Yako masimulizi matatu katika Injili yahusuyo muujiza wa kufufuka
watu. Kuna kufufuliwa Lazaro (Yn 11:1-44); kufufuliwa binti wa Yairo (Mk.
5:21-43; Mt 9:18-23; Lk 8:40-56) na leo kufufuliwa kijana wa Nain. Budi
tuelewane toka mwanzo kwamba kufufuka maana yake ni kuingia katika maisha ya
milele baada ya kufa. Mtu ukishakufa huwezi kurudi tena nyuma. Mtu akirudi tena
ujue huyo hakufa bali alikuwa hali ya tepekatepeka au
mahututi, au kwa maneno mengine alikuwa ICU, huko wanakochungulia watu
wanakochungulia kifo! kisha mganga akamponya Huko siyo kumfufua bali ni kuponya
au kuhuisha yaani kumrudisha mtu katika maisha ya uzima. Kadhalika katika kesi
ya leo, mtoto anayesmwa amekufa kumbe alikuwa tepekatepeka bila
matumaini ya kupona. Hali namna hiyo walikata tamaa na kuona kuwa amekufa. Kwa
hiyo hata uponyi wake ukafasiriwa kuwa ni ushindi dhidi ya kifo. Kumbe, mfu
aina hiyo akiwa mzima anajulika kuwa amehuishwa na siyo kufufuliwa.
Leo Mwinjili Luka anatafakari kituko hicho kwa mtindo wa Katekesi
na kutuundia fundisho la msingi kwa imani juu ya ushindi dhidi ya kifo yaani
Fumbo la ufufuko. Kwa hiyo kuhuisha kwa kijana huyu siyo ushindi kamili dhidi
ya kifo, bali ni ushindi wa mpito kwani baada ya kuhuishwa kifo kiliendelea
kumwinda na kumwua mara ya pili. Kumbe ushindi kamili ni dhidi ya kifo cha
kimwili yaani kuhitimisha maisha haya na kuingia maisha mapya
yaliyozawadiwa na Mungu hayo ndiyo maisha ya uzima wa milele. Tunaalikwa kuuona
muujiza wa leo kuwa kama kichokoo kinachotuelezea jinsi Mungu anavyoyafanyia
maisha haya ya kimwili tuliyo nayo.
Tunafunguliwa pazia la Injili kwa maneno haya: “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja
uitwao Nain.” Yesu anatokea Kapernaumu alikokuwa amemponya mtumwa wa akida
mmoja. Kapernaumu ilikuwa upande wa Mashariki yapata kilometa hamsini kutoka
kijiji cha Nain kilichokuwa kusini mashariki ya kijiji cha Nazareti (Galilea).
Mji wa Nain kwa Kihebrania nipendevu au neema, jina litokanalo na hali nzuri ya hewa na ardhi yenye
rutuba na chemchemi ya maji safi. Kwa kweli Nain ilineemeka na watu wake
walineemeka, wakaishi kwa furaha na kicheko.
Mandhali hiyo ya kijiji cha Nain inaweza kulinganishwa na maisha
ya watu waliobahatika kuwa na neema, kustawi, na furaha katika miji na vijiji
vyetu; watu wanaokula kuku kwa mrija na wengine kufurajia bata! Lakini kuna
wakati furaha hiyo inaisha na mtu analia machozi kama mama huyu mjane wa Nain
na watu wote kijijini wakaungana naye kuona uchungu na kuomboleza. Huo ndiyo
ukweli wa maisha kama asemavyo mzaburi: “Watu wote
watakufa na kuwaachia wengine mali zao.” (Zab
49:10). Hapa waswsahili wakaongeza kusema, na kaburi linakuwa nyumba yao ya
kudumu!
Katika msafara wa Yesu kulikuwa na “wanafunzi wake pamoja na mkutano mkubwa” wakalikabiri
lango la kijiji cha Nain. Hapo kijijini “palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni
mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa paoja
naye.” Unaona hapa ni makutano ya misafara miwili tofauti na viongozi
wao. Msafara mmoja unaongozwa na Yesu aliye Bwana wa uzima unaingia kijijini.
Msafara mwingine unaongozwa na jeneza la mtu aliyekufa unaenda nje ya kijiji.
Kadiri ya utamaduni wa Wayahudi mazishi yalifanyika jioni linapozama jua. Hata
Yesu alizikwa jioni. Aidha makaburi yalijengwa Magharibi linakozama jua. Giza
liliwakilishwa kwa maombolezo, vilio na matanga ambayo kwa kawaida yanafanyika
usiku.
Baada ya maiti kuzikwa kulining’inizwa kitamba nje ya kaburi kama
alama kwa wapitao wanapoona kitamba waliweka jiwe hapo kaburini. Utamaduni huo
upo hadi sasa. Mawe hayo yalikuwa ni mchango wao wa kulijengelea kaburi ili
kukumbuka umaarufu wa mtu huyo na kumpa heshima stahiki. Hata vijijini ambako
bado kuna mawe, makaburi yanapambwa kwa mawe, wingi wa mawe unashuhudia pia
umaarufu wa mtu! Kutokana na kukosekana kwa mawe kutokana na uharibifu wa
mazingira, leo hii makaburi yanapambwa kwa mashada ya maua na mishumaa.
Kutokana na utamaduni huo hata Yesu anawacharua Wayahudi anapowaambia: “Ninyi mnawaua manabii halafu mnajengea
makaburi yao ili kuwatambua kuwa walikuwa maarufu na wanaofaa.”
Katika msafara wa leo mfiwa hatajwi jina, badala yake imesemwa
kwamba mfu alikuwa “ni mwana pekee
wa mamaye ambaye ni mjane.” Mama huyu analinganishwa na mama yeyote yule aliyetuzaa na
kutupatia uhai wa kibinadamu. Aidha mama huyu wa leo ni mjane yaani hana mume,
hivi hawezi kuzaa tena. Sasa tutashuhudia mambo ya ajabu pindi mama wa
mtoto pekee aliyekufa anapokutana na Yesu Bwana wa uzima aliyekuja kutangaza
Injili ya uhai, huruma na mapendo si tu kwa maneno, bali kwa njia ya ushuhuda
wa maisha yake! Sikia maneno haya!
Yesu “alipomwona mama
huyu alimwonea
huruma.” Hapa unaona nguvu ya kutazama inavyopenya hadi
moyoni. Neno la kigiriki esplanchnisthe lina
maana ya kuonea huruma yaani unaoona huruma toka ndani kabisa ya moyo wako.
Katika Injili neno hili linatokea mara kumi na mbili na linatumika kumhusu
Mungu na Yesu peke yao. Yesu anachomwa hadi moyoni anapoona hali halisi ya
machungu, maumivu na kilio cha binadamu huyu anayetaka kuyaishi maisha haya
yasiyodumu. Yesu anaionea huruma hali ya mama huyu anayewakilisha hali ya
majonzi ya mama ambaye ni ulimwengu mzima. Kifo kimempenya Yesu hadi moyoni kwa
vile ana mang’amuzi ya mateso na kifo, kwani tunasikia alimlilia Lazaro, halafu
alimzika baba yake Yosefu.
Kwa hiyo hata bila kuombwa anaingilia kati: “Akakaribia, akaligusa jeneza.” Kadiri ya utamaduni wa Wayahudi kugusa jeneza na kumgusa
mfu ni unajisi. Kwa hiyo Yesu anapogusa jeneza inaonesha kuwa sasa kifo siyo
tena najisi, tusikiogope kwani kifo ni mimba itakayozaa maisha mapya yasiyokuwa
na mwisho; ni mimba ya maisha ya uzima wa milele! Yesu anapogusa jeneza,“wale waliokuwa
wakilichukua wakasimama.” Yaani msafara uliofiwa na ulioshabikia kifo umepigwa stop usiendelee
kwenda makaburini. Kwa hiyo toka sasa makaburini yanaenda mabaki tu ya mtu na
siyo nafsi ya mtu. Kifo kinamfanya mtu aingie kwenye ukamilifu wa upendo na
umoja na Mungu.
Baada ya kusimamisha msafara, Yesu anamwelekea mfu na kusema: “Kijana nakwambia: Inuka. Kumbe
maiti ile ilikuwa inasikia sauti, kwa sababu “maiti akainuka akaketi” Hapa
kuna alama mbili za ushindi dhidi ya kifo. Kwanza kuinuka kwa mfu, yaani
kushinda nguvu zote zilizomshikilia pale penye jeneza. Pili kuketi kuonesha
ushindi dhidi ya kifo, kama malaika waliofika kwenye kaburi la Yesu
wakaliviringisha na kulikalia. Kisha kijana huyu “akaanza kusema.” Huko
kusema kunaonesha kwamba kifo hakituachi wapweke bali kinatuingiza katika
mahusiano na mawasiliano ya upendo na wengine.Kumbe ufufuko katika ulimwengu wa
Mungu ni kuingia katika hali ya maisha kamili ya mahusiano.
Kisha Yesu “akampa mama
yake” yaani, Yesu anamkabidhi mtoto huyu mpya kwa
binadamu. Mtoto huyu siyo tena binadamu mwenye maisha ya kibaolojia aliyoyazaa
mama yule, bali ni mtoto mwenye maisha mapya yaliyozawadia na Mwenyezi Mungu.
Kumbe kuanzia sasa mama huyu hatazaa tena waana wanaotolewa sadaka kwenye kifo
– kwa sababu tena ni mzane. Badala yake atakuwa mama wa watoto waliozaliwa toka
kwa Yesu na wametolewa kwa maisha ya milele. Kwa hiyo Bwana anamrudishia mwana
mpya mwenye maisha mawili ya kibaolojia na maisha ya umilele. Kumbe tukiwa na
imani kila kitu kinabadilika. Ndiyo maana, “Hofu ikawashika wote wakamtukuza Mungu”yaani, Bwana wa uzima ameshinda na ametoa zawadi ya uhai
mpya ulimwenguni.
Halafu msafara ule kwa pamoja wakasema: “Nabii mkuu ametokea kwetu, na Mungu
amewaangalia watu wake.” Mwisho kabisa sisi tunapewa ujumbe ufuatao: “Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi
wote na katika nchi zote za kandokando” maana
yake kila mmoja aliyepata mwanga wa Kristo wa kutazama kwa jicho la imani
hatima ya kifo, anaalikwa kutangaza kwa furaha matumaini ya mwanga huo. Hana
budi kutangaza kwa ndugu wote kusudi waishi kwa furaha maisha haya wakitegemea
kupata furaha ya karamu ya milele katika nyumba ya Baba.
Na Padre Alcuin Nyirend, OSB.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni