Kwa wale waliopitia Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, bila shaka wanakumbuka baadhi ya nyimbo zilizokuwa zinawatia mori ili kupanda Mlima na kuvumilia mafunzo ya kijeshi kwa saburi na matumaini makubwa! “Moto wa waka mama, moto wawaka” Ni kati ya viitikio ninavyovinikumbusha mbali,wakati huo nikielekea kuvuna mpunga Ruvu JKT
.
Moto katika Biblia ni mojawapo ya lugha nyingi za picha zinazotisha. Picha ya moto hutumika kutokana na mwali wake unaounguza. Leo Yesu anatuletea picha ya moto anaposema: “Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi?” Ili kuelewa maana ya picha hii ya moto, hatuna budi kwanza tuangalie fasuli nyingine katika Biblia zinazozungumza juu ya moto. Picha ya moto katika Agano la kale ipo karibu mara mia tatu sabini na nane na katika Agano jipya ipo mara sabini na moja.
Picha ya kwanza ni Mungu mwenyewe ndiye anayeoneshwa kuwa ni Moto unaounguza maadui na wapinzani wake wote. Hapo Mungu analilinda na kulitetea taifa lake dhidi ya maadui. Katika nafasi nyingine unaona moto unapita kati ya vipande vya wanyama vilivyopangwa, wakati Mungu anapofanya maagano na Abrahamu. Hapo inaonesha kuwa Mungu anawajibika katika harakati za binadamu. Aidha, mnara wa moto uliosafiri na kuwaongoza Waisraeli jangwani, ikionesha kuwa Mungu yupo daima na watu wake akiwaongoza katika safari yao. Halafu mlima Sinai ulifuka moshi wakati anawapa amri zake, hapo sheria na miongozo yake ni Mungu aliye katika moto unaofuka moshi.
Halafu Nabii Yeremia alipotaka kughairi kwenda kuhubiri, Mungu alimwambia: “Nitafanya maneno yangu kama moto katika midomo yako.” aliposikia tu maneno haya ya Mungu akajisikia moyoni mwake kama moto unaowaka uliomsukuma kwenda kuhubiri. Hapo Mungu ni dhamiri inayotusukuma kuhuburi kwa matendo habari njema. Aidha katika kitabu cha Kutoka, kuna kichaka kilichokuwa kinaungua moto bila kuteketea. Musa aliyekuwa anachunga kondoo za mkwe wake Yetro alipokikaribia akasikia sauti iliyomwambia, “vua viatu vyako kwani mahali hapa unapopakaribia ni patakatifu.”
Hapo huonesha utakatifu wa uwepo wa Mungu. Halafu kuonesha kwamba picha ya moto inayowakilisha utakatifu wake haiko tena, na badala yake imebaki hali halisi hapo moto unapofifia tu ikasikika sauti iliyosema: Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Musa akafunika uso wake kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu.Kumbe hapo Mungu amejionesha na kujiwakilisha kwa njia ya Neno lake. Kumbe picha hii ya moto ni Neno na ujumbe wake unaounguza. Kwa hiyo Neno la Mungu ni moto unaounguza.
Picha ya pili ya moto ni ile inayomwonesha Mungu mwenye hasira inayowawakia na kuwaunguza waovu na wabaya (wadhambi). Mathalani moto uliounguza Sodoma na Gomora. Nabii Eliya aliagiza moto uliowaangamiza adui za taifa lake. Picha hii ya moto wa Eliya inatumika sana katika kutunga nyimbo za kiinjili wanayoita “moto wa Eliya.” Kadhalika Wafuasi wa Yesu walimtaka Bwana wao aagize moto kuwaangamiza Wasamaria waliokataa kumpokea. Katika Agano jipya, Yohane Mbatizaji alisema: “Mimi ninabatiza kwa maji, lakini ajaye anabatiza kwa Roho mtakatifu na moto.” Kadhalika mwinjili Mathayo anasema kwamba malaika watakusanya ndago na kuziunguza motoni. Kwa hiyo “moto wa Mungu” ni hasira yake itakayowawakia na kuwaangamiza watu wote wenye dhambi.
Ndugu zangu, sisi sote ni watoto wa Mungu, tulioumbwa kwa mfano wa sura yake. Endapo maneno ya Yesu “yalimaanisha moto ule wa motoni, aliposema:nami nina dhiki kama nini hata utimizwe,” hapo ni dhahiri kwamba Yesu ni katiri sana na hakufika kutukomboa. Kumbe Yesu hakumaanisha kuwaunguza watu wenye dhambi kwa sababu watenda dhambi wote ni binadamu ambao ni watoto wa Mungu. Moto aliousema Yesu hauna lengo la kuunguza watoto wa Mungu, kwa hiyo moto huo wa Yesu unayo picha nyingine tofauti.
Picha ya kwanza ya moto wa Mungu ambao Yesu anatamani uwashwe hapa duniani mapema uwezekanavyo ni moto wa Roho wake wa upendo, yaani habari njema ya Neno lake. Moto huo uliwashwa Pasaka, ukawashwa tena siku ya Pentekoste kwa wanafunzi. Moto huo ni nguvu ya roho wa Mungu inayounguza ulimwengu wa kale na kuingiza roho mpya, ya uwana wa Mungu itakayotusukuma tusitende kama wanyama bali tusukumwe na upendo. Huu ndiyo moto anaotaka uwashe mapema ulimwenguni kote, moto wa upendo wa kindugu anaposema: “nami natamani sana uzidi kuwaka.”
Picha ya pili ya moto ni ubatizo anaposema: “Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami ninadhiki kama nini hata utiizwe.” Ubatizo ni neno la kigirikibaptizzei maana yake, kuingia ndani na kubaki humo. Yesu kuingia au kutumbukia majini na kubaki humo ni picha inayowakilisha Yesu anayeingia katika maji ya mauti. Walioyaandaa maji hayo ya kifo ni maadui wake yaani maadui wa moto ule wa Mungu unaofika kuwaka duniani.
Watu hao walikuwa na hofu, wakachanganyikiwa kwa sababu moto huo ulifika kuunguza yale waliyoyahodhi. Kuchanganyikiwa na hasira inaweza kulinganishwa na ile ya mtu aliyeunguliwa moto nyumba yake nzuri na mali zake zote za thamani kubwa, au hata badala ya moto, mali hizo zimetumbuliwa. Hapo mtu huyo atakuwa na hasira kali na na kusababisha hata kudhulumu zaidi.
Kwa hiyo, hasira kali au maji waliyoandaa maadui wa Yesu ni hukumu na kifo. Lengo la maadui hao lilikuwa ni kuuzima moto huo moja kwa moja. Kabla ya maji hayajamtumbukiza na kumzomba kwa mawimbi yake, yaani kumwua, Yesu kwa hiari yake anaamua kujitumbukiza ndani ya maji kwa kifo na kubaki humo humo (kubatizwa). Hii ndiyo hatima ya mwanakondoo na maana ya ubatizo wa Yesu.
Baada ya kuelewa maana ya picha ya moto na ubatizo Yesu anasema: “Je mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano.” Tangazo hili Yesu linapingana kabisa na matangazo ya manabii wa Agano la kale waliowahuria watu wao kwamba wanamsubiri masiha aliye kama Musa, ambaye ni “Mfalme wa amani,” Katika ufalme huo mpya mwanakondoo ataishi na chui, wanyama wakali na wapole watachungwa pamoja na kujipatia malisho kwa amani.
Vyombo vya vita kama mishale, mikuki na mapanga vyote vitayeyushwa na kuwa majembe ya kulimia kwani hakutakuwa na vita tena. Lakini amani hiyo iliyotangazwa ilihusu taifa moja tu la Waisraeli nayo ingepatikana baada ya masiha mpya kuwapiga maadui zao. Kwa hiyo amani ya namna hiyo siyo amani ya kweli kwani ni ya wachache, ni sawa na ile aliyosema mwanafasihi Tacitus kwamba: ubi solituditem faciunt pacem appellant, maana yake Pale walipopafanya ukiwa (wameua watu wote na mali zao) wanapaita amani.
Kumbe, amani na haki ya Mungu ni upendo wa haki kwa watu wote. Yesu anasema waziwazi kwamba mbele ya mapendekezo ya kujenga ulimwengu mpya unaosimikwa katika misingi ya haki, amani, udugu, upendo na mshikamano mipasuko, kinzani na mafarakano ya kijamii ni mambo ya kawaida. Utengano na mgawanyo huo utaonekana pia pale wafuasi na wanafunzi watakakopeleka moto wa upendo, amani na mshikamano kati ya watu ulimwenguni kwani wataenda kupambana na maji yatakayotaka kuwazamisha kama kibatari! Lakini hayatafaulu kwa sababu “aliyetota hajui kutota”, kwa vile wafuasi wa Kristo wameingizwa na kuzamishwa katika kisima cha maji ya ubatizo.
Padre Alcuin Nyirenda OSB.
Chanzo cha habari ni http://sw.radiovaticana.va/
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni