Baraza hili jipya litakuwa na
dhamana ya kuhamasisha maisha na utume wa waamini walei; litajikita katika
utume wa familia mintarafu mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu pamoja na
kusimama kidete kutetea maisha ya binadamu. Baraza hili litakuwa na Mwenyekiti
atakayesaidiwa na Katibu mkuu anayeweza kuwa hata mwamini mlei akisaidiwa na
Makatibu wakuu wasaidizi watatu ambao wote watakuwa ni waamini walei. Baraza
hili limegawanyika katika vitengo vikuu vitatu: Waamini walei; Familia pamoja
na Maisha na kila kitengo kitakuwa na katibu msaidizi.
Wajumbe wa Baraza hili ni
waamini ambao wamejipambanua katika maisha na utume wa Kanisa kutoka sehemu
mbali mbali za dunia wanaoshuhudia taswira ya Kanisa la Kiulimwengu. Litakuwa
na washauri wake na kufuata sheria zote zilizowekwa na Vatican. Baraza hili
litakuwa na dhamana ya kuandaa na kusimamia makongamano ya kimataifa kwa ajili
ya utume kwa waamini walei; litasimamia taasisi za ndoa, ukweli wa familia na
maisha ndani ya Kanisa mintarafu hali ya kibinadamu na kijamii ya waamini
walei, taasisi ya familia na maisha ya binadamu katika jamii.
Kitengo cha Walei kitakuwa na wajibu wa kuwahamasisha waamini walei katika wito na
utume wao ndani ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Kitaendelea kufanya
tafiti mbali mbali ili kukazia mafundisho ya Kanisa kuhusu waamini walei ili
watambue dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa, kila mtu kadiri ya karama zake.
Kuwajengea uwezo waamini walei ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato
wa Uinjilishaji, tayari kuyatakatifuza malimwengu. Kitengo hiki pamoja na mambo
mengine kitakuwa na dhamana ya kuwafundisha na kuwahamasisha waamini walei
kushiriki kikamilifu katika Katekesi, Liturujia, Sakramenti; shughuli za
Kimissionari na Matendo ya huruma katika juhhudi za kumwendeleza mwanadamu.
Kitengo pia kitasimamia na kuratibu Mashirika na Vyama vya Kitume vyenye hadhi
ya kimataifa.
Kitengo cha familia kitakuwa na dhamana ya kuendeleza Utume wa Familia; kulinda na
kudumisha utu na mafao ya familia kadiri ya Sakramenti ya Ndoa; kwa kulinda
haki na wajibu wao ndani ya Kanisa na katika Jamii, ili taasisi ya familia
iweze kutekeleza wajibu wake barabara. Kitakuwa na wajibu wa kusoma alama za
nyakati ili kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya familia. Kitaratibu
Mashirika na Vyama vya Kitume kwa ajili ya maisha ya ndoa na familia kitaifa na
kimataifa kwa ajili ya ustawi wa familia. Kitawajibika kusimamia mafundisho
tanzu ya Kanisa kuhusu Ndoa na Familia na kuyasambaza kwa njia ya Katekesi,
tasaufi ya ndoa na familia kama sehemu ya mwendelezo wa majiundo makini.
Kitasimamia pia ustawi na maendeleo ya watoto na kwamba, kitakuwa na uhusiano
wa moja kwa moja na Taasisi ya Papa Yohane Paulo II kwa ajili ya Ndoa na
Familia” pamoja na taasisi zote ambazo ziko chini yake.
Kitengo cha Maisha kitakuwa na
dhamana ya kulinda, kutetea na kudumisha maisha ya mwanadamu tangu anapotungwa
mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na
kuhakikisha kwamba, binadamu anapata mahitaji yake msingi katika hatua zake
mbali mbali. Kusimamia na kuratibu vyama na mashirika yanayowasaidia wanawake
na familia kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya maisha dhidi ya utamaduni
wa kifo.
Kitazingatia mafundisho tanzu
ya Kanisa kuhusu kanuni maadili mintarafu matatizo na changamoto zinazoendelea
kujitokeza katika masuala ya dawa za binadamu pamoja na haki ya maisha dhidi ya
siasa na sera zinazotishia Injili ya uhai. Kitengo hiki kitakuwa na ushirikiano
wa karibu sana na Taasisi ya Kipapa ya Maisha kuhusiana na tema zinazohusiana
na kitengo hiki kama zilivyobainishwa katika Katiba ya Majaribio ya Baraza la
Kipapa la Walei, Familia na Maisha.
Na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni