0
Wapendwa, kwa namna ya pekee, padre ni Kristo mwingine, "Alter Christus." Padre ufahamika kwa kile afanyacho. Kwa kinywa chake anaweza kutamka maneno ya Bwana, "mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi," Yoh 14:6. Padre ni mtumishi wa Mungu anayejitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mungu.
Licha ya sadaka hiyo, padre ni mwanadamu kama wanadamu wengine, aliyetwaliwa kati ya watu kwa mambo ya muhusuyo Mungu, "maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi, " Ebr 5:1-3.
Kama Kristo mwingine, hakuna mtu anayependwa sana na kuchukiwa sana kama Padre. Lakini Padre hubakia kuwa chumvi na mwanga wa dunia. Kuchukiwa kwa Padre ni kutokana na kuyatenda mambo yamuhusuyo Mungu yanayopingana na mambo ya ulimwengu huu. Yesu Kristo anasema,"mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu," Yoh 17:14.
Wapendwa, tusisahau kwamba Padre hata baada ya upadrisho wake anaendelea kuwa mwanadamu. Na hali ya kibinadamu ni hali ya unyonge, uchovu, kushawishika pamoja na kukata tamaa. Kumbe si halali:

1. Watu kukasirika wanapomwona Padre mnyonge kama wao.
2. Kuwadai Mapadre kuwa na akili kama malaika.
3. Kutaka upendo wao uyeyushe ugumu wa kila mkosefu au wawe na ufundi wa kutatua matatizo yote ya maisha.
Wapendwa, Padre ni upendo wa Mungu:
1. Palipo na huzuni Padre huleta furaha.
2. Pasipo na haki Padre huleta haki.
3. Kwa Vijana, Padre huwatia moyo na kuwafundisha fadhila mbalimbali.
4. Padre ni utii kwa watu wote. Na kufikika na wote.
5. Padre ni uaminifu

Ndugu yangu, wanaoteuliwa kuwa mapadre ni viumbe wanyonge wanaoshiriki unyonge wa ndugu zao. Na hii inawawezesha kuwaombea ndugu zao bila unafiki. Padre ni zawadi kwa Mungu ya watu kwa Mungu. Padre hutoa zaidi na hupokea kidogo, zaidi hulipwa chuki na minong'ono. Kwa sadaka yake Padre inabidi apate heshima. Ni mtu anayemwakilisha Kristo. Kama Mt. Francisco alivyosema, "kama ningekutana na malaika pamoja na Padre, ningeweza kumsalimia kwanza Padre, kwani Malaika ni rafiki wa Mungu, na Padre ni Mhudumu wa Mungu." Heshima ya Padre inatamkwa wazi na Bwana wetu Yesu kristo, "awasikilizaye ninyi ananisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma," Lk 10:16
Wapendwa, malaika hufuata pale Mungu alipo, lakini Mungu ufuata pale Padre alipo. Mt. Yohane Maria Viane alisema, "acha eneo na sehemu yoyote bila Padre kwa miaka ishirini, matokeo yake watu wataanza kuabudu wanyama." Padre kwa Kanisa ni zawadi kubwa kuliko zawadi zote zitolewazo.
TUWAOMBEE MAPADRE WETU, NA TULIOMBEE KANISA. 
Amina

Pd Andrew Lupondya  


Chapisha Maoni

 
Top