Argentina! Simama na tembea! Ndiyo kauli mbiu kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina wakati wa maandamano ya kutetea Injili ya uhai na familia, yaliyofanyika Jumamosi, tarehe 2 Julai 2016 katika miji mbali mbali nchini Argentina. Lengo la maandamano haya lilikuwa ni kuwawezesha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai inayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu!
Maaskofu wanakaza kusema, wananchi wasipokuwa makini wanaweza kumezwa na utamaduni wa kifo, usioheshimu wala kuthamini utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sira na mfano wa Mungu. Watoto wana haki ya kuwa na wazazi wote wawili, yaani baba na mama watakaojisadaka kwa ajili ya malezi, makuzi na majiundo ya watoto wao kiroho na kimwili kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kanisa linatambua na kuthamini mchango wa wazazi na walezi katika kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili kwa watoto wao, kama sehemu ya mchakato wa kuunda dhamiri nyofu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina wanapinga kwa nguvu zote Protokali ya Sera la Afya inayowapatia wanawake uwezo wa kukatisha mimba kwa kutumia miundo mbinu ya ya afya inayomilikiwa na serikali a una watu binafsi, kwa kisingizio cha uhuru binafsi. Maandamano nchini Argentina yamelenga kuwatetea na kuwalinda watoto wadogo ambao wana haki ya kuishi.
Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, tarehe 2 Julai 2016 limefanya kumbu kumbu ya miaka ishirini ya matembezi kwa ajili ya kuenzi watoto pamoja na Baba Mtakatifu, ili kuonesha huruma na upendo kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Imekuwa ni nafasi ya kukusanya chakula na mavazi ili kuwasaidia watoto hao. Kwa mara ya kwanza maandamano haya yalifanyika kunako mwaka 1997 ili kuonesha umoja na upendo wa Kanisa mahalia kwa Mtakatifu Yohane Paulo II wakati ule. Maandamano haya yameendelezwa pia wakati wa uongozi wa Papa Mstaafu Benedikto XVI na sasa Baba Mtakatifu Francisko. Haya ni maandamano ambayo yamewashirikisha watoto kwa wingi, ili kufurahia zawadi ya maisha!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni