Utekelezaji wa changamoto ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni dhamana endelevu ambayo Kristo Yesu amelikabidhi Kanisa lake, lakini maisha na wito wa Kipadre unajikita kwa namna ya pekee katika dhamana ya kuinjilisha na
kutangaza Injili ya furaha kwa watu wa mataifa. Dhamana hii inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na Wakleri ambao wanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa kama wachungaji wema na watakatifu; waliopakwa mafuta matakatifu ili kuadhimisha na kugawa mafumbo ya Kanisa kwa familia ya Mungu.
Wakleri wanaitwa na kutumwa
kuwahudumia watu wa Mungu ari na moyo mkuu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wao pia waweze kuonja moyo mpendelevu wa Kristo mchungaji mwema. Upadre kwa asili ni zawadi ya Mungu kwa waja wake anaowashirikisha imani na utume wa kimissionari, ili kulinda na kuhifadhi imani ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia watu wake. Kwa namna ya pekee, Mapadre wanaitwa na Kristo ili waweze kukaa pamoja naye, kukaa pamoja na Wakristo na kuendelea kuishi duniani.
Haya ndiyo mambo makuu matatu ambayo Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri amekazia wakati alipokuwa anazungumza kwenye Kongamano la Wakleri nchini Slovenia, Alhamisi tarehe 8 Juni 2016 kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utakatifu wa Mapadre nchini humo, maarufu kama “Dies sanctificationis”. Maadhimisho haya yameongozwa na kauli mbiu “Pamoja na Kristo wachungaji kati ya watu” kwa kuwakutanisha Wakleri wote nchini Slovenia.
Ili kukuza na kudumisha wito na maisha ya Kipadre, kuna haja kwa Wakleri kujenga uhusiano wa dhati na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Wakleri watambue kwamba, daima wako katika mchakato wa majiundo endelevu na kwa yule anayedhani kwamba, amefika, huyo atambue kwamba, “ana ugonjwa wa maisha ya kiroho” kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Wakleri wajenge utamaduni wa kuchunguza dhamiri zao kwa kuangalia mahusiano yao na Mwenyezi Mungu na jinsi wanavyotekeleza dhamana na utume wao kama Wakleri.
Kardinali Stella anafafanua kwamba, Wakleri wameitwa daima kukaa pamoja na Kristo Yesu kwa ajili ya kuhudumia na kugawa mambo matakatifu, changamoto ya kuendelea kuitikia wito huu kila siku ya maisha kwa njia ya Sala za Kanisa, Ibada na uchaji katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; kwa kukimbilia mara kwa mara katika kiti cha huruma ya Mungu sanjari na kutunza useja kama zawadi na sadaka katika maisha na utume wa Kipadre. Wakleri wajenge utamaduni wa upendo na mshikamano wa kidugu kwa kuondokana na ndago za uchoyo na ubinafsi.
Wakleri wanaitwa kukaa pamoja na Kristo, ili kujenga umoja na mshikamano, kwa kuendelea kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa kutambua kwamba, umoja ni kiini cha utume wa Kanisa unaoshuhudia upendo unaomwilishwa katika huduma ya mapendo kwa jirani; huu ni upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hii ni changamoto kwa Wakleri kujenga na kudumisha umoja, ushirikiano wa shughuli za kichungaji pamoja na kushirikishana changamoto, matatizo na fursa katika maisha na utume wa Kanisa. Wakleri wazee waheshimiwe na kutunzwa kwani wao ni chemchemi ya utakatifu na utume wa Kanisa. Wakleri wajitahidi kuwa na viongozi wa maisha ya kiroho, ili wasije wakasinyaa katika maisha yao ya kiroho. Wajenge na kuimarisha udugu wa Kisakramenti, kwa kupokeana kama walivyo, kusamehe na kusahau; kwa kurekebishana kidugu ili kukuza ari na mwono wa kitume Kikanisa.
Umoja wa Wakleri katika ngazi ya kijimbo na kitaifa hauna budi kukuzwa na kuendelezwa kama njia ya kusaidiana katika uaminifu wa kipadre na kwamba, hii ni nyenzo msingi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya sanjari na sera na uhamasishaji wa miito kwani ni ushuhuda unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha, chambo kwa vijana wa kizazi kipya kukimbilia na kuambata wito na maisha ya kipadre. Kwa njia hii, wakleri wanaweza kuishi ulimwenguni pasi na kumezwa na malimwengu, kwani huko wanaweza kuonja joto ya jiwe!
Kardinali Stella amemkumbuka kwa namna ya pekee Mwenyeheri Askofu Anton Martin Slomsek, aliyekuwa shuhuda na Msamaria mwema kwa familia ya Mungu nchini Slovenia. Kiongozi aliyetoa kipaumbele cha kwanza kwa majiundo awali na endelevu kwa wakleri na waamini walei; chombo makini cha Uinjilishaji mpya, aliyethamini mchango uliotolewa na vyama vya kitume katika maisha na utume wa Kanisa, mfano wa mchungaji mwema anayeishi kati ya watu wake kwa ajili pamoja na watu wake, ili kuwapeleka mbinguni.
Wakleri wanapaswa kuwa karibu na watu wanaowangoza pamoja na kuwashirikisha katika maisha na utume wa Kanisa bila kumtenga mtu. Wawe ni sura ya Baba mwenye huruma na mapendo, wanaoguswa na shida, mahangaiko na furaha ya watu wao. Wawe ni mfano bora wa uongozi, watu wanaotambua umuhimu wa kuendeleza upendo wa Mungu unaofumbatwa katika nyoyo za watu wao. Wakleri kati ya watu wasaidie kufundisha, kufariji na kutia moyo, ili kweli watu waweze kuonja uwepo wa Mungu kati yao; yote haya yafanwe kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko!
Wakleri wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu; wanaojisadaka kwa ajili ya kuwatakatifuza na kuwaongoza watu wao; makini kwa waamini wenye shida na mahangaiko ya ndani; waoneshe ari na moyo wa kimissionari, tayari kutoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa akafa na kufufuka kwa wafu! Aoneshe huruma kwa wadhambi na wote wanaomkimbilia Mungu katika maisha yao kwa kuwoanesha ukaribu wa Mungu katika maisha yao. Waguswe kwa namna ya pekee na mahitaji ya watu wao: kiroho na kimwili, tayari kujisadaka pasi na kujibakiza ili kuwahudumia kwa ari na moyo mkuu!
Kardinali Beniamino Stella anahitimisha tafakari yake kwa Wakleri waliokuwa wanahudhuria kongamano la Wakleri kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utakatifu wa Mapadre kwa kuwakumbusha kwamba, Mapadre wanaitwa na kutumwa na Kristo kumtangaza na kumshuhudia kati ya watu wa mataifa. Wanaunda Jumuiya huduma kwa watu wa Mungu kwa kuonesha ukaribu, umoja na udugu, ili kushirikishana zawadi ya imani. Majiundo makini kwa wakleri na waamini walei yapewe kipaumbele cha pekee sanjari na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ibada na uchaji mkuu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni