0
Ndugu wapendwa, tuendelee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi nyingine aliyotupatia ya kusikiliza na kutafakari neno lake. Tumebahitika jumapili zilizopita kusikia ukweli juu ya ufufuko na juhudi zake Yesu kutuaminisha katika hilo. Katika somo la kwanza tunasikia habari juu ya mwisho wa sheria za mwanadamu. Kwa upande mwingine, tunapata sasa kusikia habari juu ya roho mpya ya Kristo inayoonekana katika Roho Mtakatifu kama ilivyo katika somo la injili. Yesu anatumia nafasi hii kuagana na wafuasi wake. Na hapa tunapata elekezo au mwito wa ugunduzi wa uwepo wake kati yetu na pia kugundua nguvu yake kati yetu.
Katika somo la pili tunaona kuwa katika Yerusalemu mpya zile alama za nje kama Hekalu, vitabu vitakatifu n.k havina nafasi tena. Badala yake tunaona mbinguni Mungu na Yesu Kristo wanaotawala. Hizo ndizo alama mpya hai na takatifu. Tuna ushirika nao moja kwa moja. Hakuna tena haja ya vitu vya kati. Katika Injili tunaona kuwa  Neno la Mungu, Fumbo la Utatu Mtakatifu unaishi ndani yake. Kinachofuata ni hitaji la kukamilishwa na amani ya Kristo. Mt. Francis wa Sale anasema kuishi kadiri ya roho ni kufikiri, kuzungumza na kutenda kadiri ya karama zilizo ndani ya roho na siyo kadiri ya vionjo vya kimwili.
Tunaendelea kuona kuwa katika salamu ya kuagana na wafuasi wake, Yesu anawakumbusha mambo mbalimbali na ahadi tena za mbinguni. Mwinjili Yohane anaonesha wazi kuwa Yesu anafahamu vizuri kuwa muda wake duniani umekwisha na kwa namna ya pekee hii inaonekana katika sura hii ya 14. Yesu anasema wazi kuwa yafaa kurudi kwa Baba baada ya kuwafungulia njia ya wokovu. Baba ndiye chanzo cha upendo unaookoa, Mwana anatimiza mapenzi hayo ya Mungu na Roho Mtakatifu anakuja Mwana anapohitimisha kazi ya wokovu katika ufufuko – Mdo. 2:33. Ndiyo maana Yoh. 7:39 anasema Roho hakuwepo kabla, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado. Kazi ya huyo Roho kwa wakristo ni ya ualimu, kukumbusha na kutuwezesha kupenda.
Kwa njia ya Roho huyu, uwepo wa Kristo ulimwenguni unaonekana na kuendelea.  Tunakumbuka katika jpili ya pili ya pasaka – Yoh. 20:19 – amani inahusianishwa na utukufu wa Kristo na ujio wa Kristo. Amani ni zawadi ya roho mtakatifu kama mwakilishi wa Kristo mfufuka. Huku kurudi kwa Baba kwaonesha utimilifu wa nguvu ya Mungu ya wokovu. Mungu ndiye chanzo cha wokovu huo. Sisi ni sehemu ya mpango huo wa Mungu. Upendo, roho mtakatifu na amani aliyotukabidhi Yesu ni mali yetu sasa. Mwinjili Yohane anaonesha kwa msisitizo kuliko wengine uhusiano wa Yesu na Baba. Yesu alikuwa mjumbe wa Mungu – Yoh. 3:17, alifundisha mbingu, mapenzi yake Baba – Yoh. 7:16, 5:30. Huyu Yesu anatambua ukuu wa Mungu Baba – Yoh. 14:28.
Amani (shalom) anayotoa Yesu ni zaidi ya kule kusema hakuna vita kati yetu. Shalom yamaanisha amani, utulivu, uhakika, mafanikio, utukufu. Maandiko huongea juu ya amani ya Mungu – Fil. 4:7 – na amani ya Mungu ipitayo kila ufahamu ilinde mioyo yenu  katika Kristo Yesu na huongea juu ya Mungu wa amani – Rum. 15:33 – Mungu wa amani awe nanyi nyote. Amina. Amani haimanishi tu amani atoayo Mungu bali huonesha kuwa Mungu ni amani. Hivyo sisi hatuwezi kupata amani ya kweli bila kuwa wa Mungu. Dante Alighieri anasema ‘katika mapenzi yake ipo amani yetu’.
Na kama tusomavyo katika injili  – iweni na imani kati yenu na iweni na amani nami – Yoh. 14:1 – mioyo yenu isihangaike. Mnasadiki Mungu, nisadikini mimi pia. Hii ndiyo amani ya kweli. Tunapotakiana amani tutambue kuwa tunawatakia wengine maisha mema, afya, mahusiano mazuri na Mungu, kati yetu na majirani zetu. Tunatakiana moyo uliojaa amani ya Kristo. Huu uaminifu ni mkubwa mno. Mwanadamu anakabidhiwa kazi ya Mungu ya kueneza ufalme wa Mungu, nendeni mkahubiri na kubatiza. Uwepo wa Kristo kati yetu uko kwa njia ya upendo kati ya Baba na Mwana, yaani Roho Mtakatifu. Hatuna budi kuutambua na kuushuhudia.
Rossini, Mwitaliano na mtunzi mzuri wa muziki,  alipewa zawadi ya saa nzuri toka kwa Mfalme wa Ufaransa. Aliifurahia sana zawadi hii kwa sababu ilitoka kwa mfalme. Baada ya miaka kadhaa akamwonesha rafiki yake hiyo zawadi. Yule rafiki yake akamwambia ingawa umekaa na zawadi hii kwa muda mrefu, lakini hujui thamani halisi ya hii zawadi. Rossini akashtuka sana na kutaka kujua rafiki yake alimaaninisha nini. Akaomba ampatie ile saa. Akaifungua kwa ndani na kumbe ndani ya saa kulikuwa na picha ndogo ya Rossini. Hili lilikuwa agizo la mfalme na ndiyo iliyobeba maana halisi ya ile zawadi. Yeye hakujua uwepo wa picha hiyo ndani ya zawadi hiyo ya saa. Aliifurahia zawadi kwa nje lakini uhalisia wa ndani hakuujua. Hii ikamwongezea furaha na umaana wa zawadi.
Je, sisi nasi ni kwa kiasi gani tunatambua na kuishi zawadi ya upendo na uwepo wa Mungu kati yetu. Ni kwa namna gani tunaishi maisha ya wokovu?
Tumsifu Yesu Kristo.
Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.


Chapisha Maoni

 
Top