JE, WAKATOLIKI WANABUDU SANAMU!?
Kumekuwa na tuhuma nyingi dhidi ya
sisi Wakatoliki kwamba tunaabudu sanamu. Je, tuhuma hizo zina ukweli gani!?
Amri ya kukataza ibada kwa sanamu
imewekwa wazi katika Biblia Takatifu, Kutoka 20:4-5, “Usijifanyie sanamu ya
miungu wa uongo, au kinyago chochote kilicho mbinguni, katika nchi au majini
chini ya dunia. Usiisujudie wala kuitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi Mungu,
Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.”
Sheria hiyo inapatikana pia katika
Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5:8-9: “Usijifanyie sanamu za miungu za
kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini
duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Isivisujudie wala kuvitumikia; kwa
kuwa mimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.”
Ni kutokana na vifungu hivyo vya
Maandiko Matakatifu, Waamini wa Kikatoliki wamekuwa wakituhumiwa, kushtakiwa na
kushambuliwa na baadhi ya waamini wa madhehebu mengine kwamba wanapingana na
maagizo ya Mwenyezi Mungu, yanayokataza ibada kwa sanamu. Tuhuma hizo zinakuwa
nzito zaidi, hasa zinapohusishwa na Ibada inayofanywa na Waamini Wakatoliki
siku ya Ijumaa Kuu kila mwaka.
KUNA TOFAUTI KATI YA KUABUDU NA
KUHESHIMU
Mpenzi msomaji, kuna tofauti kubwa
kati ya kuabuduna kuheshimu. Kamusi ya Kiswahili ya Maana na Matumizi, ya mwaka
1993, iliyoandikwa na SALIM K. BAKHRESSA, na kuchapishwa na OXFORD UNIVERSITY
PRESS, DAR ES SALAAM, inaeleza kuwa neno “kuabudu” maana yake ni “kuomba au
kufanya ibada”; na neno “kuheshimu” maana yake ni “kutukuza, kustahi au
kuogopa.”
Katika maana yake ya ndani,
anayeabudiwa na mwenye haki ya kuabudiwa ni Mungu peke yake.Hakuna mtu, kiumbe
wala kitu chochote kinachopaswa kuabuduiwa na chenye haki ya kuabudiwa. Mtu,
kiumbe au kitu hupewa heshima tu, tena ya kiwango maalum. Kwa mfano, Bikira
Maria, kwa sababu ya nafasi yake katika kazi ya ukombozi, anapewa heshima ya
juu kuliko watakatifu wengine. Watakatifu hao wengine hupewa heshima ya kadiri
tu, chini ya heshima ile anayopewa Bikira Maria.
KWA NINI MUNGU PEKE YAKE ANASTAHILI
KUABUDIWA?
Tumesema ni Mungu pekee yake, ndiye
anayestahili kuabudiwa, kwa sababu ndiye MUUMBA wa vitu vyote, vinavyoonekana
na visivyoonekana; ndiye anayevitawala na kuviongoza vitu vyote; ndiye mwenye
uwezo juu yetu sisi wanadamu na viumbe vingine vyote; ndiye anayejua yote;
ndiye aliye pote kwa ajili yetu; ndiye mwanzo na mwisho wa kila kitu; ndiye
mkuu na Bwana wa wote.
Aidha, tunapomwabudu Mungu, tunakiri
kwamba ndiye aliyetuumba na “ndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu na
tuko!” (Mdo.17:28). Kwa kufahamu hilo, Wakatoliki hawawezi kumwabudu mtu,
kiumbe au kitu chochote, isipokuwa Mungu tu.
MAMBO MAKUU NA MUHIMU KATIKA IBADA
YA SANAMU
Ili kufahamu vema kinachofanywa na
Wakatoliki ni vema kufuatilia na kutafakari yale wanayoyafundisha na kuyasadiki
wao wenyewe, badala ya kuwahukumu kadiri watu wengine wanavyofikiri na kusema.
Ukweli ni kwamba hakuna Ibada yoyote ya sanamu katika Kanisa Katoliki. Hilo ni
dhahiri kwa sababu ili ibada ya sanamu iwe kweli kuabudu sanamu lazima yawepo
mambo makuu na muhimu mawili: Kwanza, NIA KAMILI YA KUABUDU SANAMU INAYOHUSIKA;
Pili, KUWEPO NA IBADA YA DHATI YA
KUABUDU SANAMU. Ikitazamwa kwa makini, hayo mambo mawili yanakosekana katika
Kanisa Katoliki linapokuja suala la picha na sanamu. Kwa hiyo, Wakatoliki
hawaabudu sanamu wala picha. Kama ni hivyo, wakatoliki wanafanya nini na hizo
sanamu au picha? Wanaziheshimu tu! Tukumbuke kuwa anayemwabudu mtu, kiumbe au
kitu, ni sharti akihesabu na kukisadiki kuwa ndicho kinachomwezesha kuishi,
kujimudu na kuwa na uhai wake (Rej. Mdo.17:28).
JE, BINADAMU TUNAHITAJI SANAMU AU
PICHA?
NDIYO. Binadamu tunahitaji sananmu
au picha, tena ni jadi yetu! Kwa sababu gani tunahitaji picha maishani mwetu?
Kwa sababu katika udhaifu wetu, mara nyingi tunaweza kufikiri vema kwa kutumia
vielelezo au vichokoo vyenye kuonekana na kugusika. Kwa njia ya vielelezo
hivyo, binadamu tunaweza kuyafikia kwa urahisi mambo magumu na mafumbo yaliyo
juu ya fikra zetu za kawaida. Ndiyo maana tukiona picha au sanamu ya Yesu au
Mama Maria au Watakatifu wengine, akili zetu zinaweza kutafakari mambo
matakatifu na kupata picha ya kina cha msamaha wa dhambi na mapendo ya Mungu
kwetu wanadamu.
KWA NINI WAKATOLIKI HAWAABUDU SANAMU
AU PICHA?
Wakatolikihawaabudu sanamu kwa
sababu wanajua kwamba Mungu pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa. Kwa hiyo,
hawaziabudu sanamu au picha kwa sababu wanajua kwamba hivyo siyo Mungu. Zaidi
hayo, wanajua kwamba Mungu mwenyewe amekataza kuziabudu sanamu na picha kwani
hazina daraja la Muumba. Mungu amepiga marufuku kuzigeukia na kuzisujudia
(Law.19:4). Aidha, wameaswa kuziepuka sanamu na Ibada kwa sanamu – “Watoto
wangu, epukaneni na sanamu za miungu!” (1Yoh.5:21). Pia wakatoliki wanajua kuwa
sanamu na picha hazina uwezo wowote wa kimungu. “Mungu wetu yuko mbinguni,
hufanya yote anayotaka. Miungu yao ni fedha na dhahabu; imetengenezwa na mikono
ya wanadamu. Ina vinywa lakini haisemi. Ina macho lakini haioni. Ina masikio
lakini haisikii. Ina pua lakini hainusi. … Wote wanaoitengeneza wanafanana
nayo, kadhalika na wote wanaoitumainia. Enyi wa nyumba ya Israeli mtumainieni
Mwenyezi Mungu, yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu” (Zab.115:3-9). Pia
kuziabudu sanamu ni jambo la kidunia, ambalo haliwezi kumpeleka mtu peponi
(Rej. Isa.45:16; Isa.45:20; Gal.5:20). Kwa hiyo, Wakatoliki wanajua kuwa
kuabudu sananmu na picha ni jambo haramu kabisa mbele ya Mungu, Mwumba wao
(1Pet.4:3-4).
IBADA YA KWELI YA SANAMU INAKUWAJE?
Ibada ya kweli ya sanamu siyo rahisi
hivyo, kama baadhi ya watu wanavyodhani! Ibada ya kweli ya sanamu siyo kitu cha
mchezomchezo, kama baadhi ya watu wanavyofikiri na kusema. Ibada ya Sanamu ni
suala la kuabudu, na kuabudu siyo suala la kuwa na kitu au kikiheshimu tu, bali
ni kwenda mbali zaidi ya hapo! Hivyo kumiliki sanamu au picha, mathalani
majumbani au kanisani, hakusemi lolote juu ya uwepo wa ibada ya sanamu kwa wale
wanaohusika nazo. Kwa hiyo, ikiwa watu hawazipi sanamu au picha hizo mahali pa
Mungu wa kweli, basi hawana hatia yoyote.
Jambo muhimu hapa ni kwamba wamiliki
wa sanamu au picha hizo wanaziheshimu tu huku wakijua kuwa wenyewe
wanaowakilishwa na sanamu au picha hizo hawapo pale kwa hali halisi. Katika
maana hiyo, inakuwa sahihi kabisa kuziheshimu picha za marais, ndugu na
marafiki wetu tunaowapenda, ambao hawapo karibu nasi. Picha zao hatuzikejeli
wala hatuzibwagi chini na kuzikanyaga au kuzitia vumbi. Hatufanyi hivyo, siyo
kwa sababu tunawaabudu watu hao au vitu hivyo, bali kwa sababu tunawapenda na
kuwathamini wenyewe katika hali zao halisi.
Kwa mfano ikiwa tuna kitabu cha
picha (Album) chumbani, chenye picha 100 za ndugu, rafiki na jamaa zetu,
hatusemi tuna miungu 100 tunaowaabudu nyumbani mwetu! Vinginevyo, mambo
yangetisha sana majumbani mwetu! Wenye picha hizo hatuwaabudu kamwe, ila
tunawapa heshima tu kwa sababu tunawajali na kuwapenda. Kwa nini tusiwape
heshima hiyo, ambayo ni kitu cha bure! Ukweli huo pia unahusu Bendera ya Taifa,
Wimbo wa Taifa, nk.
JE, MUNGU ANACHUKIA KILA SANAMU NA
PICHA?
Mungu hachukii kila sanamu au picha.
Hapa inafaa ieleweke vema kwamba Mungu alipopiga marufuku sanamu katika Kitabu
cha Kut. 20:3-5 na Kumb. 5:7-10, hakupiga marufuku kila sanamu. Yeye mwenyewe
anaonesha kwamba anazichukia sanamu zinazotengenezwa kusudi zichukue nafasi
yake tu. Kama sanamu au picha hazihatarishi nafasi yake, hana maneno nazo!
Ndiyo maana, basi, baada ya kumwagiza MUSA awaambie watu wasizitengeneze sanamu
na kuziabudu kama miungu (Kut.20:4-5), alimwagiza MUSA huyo huyo azitengeneze
sanamu zisizokuwa hatari, ambazo hazikupewa daraja la Mungu. Mungu alimwagiza
MUSA kutengeneza sanamu katika nafasi mbili:
(i) Musa anaagizwa atengeneze sanamu
mbili za Makerubi azibandike kwenye Sanduku la Agano wakifunike kiti chake cha
rehema. “Utatengeneza pia mfano wa viumbe hai viwili kwa kufua dhahabu, uwaweke
kwenye miisho miwili ya kiti hicho; kiumbe kimoja mwisho mmoja na kiumbe
mwingine mwisho mwingine. Waweke viumbe hao kwenye miisho ya hicho kiti, lakini
wawe kitu kimoja na hicho kiti. Viumbe hao wataelekeana, mabawa yaoyamekunjuka
kukifunika kiti cha rehema, nyuso zao zitakielekea kiti hicho” (Kut.25:18-20;
Rejea pia Ebr.9:5).
(ii) Mungu alimwagiza pia Musa
atengeneze Nyoka wa Shaba kama dawa kwa wale ambao waling’atwa na nyoka wa moto
kule Jangwani. Musa alielezwa wazi kwamba wale ambao wangemtazama huyo nyoka wa
shaba kwa imani kwa Mungu wa Israeli wangepona.“Ndipo naye Mwenyezi Mungu
akamwambia Musa: Tengeneza Nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu
yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona. Basi,
Musa akatengeneza nyoka wa shaba, akamtundika juu ya mlingoti. Kila mtu
aliyeumwa na nyoka alipomtazama huyo nyoka wa shaba, alipona” (Hes. 21:8-9;
Rejea pia Yoh.3:14-15).
Basi, Musa alitekeleza maagizo hayo
ya Mwenyezi Mungu, naye alifurahia. Kwa maagizo hayo mawili ni dhahiri kwamba
Mungu hachukii kila sanamu au picha. Mungu anachukizwa na sanamu zile ambazo
zimekusudiwa kuchukua daraja la umungu wake, maana ni yeye tu ndiye
anayestahili kuabudiwa. Yule nyoka wa shaba alikuwa dawa kwa wale walioumwa na
nyoka wa moto. Watu hao hawakumwabudu nyoka wa shaba, lakini walipona, siyo kwa
sababu ya nguvu zake, ila kwa nguvu za mwokozi zilizokuwa nyuma yake. “Kama mtu
akiitazama alama hiyo aliponywa, lakini kilichomponya siyo hicho kitu
alichokiona, bali wewe uliye Mwokozi wa watu wote” (Hek.16:7).
Hapa ni vifungu vingine vya Maandiko
Matakarifu, vinavyoonesha kuwa Mungu hachukii kila sanamu au picha.
1Fal. 7:29 “kulikuwa na sanamu za
simba, mafahali na viumbe vyenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali
zilikuwa, zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuri”.
2Nyak.3:10 “Alitengeneza sanamu
mbili za viumbe wenye mabawa kwa mbao, akazifunika kwa dhahabu na kuziweka
mahali patakatifu sana”
Ezek.41:17-18 “… kwenye ukumbi
palikuwepo na michoro iliyofanana na mitende na picha za viumbe vyenye mabawa.
Kila baada ya mtende kulichorwa picha ya kiumbe chenye mabawa kukizunguka
chumba chote”.
Yoh. 3:14-15 “Kama vile Musa
alivyomwinua yule nyoka wa shaba kule Jangwani, naye Mwana wa mtu atainuiliwa
juu vivyo hivyo, ili kila anayemwamini awe na uhai wa milele.”
Ebr.9:5 “Juu ya hilo sanduku
kulikuwa na viumbe wenye mabawa, na mabawa yao yalitanda juu ya mahali ambapo
dhambi huondolewa”
UBAYA WA SANAMU AU PICHA UKO WAPI?
Ubaya wa sanamu au picha upo katika
kuzipa sanamu au picha daraja la Mungu. Hatari na ubaya wa sanamu au picha vimo
katika kitendo cha binadamu kuzipa sanamu au picha hizo daraja la Mwenyezi
Mungu. Kama sanamu au picha hazipewi daraja la Mungu, haziwi hatari na wala
hazina ubaya wowote mbele ya Mungu. Kwa sababu hiyo, basi, mtu anaweza kuwa na
sanamu au picha ndani ya nyumba yake au kanisani, lakini bila kumkasirisha
Mungu.
Zaidi ya hayo, Mungu mwenyewe anajua
fika kuwa sanamu au picha fulani imepewa daraja lake au siyo. Kwa nini Mungu
akasirike pale ambapo sanamu au picha haziingilii daraja na ukuu wake? Mungu
mjinga wa aina hiyo hayupo! Mungu wa kweli hawezi kukasirikia picha na sanamu
ambazo zinaheshimiwa tu, na wala haziabudiwi. Aidha, Mungu mwenye haki hawezi
kumwadhibu na kumtupa Jehanamu mtu ambaye anamiliki picha au sanamu duniani
lakini bila kuziabudu, yaani pasipo kuzipa daraja la Mungu.
BIBLIA INAWEZA KUTUSAIDIA KUIELEWA
IBADA YA SANAMU?
Jibu ni ndiyo! Biblia inatoa maelezo
ya kina na ufafanuzi mzuri juu ya ibada ya sanamu. Tumesema hapo juu kuwa ibada
ya sanamu siyo jambo la mzaha au mchezo wa kitoto! Ni suala la kuabudu, na
kuabudu siyo tu jambo la kuwa na sanamu au picha na kuiheshimu tu. Ni zaidi ya
hapo! Kuna mambo muhimu ambayo lazima sanamu zitendewe, ndipo ihesabike kuwa ni
ibada ya sanamu.
a) Tukitaka kujua kama kitendo
fulani mbele ya sanamu ni kuabudu au sivyo, kwanza lazima iweponia thabiti ya
mtu anayehusika katika kitendo hicho kinachofanyika. Ibada inakuwa ya kuabudu
sanamu ikiwa mtu anayefanya kitendo hicho anaamini moyoni mwake kwamba hiyo
sanamu au picha inayofanyiwa kitendo hicho inachukua daraja na nafasi ya
Mwenyezi Mungu. Katika kitendo hicho, mtu anaamini kuwa sanamu au picha hiyo
ndiyo inayomwezesha kwenda, kuishi, kujimudu na kuwa na uhai wake hapa duniani.
b) Jambo la pili ni kuangalia kama
kitendo hicho kinachofanyika katika ibada hiyo ni Liturujia ya kueleweka/maalum.
Baada ya kubaini nia thabiti ya mtendaji, tunaweza kuitambua ibada ya sanamu
kwa kuangalia yale yanayofanyika mbele ya sanamu au picha kwa kufuatilia mambo
ambayo waabudu sanamu huyafanya. Mambo hayo, ambayo waabudu sanamu wanayafanya
tunaweza kuyakusanya kutoka katika Biblia yetu. Agano la Kale linaonesha kuwa
Ibada ya Kuabudu Sanamu inajumuisha mambo makuu yafuatayo:
i. Kuzitolea sadaka: za kuteketezwa:
Rej. Hos.4:13; nafaka na vyakula 2Fal.5:17.
ii. Kuzitolea ubani kwa heshima
kamili: Rej. 1Fal.11:8; Isa. 57:6; Yer.7:18.
iii. Kuzimwagia matambiko: Rejea
Isa. 57:6
iv. Kuzitolea zaka ya sehemu ya kumi
ya mapato ya mwaka ya mazao ya mashambani: Rejea Hosea 2:8
v. Kuziandika meza mbele yao: Rejea
Isa. 65:11
vi. Kuzibusu sanamu kwa kuzisujudia
kama viumbe vyenye enzi.
Rejea 1Fal. 19:18; Hos.13:2; Ayu.
31:2.
vii. Kuziinulia sanamu mikono katika
kuzisujudia: Rejea Isa.44:20
viii. Kuziangukia sanamu kifudifudi
ama kuzipigia magoti kwa kuziabudu: Rejea 1Fal.18:26,28.
ix. Kuzichezea ngoma na wakati
mwingine kujikatakata kwa visu kama kitendo cha ibada kwa sanamu: Rejea
1Fal.18:26,28.
Hayo yote yakichunguzwa kwa makini,
tutaona wazi kuwa hakuna Ibada ya kuabudu sanamu katika Kanisa Katoliki. Kwa
hiyo, shutuma kwamba Wakatoliki wanaabudu sanamu siyo za kweli, hazina msingi,
na ni uchochezi wa bure wenye lengo la kuleta mafarakano na magomvi. Jambo hilo
ni dhahiri kwa sababu Wakatoliki hawana nia thabiti ya kuabudu sanamu wanapotoa
heshima kwa sanamu au picha mbalimbali. Pili, matendo ya kiliturujia
yanayofanywa na wakatoliki katika kuheshimu sanamu hayalingani na matendo ya
kiliturujia yanayofanywa na waabudu sanamu, kamailivyoelezwa katika Biblia
Takatifu, hususan Agano la Kale. Kifupi, wakatoliki hawana nia thabiti moyoni
ya kuziabudu sanamu au picha, tena hawazifanyii liturujia yoyote sanamu au
picha walizo nazo majumbani au makanisani.
Ni wapi ambapo Kanisa Katoliki
linafanya au kuwafundisha rasmi na kuwahimiza wafuasi wake wafanye matendo hayo
tisa ya kiliturujia kwa ajili ya kuabudu sanamu? Hakuna! Kwa hiyo, Wakatoliki
hawana hatia yoyote ya kuabudu sanamu mbele ya Mungu. Kama mtu mmoja akifanya
hivyo, hilo ni shauri lake binafsi, siyo shauri au utaratibu wa Kanisa lote.
Aidha, afanyaye hivyo amepotoka peke yake, kwa sababu hajafundishwa na Kanisa
Katoliki afanye hivyo. Hilo ni kweli kwa sababu mambo binafsi, siyo mambo rasmi
ya Kanisa lote!
Kwa hiyo, tunaona wazi kwamba
Wakatoliki hawaabudu sanamu kamwe, kama inavyodaiwa na baadhi ya waamini wa
madhehebu mengine ya kikristo. Wanaotoa shutuma hizo inafaa wajiangalie kwanza
wao wenyewe, maana imeandikwa: “… mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi,
basi, kwake huwa najisi” (Rom.14:14).
JE, IJUMAA KUU WAKATOLIKI WANAABUDU
NINI?
Je, ni kweli kwamba Siku ya IJUMAA
KUU Wakatoliki wanaabudu Sanamu au Mti wa Msalaba? HAPANA! WANAMWABUDU
WOKOVU-YESU! Kiini cha utata hapa ni “NINI MAANA YA IBADA YA KUABUDU MSALABA”
inayoendeshwa siku ya Ijumaa Kuu? Madhehebu hayo yanayofanywa na Wakatoliki
Siku ya IJUMAA KUU siyo Ibada ya Kuabudu Sanamu. Labda hapa ni tatizo la lugha
au maneno yanayotumika, ndiyo yanayowachanganya watu! Hiloni kweli kwa sababu
jina la madhehebu yenyewe halisemi wazi kitu gani hasa kinanuiwa kufanywa
katika ibada hiyo.
Wengi hawajui nini hasa kinanuiwa
kufanyika siku ya Ijumaa Kuu katika “Ibada ya Kuabudu Msalaba” – jina ambalo
nimesema halitoi picha halisi ya jambo linalokusudiwa kufanyika. Mtu mwenye
akili timamu akijua kitu halisi kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu, hawezi
kusema madhehebu hayo ni Ibada ya Sanamu au kuabudu mti. Tatizo hapo ni lugha
tu inayotumika katika kuieleza ibada hiyo. Labda jina hilo lichunguzwe upya na
wataalamu wetu katika Kanisa na ikiwezekana kulirekebisha ili kuondoa utata kwa
baadhi ya watu wenye uelewa mdogo, wenye wanaokwazwa nalo!
NINI HASA KINAFANYIKA SIKU YA IJUMAA
KUU?
Wanachofanya Wakatoliki Siku ya
Ijumaa Kuu niKUUHESHIMU MTI WA MSALABA na KUMWABUDU WOKOVU. WOKOVU ni nani?
WOKOVU NI YESU KRSITO BWANA WETU. Basi, kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu ni
kumwabudu WOKOVU yaani YESU KRISTO, ambaye alitundikwa msalabani. Hivyo ndivyo
anavyotangaza Kiongozi wa Ibada hiyo ya Ijumaa Kuu, pale anapotoa mwaliko kwa
waamini mara tatu, ili kila muumini ausikie na kuelewa vema: “HUU NDIO MTI WA
MSALABA, AMBAO WOKOVU WA DUNIA UMETUNDIKWA JUU YAKE, NJOONI TUUABUDU.” Waamini
wanaalikwa kiimani kuuabudu WOKOVU, na hilo ndilo linalofanyika, yaani kuuabudu
WOKOVU – YESU KRISTO. Waamini wote wanaalikwa kujongea mbele kwa imani kwenda
kumwabudu YESU. Watu wanamwabudu YESU kwa sababu WOKOVU maana yake ni YESU.
Jina YESU ambalo linatokana na Kiebrabia
“YESHUA”, maana yake “WOKOVU” (Rej. Mt.1:21;1:25; Lk.1:31). Ikiwa wokovu ni
YESU, basi Ijumaa Kuu Wakatoliki hawaabudu sanamu au mti, bali wanamwabudu YESU
KRISTO. Kwa sababu hiyo, yote yanayofanyika Siku ya Ijumaa Kuu, yanafanyika
kihalali na kwa haki kwa sababu YESU KRISTO, ambaye ni WOKOVU ni MUNGU, na
MUNGU peke yake ndiye mwenye haki na anayepaswa kuabudiwa. Ikiwa mkristo hataki
kumwabudu YESU KRISTO, aliye Mwana wa Mungu na Mungu kamili, na ambaye ameeleta
wokovu, anafanya makosa makubwa!
Basi, nasisitiza kuwa Siku ya Ijumaa
Kuu, Wakatoliki hawaabudu sanamu wala mti. Wanamwabudu WOKOVU, yaani YESU
KRISTO, Nafsi ya Pili ya MUNGU. Kutomwabudu YESU KRISTO ni sawa na kumkana
Mungu, kukana wokovu ulioletwa naye. Basi, tujiepushe na ukanaji Mungu wa aina
hiyo. Nawaalika wote Siku ya Ijumaa Kuu tufungue mioyo yetu kwa imani kubwa ili
tumwone WOKOVU aliyetundikwa msalabani, apate kuukomboa ulimwengu. Kwa imani,
wote tumsujudie YESU ili apate kutukumbuka katika Ufalme wake wa milele.
Hatimaye, niseme kwamba ingawa Mungu
ametoa amri ya kukataza sanamu na picha (Kut. 20:4-5; Kumb. 5:6-10), lakini
hachukizwi na kila sanamu au picha. Sanamu na picha ambazo hazipewi daraja la
Mungu, Yeye hazichukii, kwa sababu hazichukui nafasi yake kama Muumba. Basi,
Wakatoliki hawaendi kinyume na Biblia kwa kuziheshimu sanamu na picha zilizoko
kwenye majumba yao na makanisani.
Nimeikuta sehemu, nikimpenda,
nimependa na wewe uipate!!!
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni