Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina kuanzia tarehe 16 – 19 Juni 2016 linaadhimisha Kongamano la XI la Ekaristi Kitaifa, sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 200 tangu Argentina ilipojipatia uhuru wake. Kardinali Giovanni Battista Re, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu na Rais Mstaafu wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini anamwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika tukio hili la kihistoria.
Kongamano hili linaadhimishwa huko San Miguel de Tucuman, mahali ambapo kunako tarehe 9 Julai 1816 “Provincias Unidas del Rio de la Plata” ilipojitangazia uhuru wake kutoka kwa Wahispania na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa uundwaji wa taifa jipya la Argentina. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Yesu Kristo Bwana wa historia, tuna haja nawe: Yesu Kristo Mkate wa uzima; umoja wa watu wetu”.
Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anawatakia heri na baraka waamini wote nchini Argentina wanapoendelea kufanya tafakari ya kina tayari kuboresha upendo wao kwa Fumbo la Ekaristi takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, anawahimiza kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, linalosaidia kuimarisha imani na kurutubisha udugu na huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Baba Mtakatifu anawatakia heri na baraka waamini wote watakaoshiriki kikamilifu katika maadhimisho haya. Anawaombea ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Lujan ambaye, Baba Mtakatifu mwenyewe ana ibada kubwa kwa Mama huyu, ili yote yaanze na kuhitimishwa vyema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Argentina.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni