MASOMO YA MISA, MEI 15,
2016
SOMO 1
Mdo. 2:1-11
Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.
Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelani, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATI KATI
Zab. 104:1, 24, 29-31, 34, (K) 30
(K) Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya upya uso wa nchi.
Au: Aleluya.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Dunia imejaa mali zako. (K)
Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wa nchi. (K)
Utukufu wa Bwana na udumu milele;
Bwana na ayafurahie matendo yake.
Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
Mimi nitamfurahia Bwana. (K)
SOMO 2
1 Kor. 12 :3b-7, 12-13
Hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.
Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Uje Roho Mtakatifu, uzienee nyoyo za waamini wako uwatie mapendo yako.
Aleluya.
INJILI
Yn. 20 :19-23
Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.
Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
[5/14, 20:03] Nyambane Maurice: “MBEGU ZA UZIMA”
Jumapili, Mei, 15, 2016.
Sherehe ya Pentekoste
Mdo 2: 1-11;
Zab, 104: 1, 24, 29-31, 34;
1 Kor 12:3-7, 12-13 au Rom 8:8-17
Yn 20:19-23 au Yn 14:15-16, 23-26
WEKA ULIMWENGU KWENYE MOTO WA MAPENDO YA MUNGU
‘Pentekoste’ ni neno la Kigiriki lenye maana ya “Hamsini”. Wakristo wanasherekea sherehe hii siku hamsini baada ya Pasaka (Mdo 2). Ikiwa ni tamaduni iliyotoka Agano la Kale, yenye maana ya “sikukuu ya mavuno” katika siku ya hamsini baada ya “Pasaka ya Wayahudi” (Kut. 23:16, Hes. 28:26-31, Kum. 16:19-21). Siku hii ilikuja kuwa muhimu kwa Wakristo kwasababu, majuma saba baada ya ufufuko wa Yesu, wakati wa sikukuu ya mavuno ya Wayahudi, Roho Mtakatifu aliwashukia wafuasi wa kwanza wa Yesu, akiwapa nguvu na uwezo wakumtangaza Kristo na kuwakusanya pamoja kama Kanisa. Kama wayahudi walivyokuwa wakitoa matunda ya mazao yao ya kwanza, wakijiandaa kwa mvua kwaajili ya mazao yajayo; wafuasi, mazao ya kwanza ya utume wa Kristo yaliyoiva, wanapokea mvua ya Roho Mtakatifu, Roho atakayewafanya wakue na kuwa mazao na mbegu kwa ajili ya vizazi vijavyo. Katika Siku hii, umoja wa watu wa Mungu kama Kanisa, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu ulianza.
Roho Mtakatifu alitumwa kama Yesu alivyo ahidi, ili kukamilisha kilele cha ufunuo wa upendo wa Mungu. Roho Mtakatifu hajiweki kwa Wayahudi peke yao, bali anafunua upendo wa Mungu usio na mipaka kwa watu wote, akileta Baraka, matunda katika nchi ambayo ilikuwa imelaaniwa kipindi cha Adamu na Eva. Lugha iliyoleta mtafaruku nakutoelewana katika mnara wa Babeli, inakuwa kiunganisho kikuu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Ukosefu wa urafiki na umoja na Mungu uliopotea katika Edeni, Roho Mtakatifu anaurudisha tena kwa kuwa na Kanisa daima.
Pentekoste tunasheherekea kazi na uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu kama waumini na Kanisa. Mungu amemimina juu yenu wote Roho Mtakatifu (Rom 8:1-11) na tunapaswa kuishi ndani ya uwepo wa nguvu ya Roho wa Mungu. Roho Mtakatifu anatusaidia kumkiri Yesu kwamba ni Bwana wetu (1 Kor 12:3), akituwezesha kumtumikia Mungu (1 Kor 12:4-11), akituunganisha pamoja kama Mwili wa Kristu (1 Kor 12:12-13), anatusaidia kusali (Rom 8:26), anatuombea ndani ya Mungu Baba (Rom 8:27). Roho Mtakatifu anatuongoza (Gal 5:25) na Roho Mtakatifu anatusaidia tuishi kama Yesu (Gal 5:22-23).
Baba Mtakatifu Fransisko anamuita Roho Mtakatifu “Upendo” unaokosekana ndani ya familia zetu na Ulimwenguni. Katika ujumbe wake wa siku hizi tuu ndani ya “Amoris Laetitia”, “Furaha ya Upendo” anamuonesha Roho Mtakatifu kama mfano halisi wa Familia za Kikristo na Kanisa.
“Upendo ndani ya familia ya Kimungu, ni Roho Mtakatifu….tunaweza kutambua upendo wa Mungu ndani ya Roho Mtakatifu….kwa njia ya Kanisa, ndoa na familia zinapokea neema za Roho Mtakatifu kutoka kwa Kristo, ili tuweze kutoa ushuhuda wa Injili ya Upendo wa Mungu.”
Baba Mtakatifu anazialika familia zote za Kikristo “kila wakati kualika usaidizi wa Roho Mtakatifu anayetakatifuza umoja wenu, ili neema zake ziweze kutawala katika kila jambo mnalokutana nalo”. Pia anasema, bila Roho Mtakatifu umoja wa familia za Kikristo hauwezekani. “hakuna hata moja kati ya haya, litakalo wezekana bila kusali kwa Roho Mtakatifu ili amimine neema zake, nguvu zake na moto wa roho, kutufanya wake, kutuongoza na kubadili mapendo yetu kwa kila hali”
Leo tunaitwa, tuweze kujali kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu binafsi, familia, jumuiya na Kanisa zima. Je sisi ni vyombo vya kazi ya Roho Mtakatifu? Je, tumekuwa wasikivu wakati Roho Mtakatifu anapotuongoza? Matunda ya Roho Mtakatifu (Upendo, furaha, Amani nk.) yanakuwa ndani mwangu? Sisi wote tunaishi ndani ya uwepo wa nguvu ya Roho Mtakatifu lakini katika viwango tofauti. Tunazuiwa na uoga wetu, dhambi zetu, Mapungufu yetu na uharibifu wetu wa kila siku unaotufanya tushindwe kuhisi uwepo wa zawadi ya Mungu ya Upendo ‘Roho Mtakatifu’. Pentekoste inatupa tena wakati wa kuhisi moto wa Roho Mtakatifu na kuuweka Ulimwengu kwenye moto wa upendo wa Mungu.
Sala: Bwana, ninaomba nipokee kwa moyo uliowazi, zawadi yako ya Roho Mtakatifu. Naomba nimruhusu aniweke kwenye moto wa mapendo yako. Amina.
By Maurice Nyambane
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni