Liturujia ya Neno la Mungu,
Jumapili ya 10 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inaonesha kiini cha imani ya
Kanisa, yaani ushindi wa Mungu dhidi uchungu na kifo. Injili inaonesha
matumaini yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka ambalo kwalo Kristo Yesu
anashuhudia na kufunua Uso wa huruma ya Mungu unaowafariji wale wanaoteseka na
kuvunjika moyo, changamoto kwa waamini kuendelea kuambatana na Kristo Yesu, ili
aweze kuwaonesha nguvu ya Fumbo la Ufufuko.
Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko
kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya kuwatangaza Wenyeheri Stanislaus wa Yesu na
Maria pamoja na Sr. Maria Elizabeth Hesselblad kuwa watakatifu, Jumapili tarehe
5 Juni 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Katika mateso ya Kristo, Mwenyezi Mungu anaonesha umuhimu wa kufumbata Msalaba
kama alivyofanya Bikira Maria pale Mlimani Kalvari alipomwona Mwanaye mpendwa
akiinama kichwa na kukata roho, akajaliwa kupata neema ya matumaini dhidi ya
matumaini yote!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, hivi ndivyo ilivyokuwa kwa
watakatifu waliotangazwa na Mama Kanisa mwanzoni mwa Ibada ya Misa takatifu.
Hawa ni mashuhuda wa imani walioamwambata Kristo Yesu ambaye hatimaye,
aliwaonesha nguvu ya ufufuko wake, kama inavyojidhihirisha katika muujiza
uliotendwa na Nabii Eliya pamoja na ule wa Yesu aliyemfufua Mtoto wa mjane wa
Naini. Katika shida na mahangaiko ya binadamu, Mwenyezi Mungu anajitwalia
dhamana ya kushuhudia ukuu wake dhidi ya kifo! Kwa njia ya Sala, Nabii Eliya
alipambana na Mwenyezi Mungu, akimwomba kurudishia tena yule mtoto zawadi ya
uhai, mwishoni, Mwenyezi Mungu akaridhia ombi la Eliya na kumfufua yule kijana.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Injili inaonesha jinsi ambavyo Yesu
alivyokuwa na huruma kwa yule mwanamke wa Naini, akajitwalia dhamana ya kupambana
na mauti na hatimaye kushinda na kumrudisha yule mtoto kwa mwanamke wa Naini,
ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika maisha na utume wa
Kristo Yesu. Mtume Paulo anashuhudia akisema, katika maisha yake alikuwa ni mtu
wa hatari kabisa kwani aliwatesa na kuwadhulumu Wakristo, lakini sasa ni
shuhuda wa Injili ya Kristo, zawadi ya huruma ya Mungu iliyomwita, ikamchagua
na hatimaye, kumfunulia Mwanaye mpendwa, ili kumtangaza na kumshuhudia kati ya
Watu wa Mataifa.
Mwenyezi Mungu kwa wema na upendo wake amemfunulia Kristo Yesu
aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kwa neema hii, Paulo mtume amekuwa ni
mjumbe na shuhuda wa Injili ya Kristo. Yesu anaendelea kuwaangazia na
kushuhudia neema inayoleta maisha. Mama Kanisa anabeba dhambi za watoto wake
ili kuwatakasa na kuwarejesha tena ndani ya Kanisa wakiwa na maisha mapya. Haya
ndiyo matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.
Na watakatifu Stanislaus wa Yesu na Maria pamoja na Sr. Maria Elizabeth
Hesselblad ni mashuhuda amini wa Fumbo la Ufufuko. Hawa ndio wanaomwimbia
Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kugeuza kilio chao kuwa ni wimbo
wa sifa na shukrani, wanamshukuru kwa sababu amewanyanyua na kuwapandisha juu
kabisa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni