaka inavyokwenda ndivyo vikwazo vinavyozidi kuongezeka na ndiyo inavyokuwa vigumu zaidi kuvitatua.
Wale wachache waliosema hawana vikwazo walionyesha wasiwasi kuhusu hatima yao kutokana na jinsi maisha yanavyozidi kuwa magumu.
Nilipowauliza ni aina gani ya vikwazo vinavyowasumbua walitaja vingi. Baadhi vilikuwa kama vile uhaba wa pesa, mizozo ya kifamilia, mitafaruku katika ndoa, utata katika ushirikiano na jamii na changamoto zinazohusiana na maafa ya asili.
Hivi ni baadhi ya vikwazo ambavyo huwakabili na wakati mwingine wakashindwa kabisa kuvitatua. Je, wanapokwama wakate tamaa na kusubiri itokee bahati itakayoondoa vikwazo hivyo?
Hakuna muujiza wowote unaoweza kutokea ili kumnusuru mtu aliyeshindwa kupata ufumbuzi.
Hakuna muujiza wowote isipokuwa kila mtu kujijengea uwezo wa kukabiliana na vikwazo vitakavyomfika katika maisha. Maisha bora ni pamoja na kuwa na uwezo wa kukabiliana na vikwazo vinavyomkabili mtu katika maisha.
Ingawa kuna fikra mbalimbali kuhusu namna ya kutatua au kukabiliana na vikwazo, katika makala hii tunaelezea mbinu chache ambazo tunafikiri kila mtu anaweza kuzitumia.
Unyumbufu
Unyumbufu ni hali ya mtu kuwa tayari kwa hiari kubadilisha utashi au matarajio kufuatana na mazingira au hali halisi ya jambo au kitu fulani. Kuna baadhi ya vikwazo ambavyo utatuzi wake unamtaka mtu awe mnyumbufu.
Mtu ambaye ni mgumu kubadili au anataka kila jambo liende kama anavyotaka au alivyozoea hata kama hali hairuhusu hupata shida.
Anaweza kuwa na tabia mbili tofauti kwa wakati mmoja au zinazotofautiana sana kufuatana na mazingira. Mwanasaikolojia mmoja amesema kuwa mtu asiye mnyumbufu ni kama gari lisilo na gia ya kurudi nyuma.
Udadisi na ubunifu
Mbinu ya udadisi na ubunifu ndiyo maarifa kuliko zote ingawa huwa inataka uwezo mkubwa wa kiakili. Mara unapogundua kuna kikwazo kinachokukabili kwanza chunguza nini kilichotokea na sababu zilizofanya kikatokea.
Kumbuka kulielewa tatizo na sababu zake ni nusu ya hatua ya kulitatua tatizo lenyewe.
Kisha fikiria njia au mbinu kadhaa unazofikiria zinafaa kwa kulitatua tatizo au changamoto hiyo. Baada ya hapo chagua mbinu moja miongoni mwa hizo ulizozifikiria ambayo una hakika ndiyo inayofaa kuliko zote.
Njia bora ya kufanya hivyo ni kuzipima zote na kuchagua moja inayoonekana ni hafifu kidogo na kuiweka kando. Chunguza zilizobaki na kuweka kando nyingine unayoona ni hafifu kidogo.
Endelea kufanya hivyo hadi ibaki mbinu moja inayoshinda zote kwa ubora. Hiyo ndiyo itumie.
Unaweza kutumia mbinu hii vyema zaidi kwa kutumia ujuzi na uzoefu wote uliokusanya katika maisha yako yote. unaweza kutazama mbinu walizozitumia wengine katika kukabiliana na changamoto zinazofanana na zako. Hapo ndipo mtu anapolazimika kutafuta ushauri kutoka kwa watu wengine wenye uzoefu zaidi. Hata hivyo, kwa kila hali mbinu hii hutegemea ukomavu wa akili, uwezo na uzoefu alionao mtu.
Kujihami binafsi
Katika makala zangu niliwahi kueleza kuwa kila binadamu ana silika ya kujihami binafsi inayoanza tangu akiwa mtoto hadi anapokuwa mtu mzima. Mtoto mchanga asiye na uwezo kila anapokabiliwa na tatizo lolote hujihami binafsi kwa kulia. Anapolia mama yake huenda kuchunguza tatizo linalomkabili. Inaweza kuwa njaa, maumivu au amejisaidia na nguo yake imechafuka.
Mtu anaweza kuvuka vikwazo vinavyomkabili katika maisha kwa kutumia mbinu ya kujihami binafsi.
Uwezo mkubwa wa kujihami binafsi humjengea mtu dhamira thabiti katika kufanya kazi zitakazomuwezesha kukabiliana na vikwazo vinavyohusiana na upatikanaji wa chakula, mavazi na malazi.
Aidha, hulka hii humuwezesha kukabiliana na vikwazo vinavyohusiana na maadui wakuu watatu wa maisha ya binadamu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.
Pia, kuna vikwazo vingine ambavyo huweza kusababishwa na binadamu wenzake.
Hii ni kwa sababu kuna watu wengine wasio waungwana ambao huweza kuwakwaza wenzao kwa kuwafanyia vitendo visivyofaa na vinavyoudhi.
Ili kuondokana na kadhia za watu wa aina hii ni vyema kuwaepuka. Kama ni ndugu au jamaa ambaye huwezi kumkwepa tafuta mbinu itakayoleta suluhu ya salama.
Akili huria
Mbinu nyingine ya kukabiliana na vikwazo katika maisha ni kuwa na akili huria, yaani iliyo wazi kwa kupokea mawazo au fikra tofauti. Watu wasio na akili huria huwa wanalitazama tukio au jambo fulani kwa mawazo ya upande mmoja tu wanaoufikiria wao.
Watu wasio kuwa na akili huria ambao mawazo yao hufungamana na upande mmoja, hulitazama kila jambo kwa mtazamo wa ubaya au kasoro badala ya upande mzuri.
Kwa mfano anaweza kusema “maua ya waridi hayafai kupanda kwa sababu miti yake ina miba” , lakini anayelitazama ua hilo kwa upande huria ataweza kusema au la waridi ni zuri kulipanda kwa sababu lina harufu nzuri.
Unapokabiliwa na kikwazo tumia akili huru kulipima ili utazame pande zake zote mbili. Watu walio na akili isiyo huru wanapokabiliwa na jambo linalowatatiza huamua haraka kuwa ni baya na kama ni mtu pia huamua ni mbaya.
Kwa mtazamo huu huwa wameshindwa kuchukua uamuzi sahihi. Hii ni kwa sababu wenye akili zisizo huria huwa na uwezo mdogo wa ubunifu. Wale wasio na kasoro hii huwa wepesi kuchambua kikwazo kwa usahihi na kubuni njia ya kukitatua.
By Abeid Sakara


Chapisha Maoni

 
Top