0
Mwenyeheri Paulo VI kunako tarehe 26 Machi 1967, miaka 50 iliyopita alitia mkwaju kwenye Waraka wa kitume “Populorum progressio” yaani “Maendeleo ya watu”. Huu ni waraka ambao bado uko hai sana hasa katika ulimwengu huu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni waraka ambao unatoa kipaumbe cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi kama sehemu muhimu sana wa utume wa Kanisa linalotakiwa kuwa aminifu kwa tunu msingi za Kiinjili. Maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili, ni kati ya vipaumbele vya Kanisa tangu mwanzo na kwamba, maendeleo ni jina jipya la
amani.

Mwenyeheri Paulo VI alionesha ushuhuda wa kinabii kwa kutaka rasilimali na utajiri wa dunia utumike kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu katika ujumla wake na wala si kwa ajili ya kutosheleza matakwa ya watu wachache ndani ya jamii, kielelezo cha kutisha katika ulimwengu mamboleo. Hii ilikuwa ni changamoto kwa Jumuiyaya Kimataifa kushikamana kwa dhati ili kuvunjilia mbali mnyororo wa umaskini, ambao unaendelea kuwatumbukiza maskini katika lindi la umaskini wa hali na kipato, wakati matajiri na wenye nguvu wanaendelea kuneemeka kwa rasilimali na utajiri wa dunia, kwa “kula kuku kwa mrija, wakati maskini wakiendelea kuhesabu mbavu”!
Mwenyeheri Paulo VI akakazia kwa namna ya pekee mshikamano unaosimikwa katika kanuni auni. Kwa Waraka huu, Kanisa katika kipindi cha miaka 50 limeendelea kutoa mchango wa pekee katika sera na mikakati ya kumwinua mwanadamu kutoka katika unyonge wake kwa kujikita katika huduma makini ya binadamu hususan kwenye: sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii kama kielelezo cha Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Kiini cha Waraka wa kitume “Maendeleo ya watu ni kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kutafuta, kukuza na kudumisha amani, haki msingi za binadamu na mshikamano kwa kuwa na mtazamo mpana zaidi unaofumbata binadamu wote.
Waraka huu ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto ambayo ilivaliwa njuga kwa namna ya pekee na Mwenyeheri Paulo VI, kwa kukazia umuhimu wa kushirikiana na kutegemezana ili kuweza kukamilishana kwani binadamu kwa asili ni kiumbe jamii, hawezi kukaa kama kisiwa. Kumbe, hata rasilimali na utajiri wa dunia hauna budi kusaidia katika mchakato wa kupambana na maadui wakuu wa binadamu yaani: ujinga, umaskini na maradhi; mambo ambayo yanaendelea kumnyanyasa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, leo hii hakuna mtu anayeweza kujikinai kwamba, yuko salama asilimia mia moja!
Athari za mabadiliko ya tabianchi kwa mfano zinawagusa na kuwanyanyasa maskini na matajiri pasi na upendeleo. Kwa maneno mengine, haya ndiyo matokeo ya wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi sehemu mbali mbali za dunia, watu wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Kumbe, hapa, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanapaswa kupewa kipaumbele katika sera za kitaifa na kimataifa. Mkazo wa pekee ni kukazia mchakato wa ujenzi wa utamaduni unaoheshimu maisha, utu na haki msingi za binadamu.
Haya ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga na kushuhudiwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Mfumo mzima wa elimu hauna budi kuchangia katika kurithisha tunu msingi za maisha ya kiutu na kijamii katika ulimwengu ambamo kuna tofauti kubwa za kidini, kiimani, kitamaduni na kifikra. Huu ni utajiri unaopaswa kuwaunganisha watu na wala si kuwa chanzo cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kidini. Majadiliano ya kidini, kiekumene na maridhiano kati ya watu ni vipaumbele kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka wake wa Kitume “Maendeleo ya watu” anakaza kusema, maendeleo ni jina jipya la amani duniani. Huu ndio mwelekeo wa Mama Kanisa katika kukazia umuhimu wa uchumi shirikishi unaozingatia mahitaji msingi ya binadamu; kwa kuheshimu utu na haki msingi za binadamu. Ni mwelekeo unaopaswa kumwilishwa katika masuala ya kijamii kwa kujenga na kuimarisha majadiliano katika ukweli na uwazi ili kudumisha utandawazi unaoguswa na mahitaji ya jirani na wala si kinyume chake.
Ni mshikamano unaofumbatwa katika kanuni auni na uhuru wa watu kwani Kanisa kwa njia ya Uinjilishaji wa kina linapania kumwokoa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linataka kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kama alivyowahi kusema, Papa Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume “Spe salvi” yaani “Tumaini linalookoa”. Mwanadamu anaweza kukombolewa kutoka katika shida na mahangaiko yake ya kiroho na kimwili kwa njia ya huruma inayomwilishwa katika upendo wa dhati anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Upendo wa Kikristo unawakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi. Kanisa linataka kuwatangazia watu wa Mungu ukweli mfunuliwa ambao ni Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kanisa linataka kuwa ni shuhuda, chombo na Sakramenti ya wokovu kwa binadamu wote!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top