Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwa makini sana katika matumizi ya rasilimali maji, kwani hii ni sehemu ya haki msingi za binadamu! Kuna maelfu ya watoto wanaopoteza maisha yao kutokana na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji machafu! Kuna watu ambao hadi wakati huu hawana uhakika wa maji safi na salama na matokeo yake afya zao daima ziko mashakani kutokana na kushambuliwa na magonjwa! Baba Mtakatifu Francisko anawataka watu kuwajibika vyema katika kulinda, kutunza na kudumisha vyanzo vya maji kwani maji ni uhai!
Wananchi kwenye vijiji mbalimbali vilivyoko Tarafa ya Ruvuma Wilayani Songea Mkoani Ruvuma, nchini Tanzania, wameondokana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama baada ya kuzinduliwa kwa miradi 20 ya visima vya maji ya pampu yenye thamani ya zaidi ya Mil.140 ambayo yatatumika na wananchi hao. Akizindua miradi mitatu ya visima hivyo kwenye shule za msingi za Mgazini, Mapinduzi na Kiburungi, mfadhili wa miradi hiyo, Bruda. Dr. Ansigar wa Shirika la Mtakatifu Benedikto Peramiho, amesema ni jukumu la kila mmoja, likiwemo Kanisa, kuhakikisha wanafunzi mashuleni wanakuwa na maisha bora na afya njema ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao, kwa kuboresha miundombinu hasa upatikanaji wa maji safi na salama.
Hii pia ni njia ya kupambana umaskini, kwani magonjwa yanawanyong’onyeza watu kiasi hata cha kushindwa kuchangia katika ustawi na maendeleo yao binafsi na taifa katika ujumla wake! Akiwa Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Joseph Peramiho, ambayo inaendeshwa na Kanisa Katoliki, amesema tangu afike nchini Tanzania miaka 30 iliyopita ameshuhudia jamii na hasa watoto wakikumbwa na matatizo makubwa ya kiafya kama upungufu wa damu, ugonjwa wa kuhara, minyoo, malaria, surua na upele, ambayo yamechangiwa na ukosefu wa huduma za maji safi na salama.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Hospitali hiyo ya Misheni, jitihada mbalimbali zimefanyika ambazo zinakabiliana na magonjwa ya watoto, na kuongeza kuwa kwenye Hospitali hiyo ameletwa Daktari bingwa wa watoto hali ambayo imepunguza vifo vya watoto wachanga. Katika hatua nyingine ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo, Hospitali hiyo itajenga wadi pekee ya watoto ambao watalala watoto tu na jirani yake itajengwa wodi ya wazazi na wataenda wadi ya watoto wao kuwanyonyesha tu, kabla hawajaruhusiwa kurejea makwao. Aidha amesema mpango huo utakuwa ni wa pekee nchini Tanzania kwani kwa hivi sasa takribani kwenye Hospitali zote nchini Tanzania, wazazi hulala kwenye wodi pamoja na watoto wao wachanga, hali ambayo wakati mwingine si nzuri sana kwa afya ya watoto wachanga! Lengo la Kanisa ni kuendelea kuwa shuhuda na chombo cha kukuza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Mkakati huu ni sehemu ya Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Na Padre ANTHONY CHILUMBA.
Songea, Tanzania
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni