Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia anapenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha vijana wa kizazi kipya kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 yanayoongozwa na kali mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, tema muhimu sana katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II inayovaliwa njuga kwa wakati huu na Baba Mtakatifu Francisko.
Kwa muda wa miaka mitatu, familia ya Mungu nchini Poland imechakarika kufanya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, ili kuwashirisha vijana imani, matumaini, mapendo na mshikamano unaobubujika kutoka katika Injili ya huruma ya Mungu. Vijana wengi wamepata hifadhi kwa familia za Kikristo nchini Poland, hali inayoonesha umuhimu wa kukaa pamoja kama waamini ili kushirikishana utajiri wa tunu msingi za Kiinjili.
Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia ni mashuhuda wa imani, upendo, amani na mshikamano, mambo msingi katika ulimwengu mamboleo unaoonekana kutawaliwa na kinzani na mipasuko ya kijamii na ukanimungu! Familia ya Mungu nchini Poland inatumainia huruma, wema na upendo wa Mungu wakati wote wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani na wala haina wasi wasi wowote. Mwenyezi Mungu kwa maombezi ya watakatifu wake, atawalinda vijana katika maadhimisho haya.
Vijana wengi wanaohudhuria maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani hawakubahatika kumwona Mtakatifu Yohane Paulo II, lakini wamesikia makali yake katika maisha na utume wa vijana ndani ya Kanisa. Ni kiongozi ambaye aliwapenda, akawathamini na kuwatumia vijana katika maisha na utume wa Kanisa, wengi wao leo hii ni watu walioshibana na Kanisa kwa hali na mali. Kiini cha maadhimisho haya anasema Kardinali Stanislaw Dziwisz ni Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma unaofumbatwa katika Ibada ya huruma ya Mungu iliyoasisiwa na Mtakatifu Faustina Kowalska na kuendelezwa na Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati katika Jumuiya ya Kimataifa, kuna haja ya kuambata huruma ya Mungu kwa kutambua na kuheshimu: maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huruma ya Mungu ni chemchemi ya amani na utulivu wa ndani; msamaha na upatanisho wa kweli. Kumbe, ni wajibu wa vijana kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, upendo na mshikamano kati ya watu.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa walimwengu ni kuwa na huruma kama Baba wa mbinguni, kiini na msingi wa mafundisho ya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: familia ya binadamu inahamasisha kukumbatia huruma ya Mungu kwani hii haina ubaguzi wa kidini, rangi, kitamaduni au mahali anapotoka mtu!
Baba Mtakatifu Francisko anataka kuwafunda vijana wa kizazi kipya kuhusu dhana ya huruma ya Mungu kwani jina la Mungu ni huruma iliyofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu na inaendelea kumwilishwa kwa njia ya Kanisa: katika Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma kiroho na kimwili! Ndiyo maana Njia ya Msalaba wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka huu imejikita katika Vituo vya Matendo ya Huruma: kiroho na kimwili.
Pili, Baba Mtakatifu Francisko anataka kuungana na familia ya Mungu nchini Poland kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo. Hapa waamini watakumbushwa dhamana na wajibu wao waliojitwalia siku ile walipoipokea Sakramenti ya Ubatizo, wakashirikishwa: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo, dhamana wanayopaswa kuiendeleza kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji.
Viongozi wa Serikali kwa miaka kadhaa walikataa katu katu kutoa kibali kwa Mwenyeheri Paulo VI na hata Papa Yohane Paulo II kwa kuogopa moto wa Injili ambao ungewashwa na viongozi hawa wa Kanisa nchini Poland. Wachunguzi wa mambo anasema Kardinali Stanislaw walikuwa na haki kabisa, kwani “wangeisoma namba ya Kanisa”.
Baba Mtakatifu Francisko atatembelea kwenye kambi za mateso na mauaji ya kimbari, ili apate nafasi ya kulia, tayari kuendeleza mchakato wa uponyaji unaojikita katika haki, amani, msamaha na maridhiano kati ya watu. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani nchini Poland ni nafasi ya kupyaisha imani, matumaini na mapendo miongoni mwa familia ya Mungu na hata miongoni mwa vijana wenyewe kwani watarudi nchini mwao wakiwa na mang’amuzi mapya kabisa.
Kanisa Katoliki nchini Poland ni imara, lakini halina budi kuimarishwa zaidi na zaidi, ili kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu bila kigugumizi wala makunyanzi! Waamini wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Katekesi awali na endelevu ni moto wa kuotea mbali bila kusahau umuhimu wa mafundisho ya dini shuleni na kwenye taasisi za elimu, ili kuwapatia vijana wa kizazi kipya nyenzo muhimu katika mapambano ya changamoto mbali mbali za maisha ya ujana. Vijana wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za Kiinjili, Kanuni maadili na utu wema na kamwe wasiwe kama bendera kufuata upepo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni