0
Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali ya treni mbili za abiria kugongana uso kwa uso huko Kusini mwa Italia na kusababisha zaidi ya watu 27 kupoteza maisha na wengine wengi kupata majereha.  Ajali hii imetokea Jumanne tarehe 12 Julai 2016 majira ya asubuhi kati ya Andria na Corato wakati wananchi wengi wakiwa wanakwenda kazini. Idadi ya watu waliofariki dunia inatarajiwa kuongezeka kwani kazi ya kuokoa imeendelea kufanywa usiku kucha.


Baba Mtakatifu katika ujumbe uliondikwa kwa niaba yake kwenda kwa Askofu mkuu Francesco Cacucci wa Jimbo kuu la Bari-Bitonto na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, anapenda kutoa salam za rambi rambi kwa wote waliofikwa na msiba huu mzito. Anawaombea majeruhi waweze kupona haraka na kurejea tena kuendelea na shughuli zao za kila siku. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anaziweka roho ya marehemu wote waliofariki kwenye ajali hii chini ya maombezi ya Bikira Maria, mfariji wa wanaoteseka. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anatoa baraka zake za kitume.
Wakati huo huo, Serikali ya Italia imetoa salam za rambi rambi kwa wote walioguswa na msiba huu mkubwa na kwamba, Serikali itawasaidia wale waliopata ajali na kuendelea kutafuta ukweli kuhusu ajali hii kwani wananchi wana haki ya kufahamu kuhusu ukweli wote. Takwimu zinaonesha kwamba, tangu mwaka 2009 hadi mwaka 2016 kumekuwepo na ajali 120 za Treni nchini Italia na kusababisha watu 74 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 300 kupata majereha. Sababu kubwa ya ajali hizi ni ukosefu wa matengenezo ya mara kwa mara ya njia ya reli hasa kusini mwa Italia.
Naye Askofu Luigi Mansi wa Jimbo Katoliki la Andria anasema wananchi wa kawaida wanatumia usafiri wa treni kwa ajili ya kwenda kazini, shuleni au katika mihangaiko mbali mbali ya maisha. Pale ajali inapotokea na watu kupoteza maisha na mali zao, jambo la msingi ni kuwaombea huruma ya Mungu pamoja na kuwahakikishia watu kwamba, Kanisa liko pamoja nao wakati wa raha, lakini zaidi wakati wa shida na maombolezo. Ni nafasi ya kufanya upembuzi wa kina ili kufahamu sababu  za ajali ili hatimaye kurekebisha kasoro hizi, kwa lengo la kulinda maisha ya watumiaji wa usafiri wa treni.
Chanzo cha habari
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top