Jumapili 4 Septemba 2016 , Papa Francisko alimtangaza Mama Tereza wa Calcutta, kuwa Mtakatifu , anayemulikia wengi walio katika giza la maisha, wengi waliokata tamaa, na waliopoteza matumaini ya kuondokana na hali ya umasikni na mateso. Na kwa sifa zake za upole , huruma na utakatifu aliyokuwa nao , na wingi wa matunda ya kiroho aliyozalisha, inawia vigumu kumwita tu Mtakatifu Tereza, lakini inakuja bila hata kufikiria kuendelea kutumia jina lililozoeleka la mama Tereza wa Calcutta, na hivyo atajulikana kama Mtakatifu Mama Tereza, Papa alieleza na kushangiliwa kwa nguvu na waliokuwa wakimsilikiza.
Papa alieleza hili wakati wa homilia yake aliyoitoa katika Ibada iliyofanyika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Vatican kwa nia ya kumtangaza kuwa Mtakatifu Mama Tereza wa Calcutta. Ibada ilihudhuriwa na umati mkubwa wa watu karibia 120,000, kutoka pande zote za dunia.
Homilia ya Papa , ililenga katika maisha ya Mtawa Mama Tereza wa Calcultta, mtu maskini aliyefariki mwaka 1997, ambaye alizamisha maisha yake kusaidia jamii iliyosahaulika na kutengwa , watu wanaoishi mitaani bila makazi, wanaodharaulika katika mitaa ya India , wakionekana kama watu wasiokuwa na faida. Juhudi za Mama Tereza , kusaidia maskini hao, ziliwatia aibu viongozi wa dunia kwa kutojali umaskini ulioundwa na wenye mamlaka. Juhudi za Mtawa huyo kwa maskini , ziligusa mioyo ya wengi , na hivyo kuona haja ya kutoa msaada kwa maskini na wanaoteseka.
Papa Francisko , alieleza na kumtangaza Mama Tereza wa Calcutta, kuwa Mtakatifu , mfano wa unaong’ara wa Kanisa linalokwenda hadi katika mipaka yote ya dunia na vitongojini , mijini na vijijini, kutoa mwanga wa injili kwa maskini na mioyo iliyojeruhiwa , mwanga wenye faraja zote.
Papa altoa mwaliko kwa wote , kulibeba tabasamu la Mama Tereza moyoni na kuonyesha tabasamu hilo kwa wengine wote wanaokutana nao katika safari ya maisha na hasa wale walio katika hali za umaskini na wanaoteswa na sababu zilizo nje ya uwezo wao. Papa amemtaja Mtakatifu Mama Teresa kuwa Mtakatifu mwenye huruma , anayetetea maisha tangu yale yasiyozaliwa bado hadi yale yanayotelekezwa mitaani.
Alisema kuwa, Mtakatifu Tereza , aliinamia wote na hasa walikuwa wameachwa kufa barabarani , aliwafariji na kuinua hadhi ya utu wao, ambayo ni zawadi ya Mungu kwa binadamu wote. Papa ameomba Mwanga wa Imani na huruma wa Mtakatifu Mama Tereza, uendelee kumulikia njia sahihi kwa watu wengi waliogubikwa na giza la maisha, hasa walipoteza matumaini ya kuwa na maisha bora . Ushuhuda wa Mama Tereza wa kuishi kwa kumtegemea Mungu , na uendelee kuwaleta wote hasa maskini wa maskini , karibu na Mungu.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni