0
Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana linasikitishwa sana na vitendo vya ukatili dhidi ya Mahakimu ambao wamepewa dhamana na Katiba kulinda, kutetea na kutekeleza utawala wa sheria, kwani vitendo hivi vinahatarisha uhuru, amani na mafungamano ya kijamii nchini Ghana. Shutuma hizi za Maaskofu zinakuja mara baada ya Kituo cha Radio cha Muntie FM kurusha matangazo yaliyokuwa yanawashambulia Mahakimu kutokana na utekelezaji wa majukumu yao. Baraza la Maaskofu linaungana na wapenda amani, huru na utawala wa sheria kulaani vitendo vya namna hii vinavyoweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Shutuma dhidi ya Mahakimu zinapaswa kushughulikia kikamilifu ili haki iweze kutendeka na amani kurejeshwa tena katika nchi. Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana linaviomba vyombo vya ulinzi na usalam kufanya uchunguzi wa kina, ili wahusika waweze kufikishwa kwenye mkondo wa sheria. Maaskofu wanaipongeza Serikali kwa kuonesha msimamo wake kwamba, itawalinda viongozi wa Serikali, Mahakama na Bunge, ili waweze kufurahia uhuru wao binafsi unaotolewa kadiri ya Katiba ya nchi.
Maaskofu Katoliki Ghana wanavitaka vyombo vya habari nchini humo kuwajibika barabara katika kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa badala ya kujikita katika mahojiano yanayoweza kusababisha mipasuko na kinzani za kijamii. Vyombo vya habari nchini Ghana vina ajenda iliyofichika inayopania kupandisha homa ya wanasiasa wakati huu Ghana inapojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu wa 2016.
Maaskofu wanahawamasisha wananchi wote wa Ghana kushusha joto la uchaguzi, ili kujenga mazingira yatakayodumisha haki, amani na utulivu ili kufanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu unaopaswa kuwa wa kweli, huru na wa haki! Wanasiasa nao wanapaswa kudumisha amani na utulivu, umoja, udugu na uzalendo kwa nchi yao kwa kutambua kwamba siasa ni wito na dhamana ya huduma kwa wananchi na wala si vinginevyo! Baraza la maaskofu Katoliki Ghana linawahamasisha wananchi wote kujifunga kibwebwe kudumisha misingi ya haki, amani na umoja wa kitaifa, ili Ghana iweze kusonga mbele katika ustawi na maendeleo kwa watu wake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top