Chama cha Skauti nchini Italia, Jumapili tarehe 4 Desemba 2016 kimeadhimisha Jubilei ya miaka 100 tangu kilipoanzishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kiapapa la Utamaduni kwa kushirikiana na viongozi washauri wa Skauti. Lengo la Ibada hii ya Misa Takatifu lilikuwa ni kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hija ya maisha na utume wa Skauti nchini Italia. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu “Giorgio al Velabro”.
Imekuwa ni nafasi ya kuwakumbuka na kuwaombea wanachama na viongozi wa Skauti waliokwisha kutangulia kwenye usingizi wa milele wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na uzima wa milele! Kwa mara nyingine tena, Chama cha Skauti nchini Italia kimejiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Roho Mtakatifu ili aweze kukiongoza na Yesu aendelee kuwa ni kiongozi wao mkuu, kwa ajili ya huduma kwa watoto na vijana wanaofundwa na Chama cha Skauti Italia. Miaka 100 ya Skauti nchini Italia imesaidia kwa kiasi kikubwa majiundo ya watoto na vijana: kiutu, kiroho na kijamii na kwamba, kuna idadi kubwa sana ya wazazi wanaothamini mchango wa malezi unaotolewa na Chama cha Skauti nchini Italia na kwamba, Kanisa linawapongeza kwani wamekuwa kweli ni wanachama waaminifu na wa kweli katika mchakato wa malezi na majiundo kwa watoto na vijana nchini Italia.
Kardinali Ravasi amewapongeza wanachama wa Skauti kwa kujenga na kudumisha ari na moyo wa uvumilivu katika utekelezaji wa majukumu yao na kwamba, kwa njia hii wamejengewa ujasiri na ukakamavu katika kukabiliana na changamoto za maisha bila woga wala ukakasi katika maamuzi. Amekazia umuhimu wa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, ili liweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha.
Wanachama wa Skauti wametakiwa kujitahidi kujenga dhamiri nyofu, sauti ya Mungu inayosikika kutoka katika undani wa maisha yao, ili waweze kukua na kukomaa katika fadhila za Kikristo na utu wema. Amewataka wanachama wa Skauti nchini Italia kuendeleza mchakato wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, kwani kimsingi Skauti ni huduma ya upendo kwa jirani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni