Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wagonjwa na walemavu kuanzia tarehe 10- 12 Juni 2016 yanaongozwa na kauli mbiu “Huduma makini kwa watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ukoma kwa kuheshimu utu wao”. Kilele cha maadhimisho haya ni Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia
saa 4:30 asubuhi kwa saa za Ulaya, ili kuwaonesha na kuwaonjesha wagonjwa na walemavu huruma na upendo wa Mungu unaoganga, unaoponya na kumkirimia mwamini amani na utulivu wa ndani.
Kongamano la kimataifa kwa ajili ya ugonjwa wa Ukoma linafanyika mjini Roma kuanzia tarehe 9-10 Juni 2016, kwa kukazia umuhimu wa kuheshimu utu wa wagonjwa wa Ukoma duniani. Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya tiba ya mwanadamu minataru ugonjwa wa Ukoma, lakini bado kuna watu wanaoendelea kuathirika kutokana na ugonjwa huu na wengi wao wako: India, Indonesia, Brazil, baadhi ya nchi za Asia na Barani Afrika ukoma bado unaendelea kutesa watu katika nchi kumi.
Waathirika wa ugonjwa huu mara nyingi wanajikuta wakitengwa na jamii na hivyo kuwa ni watu wa kutangaza tanga barabarani ili kujipatia riziki yao ya kila siku, jambo linalodhalilisha utu na heshima yao. Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wanataka kupembua na kuangalia jinsi ambavyo Kanisa katika shughuli za mikakati yake ya kichungaji linaweza bado kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza utu na heshima ya wagonjwa wa ukoma sehemu mbali mbali za dunia.
Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya linataka wagonjwa hawa waweze kuhudumiwa na hatimaye kurejeshwa tena katika jamii, ili kuendelea na maisha yao ya kila siku bila kutengwa. Kongamano hili la kimataifa linahudhuriwa na wajumbe 200 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Mambo makuu matatu yanapewa kipaumbele cha kwanza: Mosi ni kupunguza athari za ugonjwa wa Ukoma; Pili ni kuwahudumia wagonjwa wa Ukoma na familia zao na tatu ni kuwarejesha tena katika jamii.
Mabingwa wa tiba ya ugonjwa wa Ukoma wanajadili mbinu mkakati wa kuzuia, kutibu na tafiti, huu ni mwelekeo wa tiba na sayansi mintarafu ugonjwa huu. Wajumbe wanachambua pia ugonjwa wa Ukoma mintarafu haki msingi za binadamu; mchango wa Kanisa na kutoka katika dini mbali mbali. Kongamano hili ni uwanja wa kusikiliza shuhuda zinazotolewa na wadau mbali mbali ambao wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma na tiba kwa wagonjwa wa Ukoma sehemu mbali mbali za dunia.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni