Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika safari yake kitume nchini Malawi, kuanzia tarehe 3 - 7 Novemba, 2016 amepata nafasi ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kuzungumza na Wakleri pamoja na Watawa nchini Malawi na tarehe 5 Novemba 2016, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ametabaruku Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Jimbo Katoliki Karonga; Ibada ambayo imehudhuriwa na viongozi wa Kanisa na Serikali ya Malawi, chini ya uongozi wa Rais Arthur Peter Mutharika.
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika safari yake kitume nchini Malawi, kuanzia tarehe 3 - 7 Novemba, 2016 amepata nafasi ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kuzungumza na Wakleri pamoja na Watawa nchini Malawi na tarehe 5 Novemba 2016, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ametabaruku Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Jimbo Katoliki Karonga; Ibada ambayo imehudhuriwa na viongozi wa Kanisa na Serikali ya Malawi, chini ya uongozi wa Rais Arthur Peter Mutharika.
Baada ya Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi kutabarukiwa rasmi sasa limekuwa ni nyumba ya Mungu, Hekalu la Roho Mtakatifu, mahali pa kujenga na kudumisha umoja wa familia ya Mungu Jimboni Karonga. Hili ni kati ya majimbo machanga kabisa nchini Malawi, linaloadhimisha miaka 6 tangu kuanzishwa kwake, lakini kumekuwepo na ongezeko kubwa la Wakristo na Majandokasisi wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Kanisa kuu ni mahali ambapo Familia ya Mungu itamzunguka Askofu Mahalia kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, ili kujipatia amana ya maisha ya milele.
Kanisa kuu ni Nyumba ya Mungu, inayoonesha uwepo endelevu wa Mungu katika maisha ya watu kwa njia ya: Uaminifu, huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka hata pale waamini wanapotenda dhambi na kukengeuka katika maisha. Ibada ya kutabaruku Kanisa inawakumbusha waamini umuhimu wa kufurahia neema na baraka za Mungu katika maisha yao, ili kuweza kumpokea Mungu anayefanya hija pamoja nao. Ni changamoto kwa kila mwamini kujitakasa, ili aweze kuwa ni Hekalu takatifu la Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo Yesu, ili aweze kufahamika na kupendwa na wote.
Waamini waliozaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu katika Ubatizo na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, wanahamasishwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kwa kujikita katika imani, matumaini na mapendo. Waamini watambue kwamba, wao ni mitume wamissionari wanaotumwa Kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yenye mvuto na mashiko katika medani mbali mbali za maisha; kwa kujikita katika upendo na msamaha; tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazopaswa kumwilishwa kuanzia ndani ya familia. Waamini wa Jimbo Katoliki Karonga, wawe mstari wa mbele kushuhudia tunu msingi za Injili ya familia; kwa kufuata mfano wa Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Msimamizi wa Jimbo Katoliki Karonga.
Hili ni Kanisa ambalo limejengwa kwenye msingi thabiti ambao ni Kristo Yesu, chemchemi ya umoja, maisha, utume na mafundisho ya Kanisa. Huu ni mwaliko kwa Makanisa Mahalia kuendelea kuungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ibada ya kutabaruku Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Jimbo Katoliki Karonga, imekuwa ni sababu ya furaha kwa Familia ya Mungu nchini Malawi katika ujumla wake. Hili ni Hekalu la Roho Mtakatifu, mwaliko kwa familia ya Mungu kujikita katika uaminifu katika maisha ya ndoa na familia, katika wito na utume wa kipadre na kitawa; daima ikitoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Mwishoni mwa Ibada, Kardinali Filoni kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ameitaka Familia ya Mungu nchini Malawi, kujenga na kudumisha Jamii inayojikita katika misingi ya haki, amani na upatanisho, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji nchini humo. Jamii ya Malawi inapaswa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa utamaduni wa mshikamano; kwa kusimama kidete katika elimu bora, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na kuzisaidia familia ambazo zinakabiliwa na changamoto mbali mbali za maisha.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni