0
Dumishemi umoja na mshikamano kati ya waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ili kujenga upendo na udugu, kikolezo kikuu cha maendeleo endelevu ya binadamu na kama njia ya kukabiliana na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo! Ni maneno ambayo yanakumbukwa na wengi kutoka kwa Padre Gallus Thomas Marandu, C.SS.P., wa Shirika la Roho Mtakatifu aliyefariki dunia
Jumapili tarehe 26 Machi 2017, Temeke, Jijini Dar es Salaam, Tanzania. Marehemu Padre Gallus Marandu ataagwa rasmi Jumatano tarehe 29 Machi 2017 kwa Ibada ya Misa takatifu kwenye Makao
Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini, Dar es Salaam, saa 6:00 mchana. Ibada ya Mazishi itafanyika Ijumaa, 31 Machi 2017 kwenye Seminari ya USA River, Jimbo kuu la Arusha, kuanzia saa 6:30 kwa saa za Afrika Mashariki.

Padre Raymond Saba, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, Familia ya Mungu nchini Tanzania imepokea msiba huu mzito kwa huzuni, masikitiko na imani kwa mapenzi  ya Mungu ambayo yametendeka ndani ya mtumishi wake Padre Gallus Marandu ambaye alianza kufanya utume wake kwenye Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kunako mwaka 2001 akiwa ni katibu mtendaji wa Idara ya mahusiano na dini mbali mbali.
Kunako mwaka 2005 akateuliwa kuwa Katibu mtendaji wa Idara ya Wahamiaji, Wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na Utamaduni. Kunako mwaka 2013, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania likampandisha hadhi kuwa ni Msaidizi wa Katibu mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Katika uhai wake, Marehemu Padre Gallus alitekeleza wajibu wake kwa: weledi, uadilifu, ari na moyo mkuu, kiasi cha kuchangia sana katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania katika medani mbali mbali za maisha.
Itakumbukwa kwamba, Marehemu Padre Gallus Thomas Marandu, alizaliwa tarehe 26 Septemba 1956 Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, kunako tarehe 7 Julai 1982 akaweka nadhiri zake za kwanza kwenye Shirika la Roho Mtakatifu, maarufu kama “Holy Ghost Fathers”. Akakamilisha majiundo yake ya kitawa na kuweka nadhiri za daima tarehe 24 Mei 1985 na kunako tarehe 3 Mei 1986 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Padre Saba kwa niaba ya Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anapenda kutoa salam zake za rambi rambi kwa wazazi, familia, ndugu na jamaa wa Marehemu Padre Gallus Thomas Marandu pamoja na wanashirika wenzake wote ambao kwa hakika wamepoteza “Jembe la nguvu” hasa wakati hii Kanisa Katoliki nchini Tanzania linapoendelea na maadhimisho ya Mwaka wa Padre sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo Tanzania Bara.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top