0
Ratiba elekezi ya maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016, Jimbo kuu la Cravovia, Poland inayoongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao
watapata rehema” imetolewa. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuondoka kutoka Roma Jumatano tarehe 27 Julai 2016 majira ya saa 8:00 mchana na kuwasili nchini Poland saa 10:00 Jioni. Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Diplomasia na Jamii katika ujumla wake. Baadaye atamtembelea Rais wa Poland na Jioni atakutana na Baraza la Maaskofu katoliki Polandi.
Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Baraza la Maaskofu Katoliki Poland, lakini zaidi, atashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambao kwa mwaka huu, unaadhimishwa mahali alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II na Mtakatifu Faustina Kowalska, waasisi wa Ibada ya Huruma ya Mungu duniani.
Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia anasema, vijana kutoka katika nchi 194 wanatarajiwa kuhudhuria maadhimisho haya na kwamba, maandalizi ya maadhimisho yanaendelea kwa kasi ya ajabu. Vijana wanataka kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, kumsikiliza, kusali na kutembea naye katika umwilishaji wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika maisha yao yak ila siku, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa vijana wa kizazi kipya.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, yaliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II yamekuwa ni chachu ya utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Tangu wakati huo, viongozi wengi wa Kanisa wameendelea kuwekeza katika utume miongoni mwa vijana na matokeo yake ni kuongezeka kwa miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Vijana wanataka majibu katika changamoto za maisha yao ya kila siku, Kanisa linapaswa kuwaelekeza chemchemi ya majibu haya ambaye ni Kristo Yesu, njia ukweli na uzima.
Alhamisi, tarehe 28 Julai 2016, Baba Mtakatifu atatoka Balice kuelekea Jimbo kuu la Cracovia, akiwa njiani atasimama kusalimiana na Watawa wa Shirika la Kutolewa Bwana Hekaluni na baadaye ataelekea kwenye Madhabahu ya Czestochowa, hapo atasali kwenye Sanamu ya Bikira Maria wa Jasna Gora na baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland. Baada ya maadhimisho haya, jioni atashiriki katika mapokezi ya vijana watakaokuwa wanashiriki katika maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani kwenye Uwanja wa Jordan, huko Blonia, Jimbo kuu la Cracovia.
Ijuamaa, tarehe 29 Julai 2016  asubuhi, Baba Mtakatifu atatembelea Kambi ya mateso ya Auschwitz na Kambi ya Birkenau na hapo atahutubia wananchi. Jioni, Baba Mtakatifu atatembelea Hospitali ya Watoto ya Chuo Kikuu, huko Prokocim, Cracovia.  Jioni, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Njia ya Msalaba pamoja na vijana kwenye Uwanja wa Jordan pamoja na kutoa tafakari.
Jumamosi, tarehe 30 Julai 2016, Baba Mtakatifu atatembelea Madhabahu ya Huruma ya Mungu Jimbo kuu la Cracovia, atapitia Lango la huruma ya Mungu na kuungamisha baadhi ya vijana watakaokuwa wamejiandaa kupokea huruma ya Mungu. Saa 4:30 ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Wakleri, Watawa, Majandokasisi na Wanovisi kutoka Poland kwenye Madhabahu ya Mtakatifu Yohane Paulo II Jimbo kuu la Cracovia na hapo atahubiri. Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana pamoja na baadhi ya vijana kwenye Makao Makuu ya Askofu wa Jimbo kuu la Cracovia. Jioni, Baba Mtakatifu atashiriki mkesha wa sala pamoja na vijana kwenye Uwanja wa Huruma ya Mungu pamoja na kuwamegea Neno.
Jumapili tarehe 31 Julai 2016, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwenye Uwanja wa Huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu atahubiri na baada kusali Sala ya Malaika wa Bwana wakati wa mchana. Jioni atakutana na kuzungumza na vijana watakaojitolea katika huduma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani,  Kamati ya Maandalizi pamoja na wafadhili. Jioni, atafunga vilago na kurejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha pamoja na utume wake. Kama kawa, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega ili kukujuza yale yatakayokuwa yanajiri wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Cracovia, nchini Poland.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

    Chapisha Maoni

     
    Top