Sote kwa pamoja kwa ajili ya Bara la Ulaya “Together 4 Europe” ni hija ya umoja katika utofauti iliyoanzishwa kunako mwaka 1999 inayounganisha vyama, mashirika na makanisa yapatayo mia tatu kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya. Kwa muda wa siku mbili yaani kuanzia tarehe 1- 2 Julai 2016 wameadhimisha Kongamano la nne la “Sote kwa pamoja kwa ajili ya Bara la Ulaya”, huko Bavaria, Munich, nchini Ujerumani kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kukutana, Upatanisho na Yajayo”
Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika ujumbe wake kwa njia ya video, anawashukuru na kuwapongeza washiriki wote wa kongamano hili lililokuwa linapania kujenga na kudumisha Umoja wa Bara la Ulaya kwa kujikita katika mshikamano ndani na nje ya Bara la Ulaya, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Ulimwengu mamboleo unakabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kutokea katika historia ya mwanadamu, hivyo Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kushikamana na kufanya kazi kwa pamoja, huku wakisaidiana kwa hali na mali, hata pale kunapokuwepo kishawishi cha kuwatenganisha watu! Wakristo kwa namna ya pekee wanahamasishwa kushuhudia msingi wa umoja wa Kanisa “Koinonia”. Hapa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wanahamasishwa kushirikishana karama na mapaji ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha.
Pale ambapo mwanadamu anakumbana na vikwazo na changamoto za maisha, hapo kuna haja ya kusimama na kuanza kuangaliana kwa macho. Haya ndiyo mang’amuzi ambayo wajumbe wa Kongamano la Sote kwa pamoja kwa ajili ya Bara la Ulaya wameshirishana katika kipindi cha siku mbili huko Bavaria, Munich. Hii ndiyo changamoto iliyoko mbele ya wananchi wa Bara la Ulaya kwa wakati huu, ili kukabiliana na changamoto za maisha. Umoja na mshikamano ni chanda na pete katika kukabiliana na magumu ya maisha na kamwe watu wasikubali kushawishiwa kutengana wakati wa shida kwani madhara yake ni makubwa. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anawaalika wananchi wa Bara la Ulaya kuangaliana machoni kama ndugu, ili kwa pamoja waweze kuona utukufu wa Mungu katika maisha yao!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni