0
Kila mwaka ifikapo tarehe 31 Mei, Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kumtembelea binamu yake Elizabeth sanjari na kufungwa mwezi wa Mei, uliotengwa maalum kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Hii ni Siku kuu ya utenzi wa Bikira Maria unaojikita katika fadhila ya kusikiliza kwa makini, kutafakari na kutenda kwa imani, mapendo na matumaini. Bikira Maria
kumtembelea Elizabeth ni tukio la imani, upendo na ambalo linatangaza utimilifu wa nyakati, kwa kuzaliwa Mkombozi wa ulimwengu anayetanguliwa na Yohane Mbatizaji.
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeth amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujifunza kujisadaka kwa ajili ya huduma ya mapendo kwa ajili ya jirani, jambo ambalo lingeweza kuleta mageuzi makubwa duniani. Bikira Maria kumtembelea Elizabeth ni tukio linalobubujika furaha inayoyajaza maisha ya watu kutokana na ujasiri wa mwanamke mwenye uwezo wa kuona, kusikia na kuguswa na mahitaji ya ndugu yake na hivyo kuwa ni chemchemi ya furaha inayowakutanisha ndugu hawa wawili. Haya ndiyo yanayosimulia na Mwinjili Luka; Injili inayobubujika furaha inayoijaza nyoyo za watu!
Baba Mtakatifu anawataka wakristo kuwa ni watu wenye nyuso za furaha na tabasamu la kukata na shoka, ujumbe unaosheheni Liturujia ya Sherehe ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeth kwa ajili ya huduma. Bikira Maria ni kielelezo cha mwanamke msikivu, anayetafakari na kutenda kwa ujasiri na haraka, kielelezo cha ujasiri na huduma; kama inavyojionesha kwa wanawake wengi wajasiri walioko ndani ya Kanisa. Hawa ni wanawake wanaosimama kidete kutoa elimu kwa watoto wao pamoja na kuhudumia wagonjwa ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Kwao huduma inakuwa ni chemchemi ya furaha.
Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria na Elizabeth wanakutana katika kisima cha furaha, kama kielelezo cha huduma makini kwa jamii, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani, jambo ambalo linaweza kuleta mabadiliko makubwa duniani. Kukutana ni sehemu ya maisha ya Kikristo yanayojikita katika huduma inayowasukuma Wakristo kutoka katika ubinafsi wao, ili kuwahudumia jirani zao kwa upendo. Mwenyezi Mungu yuko kati ya watu wake, ili kuwahudumia na kuwakutanisha katika kisima cha furaha na upendo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top