0
Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 Jimbo kuu la Cracovia, Poland yanayoongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema” ni moto wa kuotea mbali kwani ni wakati wa vijana kushuhudia kwa walimwengu kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni wakati wa kuwasha moto wa Injili ya huruma miongoni mwa vijana, huku wakiwa wamemzunguka Baba Mtakatifu Francisko. Kitakuwa ni kipindi cha hija, sala, tafakari na sherehe, ili kujenga na kuimarisha mahusiano ya karibu na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake.


Waratibu wa maadhimisho haya nchini Poland wanasema, vijana wanapaswa kujiandaa kikamilifu: kiroho na kimwili, tayari kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza wakati huo. Anna Chmura, Mratibu wa Idara ya Mawasiliano Siku ya Vijana Duniani huko Poland anasema, ulinzi na usalama vinaendelea kuimarishwa, ili kuwahakikishia washiriki amani na utulivu wa ndani. Zaidi ya mahujaji millioni mbili kutoka katika mataifa 187 wanatarajiwa kushiriki huku wakisindikizwa na Makardinali 47, Maaskofu 800 na Mapadre 20, 000, matendo makuu ya Mungu.
Mkesha na kilele cha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 ni hapo tarehe 30- 31 Julai, 2016. Hapa vijana itawalazimu kutembea kwa takribani kilometa tisa hadi kwenye Uwanja wa Huruma ya Mungu. Usafiri utatolewa kwa mahujaji walemavu wapatao 2, 000 ili kuwawezesha pia kushirikiana na vijana wenzao ili kumwimbia Mungu utenzi wa sisa na shukrani kwa ajili ya utume wa Kanisa miongoni mwa vijana.
Kanisa limekuwa likishirikiana kikamilifu na Serikali ya Poland ili kuboresha miundo mbinu ya majengo na barabara ili kuweza kutoa hifadhi kwa mahujaji watakaoshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko Poland. Madaraja mapya saba yamejengwa. Kuna mahema makubwa kwa ajili ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu yamejengwa na njia za mawasiliano ya mitandao ya kijamii imeboreshwa maradufu, kwani mahali palipo na vijana pasi na mawasiliano ya uhakika ni kuwanyima raha ya kuwashirikisha wajuani wao, Injili ya furaha.
Viongozi wa Serikali wanasema, idadi ya wananchi wa Jiji la Cracovia, itaongezeka maradufu na kwamba, wamejitahidi kufanya yote wanayoweza kadiri ya mipango ya binadamu, lakini pia kwa sasa wanategemea huruma na upendo wa Mungu ili aweze kusimamia maadhimisho haya kwa njia ya ulinzi, tunza na maombezi ya Bikira Maria, nyota ya Uinjilishaji mpya. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, abariki juhudi hizi ili kweli ziwe ni sehemu ya mapilizi ya dhambi na mapungufu yao kibinadamu, tayari kuwaonesha uso wa huruma kwa njia ya Kristo Yesu.
Maadhimisho haya anasema Kardinali Kazimierz Nycz wa Jimbo kuu la Warsaw, Poland iwe ni sehemu ya mchakato wa Mama Kanisa kuimarisha huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha Imani tendaji wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Maadhimisho haya ni nyenzo muhimu sana kwa Kanisa katika mchakato wa kuimarisha utume wa Kanisa miongoni mwa vijana. Hiki ni kitalu cha miito mitakatifu ndani ya Kanisa.
Kardinali Kazimierz Nycz anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya wazazi na walezi wanasita kuwaruhusu vijana wao kujiunga katika maadhimisho makubwa kama haya huko Poland kwa kuhofia vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kusababisha hofu miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Kardinali Nycz anawataka waamini wote wenye mashaka kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kwa vikosi vya ulinzi na usalama, vinginevyo, magaidi watafanikiwa kuwajengea watu hofu ili washinwe kushiriki katika maadhimisho haya na hili ndilo lengo kuu la vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia! Waamini washinde hofu na woga kwa kujiaminisha mbele ya Mungu, mwingi wa huruma na mapendo.
Takwimu za jumla zinaonesha kwamba, hadi kufikia tarehe 30 Juni 2016 idadi kubwa ya vijana waliojiandikisha kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 walikuwa wanatoka Italia, Ufaransa, Hispania, Amerika na Brazil. Bila shaka wajumbe kutoka katika nchi za Kiafrika watakuwepo, ili waweze kuwasilimua vijana wenzao Injili ya huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika nyoyo za vijana, jeuri na matumaini ya Kanisa.
Lakini kuna idadi kubwa pia ya vijana ambao hawatajiandikisha lakini watashiriki hasa katika matukio makubwa makubwa kama vile Njia ya Msalaba, Mkesha na Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga Siku ya Vijana Duniani. Maandalizi ya maadhimisho haya yanaendelea vyema na kwamba, familia mbali mbali Jimboni Cracovia zinatarajia kutoa malazi na chakula kwa vijana laki mbili, ili kuwaonjesha ukarimu unaobubujika kutoka katika maisha ya Kikristo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CNS.

Chapisha Maoni

 
Top