0
Jukwaa la viongozi wa kidini nchini Uingereza limesikitishwa sana na kitendo cha kigaidi kilichofanyika Jijini London Jumatano tarehe 22 Machi 2017 na kusababisha watu 5 kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa vibaya na taarifa zinasema, kati yao 7 wamelazwa hospitalini na hali zao ni mbaya. Viongozi hawa wamelaani na kushutumu vitendo vya kigaidi vilivyotokea nchini Ubelgiji, mwaka mmoja uliopita na kusababisha watu 35 kupoteza maisha. Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales,
anawakumbuka marehemu wote waliopoteza maisha yao kutokana na shambulio hili la kigaidi sanjari na kuwaombea majeruhi waweze kupona haraka na hatimaye, kuendelea na shughuli zao. Anaungana na familia, ndugu na jamaa kwa ajili ya kuombolezea wote waliofariki dunia. Anawaomba wananchi kudumisha amani, utulivu pamoja na kuwa macho zaidi wakati huu Serikali ikiendelea kufanya uchunguzi wake

 
Jukwaa la viongozi wa Kidini nchini Uingereza linasema, dhamana ya dini zao ni kusimama kidete kulinda na kudumisha maisha, utu na heshima ya binadamu na kwamba, hakuna sababu msingi inayoweza kuhalalisha vitendo vya kigaidi kwa kusingizia dini. Vitendo vya kigaidi vimepitwa na wakati na wala havipaswi tena kukumbatiwa na wadau mbali mbali. Jukwaa la viongozi wa kidini nchini Uingereza linapenda kuwaalika wananchi wote wa Uingereza kuongeza juhudi za ulinzi, usalama; huruma, mapendo na matumaini.
Askofu mkuu Justin Welby, Mkuu wa Jumuiya ya Kianglian, amesitikishwa sana na vitendo hivi vya kigaidi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia na kwamba, anawaombea wale wote waliofariki dunia pamoja na majeruhi  ili waweze kupata faraja na hatimaye kupona haraka. Viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamelaani sana vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kutendeka sehemu mbali mbali za dunia.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top