0
  POMBE ni kinywaji kinachotumiwa na watu wa jinsia mbalimbali huku kinywaji hicho kikizuiliwa kuuzwa na kutumiwa kwa watoto chini ya miaka 18.
Kinywaji hiki kina madhara makubwa sana endapo kitatumiwa kwa wingi au kitatumiwa na mtu asiyestahili akiwemo mama mjamazito.

Licha ya kutoruhusiwa kwa watoto,unywaji wa  pombe kwa mama mjamzito unamadhara makubwa sana kwa mtoto aliyeko tumboni.Aliyekuwa Mratibu wa Dawati la Afya ya Uzazi na Mtoto Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Sista Mariana Sita ambaye ni muuguzi anasema kuwa wataalamu wengi wanashauri mama mjamzito kuacha pombe kabisa katika kipindi chote cha ujauzito wake.
“Pombe inaweza kuleta madhara makubwa kwa mtoto bila mama mwenyewe kuhisi madhara yake,”anasema Sista Sitta.
Sista huyo anasema kuwa madhara yanayotokana na pombe wakati wa ujauzito ni madhara ya kudumu  kwa mtoto  ambayo yatadumu katika  maisha yake yote.
Anaeleza kuwa takwimu zinaonyesha  kuwa unywaji wa pombe wakati wa ujauzito huathiri mimba  ambapo hali hii hutokea zaidi katika miezi mitatu  tangu kutungwa kwa  mimba, kipindi ambacho viungo vingi vya mwili wa mtoto hufanyika (organogenesis).

Nini kinatokea mama mjamzito anapokunywa pombe
Pombe ni sumu kwa mtoto hivyo mama anapokunywa  pombe inaingia moja kwa moja kwenye mzunguko wa damu wa mama kisha hufika kwa mtoto kwa kupitia kondo la nyuma (placenta).
Pombe  hiyo inapoingia kwenye mzunguko wa damu wa mtoto, huathiri uwezo wa mtoto kupata chakula, virutubisho na oksijeni ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya kawaida katika ubongo na viungo vingine.
Hii inaweza kuathiri ubongo wa mtoto na ukuwaji wa viungo vya mwili kwa ujumla.
Uharibifu huu unaweza kuathiri uwezo wa mtoto kujifunza na kufikiri pindi anapozaliwa hali ambayo itajionesha kwa matendo yake kama mtoto na kama mtu mzima.
Licha ya hiyo pia uwezo wa mimba kustahimili kiwango cha pombe ni mdogo mno hali ambayo huathiri ufanyikaji wa viungo na ukuaji wake kwa kiasi kikubwa.

Kiwango  cha mimba kuathirika kwa pombe
Mimba huathiriwa na unywaji wa pombe kulingana na kiwango ambacho mama mjamzito anatumia ambapo pia hutegemea mambo makuu matatu ambayo ni unywaji wa pombe,umri wa mimba na mara ngapi mjamzito anakunywa pombe.
Katika unywaji huo wa pombe yapo madhara yanayoweza kumpata mtoto aliyeko tumboni  pamoja na mimba kuharibika,mtoto kuzaliwa na uzito pungufu.
Pia mtoto anaweza kuzaliwa na ulemavu wa mbavu,mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ya mgongo.
Sista Sitta amesema kuwa pia mtoto anaweza kuzaliwa na kibiongo,vidole vilivyoundana au mtoto kuzaliwa akiwa na kichwa kidogo kuliko kawaida.
Ametaja madhara mengine kuwa ni mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ya pua,matatizo ya kutokuona mbali,matatizo ya moyo,figo,matatizo ya akili,kuzaliwa na mdomo sungura (lip palate na cleft palate) na  matatizo mengine ya kimaumbile.
Licha ya athari hizo anasema kuwa sio kila mama anayekunywa pombe wakati wa ujauzito anaweza kuzaa mtoto mwenye matatizo hayo ingawa wengi wanakuwa kwenye hatari hiyo.
Aidha mama mjamzito anapokunywa pombe viwango vya pombe hiyo huwa juu katika damu ya mtoto aliyeko tumboni na pia huathiri maini yake.
Licha ya mtoto kupata  madhara ya kudumu, kimaumbile na kiakili yanayotokana na mama kunywa pombe wakati wa ujauzito pia kuna uwezekano wa mtoto kunywa pombe pamoja na kufanya vitendo viovu katika maisha yake.
Licha ya madhara kwa mtoto pia yapo madhara mengine yatokanayo na pombe ikiwa ni pamoja na  kuathirika kwa mishipa ya fahamu mwilini.
Pia mama anayetumia pombe anaweza kuungua baadhi ya ogani za mwili hasa tumbo kutokana na pombe hizo.
Aidha upo uwezekano wa mama huyo kuchanganyikiwa na kuanza kuzungumza peke yake kutokana  na neva zake za ubongo kushindwa kumiliki mwili.
Pia mama huyo ana uwezekano mkubwa sana  wa kupoteza maisha kutokana na kunywa pombe kwani anaweza kujikwaa akadondoka,kutumbukia shimoni au sehemu yenye maji mengi na hata kugongwa na vyombo vya moto kutokana na kutokuwa na uwezo wa kujimiliki baada ya kulewa.
Aidha ogani kama tumbo,mdomo na koo vipo katika hatari kubwa ya kuathirika kutokana na kupokea pombe nyingi kila wakati mtu akinywa.
Licha ya hiyo pia ini linakuwa katika hatari kubwa ya kupoteza baadhi ya seli zake ambazo hufa kulingana na kiwango cha mama au mtu yoyete anayekunywa pombe.
Ushauri
Sista Sitta anawashauri wanawake wajawazito kuacha kutumia pombe katika kipindi chote cha ujauzito ili kuweza kuokoa maisha yao na mtoto pamoja na kupata mtoto mwenye afya njema.
Pia anawashauri manesi na wauguzi wote wanaohudumia mama wajawazito kutoa  elimu ya kutosha juu ya madhara ya kutumia pombe na vileo  vingine.
Na Liberatha Ruhikula

Chapisha Maoni

 
Top