Unapoimba kipande cha sentensi ya
wimbo ili kuwaelekeza waimbaji wako wanachopaswa kuimba, waachie warudie peke
yao ulichowaimbia bila ya wewe kuimba pamoja nao. Rudia hivyo walau mara tatu
hivi bila kuimba nao.
Hii itawafanya wajibidiishe
kujitegemea wenyewe, na itakupa wewe nafasi ya kuwasikia vema ili utambue
maeneo wanayohitaji msaada wako zaidi.
Na wakiishaelekezwa kuimba peke yao
mara tatu bila wewe kuimba nao, sasa imba nao maeneo yale tu uliyogundua
wanahitaji msaada zaidi. Usiimbe nao kipande chote, bali pale wanapotatizwa tu.
Hii itawasaidia wao kujiamini kuhusu
walipopapatia na kuboresha palipowatatiza. Pia inasaidia kuwahifadhia wao muda
na nguvu ya mwili na akili kwa ajili ya kipande kinachofuata.
Hakikisha
wimbo unaofundishwa unafanyiwa mazoezi katika ufunguo sahihi. Siyo vema kuanzisha wimbo bila kuzingatia umeuanzisha kwenye ufunguo gani hata wakati wa kuufundisha.
Tukumbuke kwamba ufunguo wa wimbo ni jambo lililopimwa kisayansi kujenga uimbikaji unaostahili kadiri ya wimbo ulivyotungwa.
Yapo mazoea kwamba "tunajifunzia hapa halafu wakati wa kuimba tutaimbia ufunguo sahihi".
Mazoea hayo siyo mema kwa sababu:
1. Yanalemaza mapokeo ya waimbaji kwa wimbo husika
2. Yanaharibu sauti za waimbaji kwa sababu lazima lazima kuna sauti itakayolazimika kuimba nje (juu zaidi/chini zaidi) ya kimo kinachokubalika kitaalamu kuimbwa na binadamu. Hata kama ni kwa kiwago kidogo lakini inachangia kuharibu sauti.
3. Kuna wakati sauti inayoathiriwa na hali hiyo hulazimisha kutafuta kimo kingine cha kuimbia na kusababisha kwaya moja ifanye zoezi la wimbo mmoja kwa funguo tofauti kwa wakati mmoja, jambo linaloleta kelele (noise) na mgongano wa ngazi kisauti.
Hii hupelekea akili za waimbaji kutumika kupita kiasi ili kuchagua kisichohusika ili zikikatae kinapoletwa na sikio, na kutambua kinachohusika ili zikikubali kinapoletwa na sikio.
Hivyo, waimbaji huchelewa kuelewa wanachofundishwa au hukielewa kwa makosa au wakati mwingine hawakielewi kabisa na hivyo muda wa zoezi kuwa umepotea bure.
NB: Namna bora ya kufundishia nyimbo kwenye ufunguo sahihi ni kuwa na kinanda au kifaa cha kupimia ngazi wakati wa mazoezi. Wako pia watu wachache wenye uwezo wa kupima funguo kwa usahihi kwa kichwa, lakini wakati mwingine wanaweza wasipime kwa usahihi kwa 100%.
--- Waimbaji wako wajue mtaala wa siku hiyo----
Jitahidi uwezavyo kuhakikisha wanakwaya wanataarifa ya wimbo gani au zoezi gani watakalofanya, na kwa malengo gani au matumizi gani.
Wakijua siku moja kabla au hata siku kadhaa kabla (kadiri ya mpango kazi), ni vema zaidi. Na yakifanyika mabadiliko wajulishwe sababu za mabadiliko. Hii inawaleta wao na akili zao na mioyo yao vizuri zaidi kwenye zoezi na kuimarisha ufanisi wao zoezini.
Wanakwaya siyo watoto wachanga. Siyo sahihi kuwashtukiza kama mtoto anavyoshtukizwa kuwekwa kwenye beseni ili aogeshwe hata bila kutaarifa kwamba ataoga dakika kadhaa zijazo.
Dondoo hii inawezekana kwa urahisi zaidi pale ambapo walimu wanafanya kazi kwa mpango kazi wa kiufundi wa pamoja ulio sehemu ya mpango kazi mkuu na rasmi wa kwaya.
(Leo nianze kwa kukiri kwamba mwanzoni nilikusuduia kuandika dondoo chache tu, hivyo nikazibagua na kuzianza bila kufuata mtiririko. Lakini nionavyo sasa inaweza kubidi kuandika nyingi zaidi wakati tayari nilikwishaanza bila mtiririko. Basi nitajitahidi kuurejea mtiririko pole pole kadiri ninavyosonga mbele.
Sasa na twendelee na dondoo ya leo)
.......Ipe milango ya fahamu ya waimbaji wako nafasi ya kupokea kinachohusika tu na kutoathiriwa na kisichohusika......
- Macho ya wanakwaya yanapaswa kuachwa kuuona mkono wa mwalimu ukiwaongoza na nyendo za mwili (gestures) zinazowafanya waelewe zaidi kile kinachokusudiwa kujifunza.
Siyo sahihi kwa mfano mwalimu kufundisha kwa mbwembwe mbali mbali kama vile kucheza muziki (kudansi), kupandisha pandisha suruali tumboni mara kwa mara, kutafuna tafuna, nk.
- Masikio ya waimbaji yasikie kinachohusika na ufundishwaji. Yasisikie porojo nyingi zisizo za msingi kama vile majigambo, kejeli, matusi, kufoka kila wakati, nk.
Tena, sikio kamwe lisitumike kufanya kazi ya macho kufuatilia mapigo ya wimbo yatolewayo na mwimbishaji. Hapa namaanisha kwamba wanakwaya wanapaswa kutumia macho kusoma mapigo yapimwayo na mpimishaji badala ya mpimishaji kusugua vidole (mara nyingi kidole gumba na kati) ili vitoe mlio wa kuongoza mapigo. Waimbaji wakishazoezwa hivyo hawataweza baadaye kufuata mapigo kwa kuyasoma mkononi mwa mpimishaji katika mazingira ambayo mlio wa vidole haiwezi kutumiwa, kama vile kwenye ibada ya misa.
- pua za waimbaji zisiwafanye wakafakari jambo nje ya kile wanachofundishwa. Kwa mfano, mwalimu akija zoezini anatoa harufu ya pombe au sigara (hata kama siyo pombe ya kienyeji), au anatoa harufu kali ya jasho, au soksi "zinapulizia", nk, itahamisha mawazo ya waimbaji na kuathiri zoezi husika.
Haya ni kwa uwakilishi tu, lakini muhimu milango ya fahamu ya waimbaji iachiwe uhuru wa kutosha kuzingatia zoezi lengwa.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni