Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukwimwi duniani kwa kutoa huduma za kurefusha maisha pamoja na kuwasaidia waathirika wa ugonjwa Ukimwi kwa hali na mali. Tarehe 15 hadi 17 Julai 2016 kunafanyika mkutano wa kimataifa huko Durban, Afrika ya Kusini ulioandaliwa na Shirikisho la Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Mtandao dhidi ya virusi vya Ukimwi duniani pamoja na wadau mbali mbali katika mapambano haya kutoka Afrika ya Kusini.
Caritas Internationalis katika mikakati yake inaendelea kuhimiza umuhimu wa watu kupima afya zao, kupata matibabu ya magonjwa nyemelezi pamoja na kuendesha kampeni dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi. Mkutano huu umefunguliwa rasmi kwa hotuba na nasaha kutoka kwa Askofu mkuu Peter Wells, Balozi wa Vatican, Afrika ya Kusini, Kardinali Wilfred Napier, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini.
Monsinyo Robert Vitillo ni mtaalam mshauri wa Caritas Internationalis kuhusu ugonjwa wa Ukimwi. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anazungumzia kuhusu mafanikio yaliyokwisha kupatikana na mtandao wa mashirika ya kidini dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita. Kumekuwepo na majadiliano ya kina na uwazi kuhusiana na huduma ya Kanisa Katoliki katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na changamoto zake katika maisha ya watu.
Kanisa Katoliki kunako mwaka 2000 wakati wa mkutano wa Ugonjwa wa Ukimwi uliofanyika mjini Durban, Afrika ya Kusini liliitaka Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na ubaguzi wa tiba kwa wagonjwa wa Ukimwi kutoka katika nchi zilizokua zinaendelea duniani. Wagonjwa kutoka katika nchi hizi walihesabiwa kuwa ni kama raia wa daraja la pili katika uwanja wa kimataifa. Huo ukawa ni mwanzo wa Mfuko wa Kimataifa dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria. Baadaye ukafuatia mpango wa Serikali ya Marekani ujulikanao kama PEPFAR, wadhamini wakuu wa mapambano ya magonjwa hayo katika nchi zenye kipato cha chini zaidi duniani.
Monsinyo Vitillo anakaza kusema, uwezekano wa kupata tiba kwa wagonjwa wa Ukimwi kutoka katika nchi changa lakini zaidi kwa wale wanaishi vijijini inaendelea kuwa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni changamoto iliyojitokeza kunako mwaka 2000 hadi sasa bado viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaendelea kukuna vichwa vyao. Kuna idadi kubwa ya wagonjwa wa Ukimwi wanaoishi vijijini ambao hawana fursa ya kupata huduma ya tiba hata kwa magonjwa nyemelezi au dawa za kurefusha maisha ikilinganishwa na wa wagonjwa wanaoishi katika nchi tajiri zaidi duniani au mijini.
Takwimu zinaonesha kwamba, walau asilimia 50% ya waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi hawajitambui na matokeo yake ni kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwa watu hawa kusambaza virusi vya ukimwi bila ya kujitambua, jambo ambalo ni hatari sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, ndiyo maana wananchi wanahamasisha kuhakikisha kwamba, wanapima afya zao, ili kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi.
Waathirika wengine ni watoto wanaoambukizwa virusi vya Ukimwi kwa njia ya kunyonya maziwa kutoka kwa akina mama walioathirika na virusi vya ugonjwa wa Ukimwi, ndiyo maana kwa sasa kuna kampeni ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama mjamzito kwenda kwa mtoto hasa pale mama zao wanaoshindwa kuendelea kutumia dawa za kurefusha maisha. Kanisa pamoja na Mashirika yake limekuwa mstari wa mbele kutoa huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi duniani hususan katika maeneo ya vijijini.
Wahudumu wa Kanisa wamekuwa wakiwapelekea waathirika huduma huko huko majumbani kwao badala ya wao kuwatafuta kwenye maofisi yao. Huduma hii inavuka ile mipaka inayogusa masuala ya kijamii na kujikita zaidi katika huduma inayomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili; kiuchumi na kijamii; kwa kuendelea kutoa msaada kwa wajane na watoto yatima. Monsinyo Vitillo anakaza kusema, Kanisa Katoliki linapenda kutoa kipaumbele cha huduma dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi kwa watoto wadogo.
Mwezi Aprili, 2016, Caritas Internationalis iliwaalika mabingwa dhidi ya virusi vya Ukimwi kutoka Umoja wa Mataifa na kutoka katika serikali mbali mbali ili kujadiliana na hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, lakini kwa kujielekeza zaidi katika huduma kwa watoto wadogo! Mkutano wa Durban unatarajiwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya huduma ya tiba kwa watoto wadogo katika nchi zinazoendelea duniani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni