Ilikuwa ni tarehe 28 Februari 2013, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipong’atuka rasmi kutoka madarakani na kuhama kutoka Vatican ili kupisha mchakato wa mikutano ya Makardinali na kuamua kwenda kuishi kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma. Alikiri kwamba, afya na umri wake, ni mambo yaliyokuwa yanamzua kutekeleza kwa ukamilifu majukumu na dhamana yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na hivyo, kuamua kung’atuka kutoka madarakani
ili aweze kupata muda wa kusali kwa ajili ya kuliombea Kanisa, kutafakari na kujipumzisha, mambo ambayo ameendelea kuyafanya tangu wakati huo!
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, tukio hili lilifuatiliwa na maelfu ya watu waliomsindikiza Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akiwa anaelekea mjini Castel Gandolfo kwa Elikopta! Kila sehemu alikopitia, watu walimpungua mkono, ishala ya kumtakia mema katika maisha yake mapya baada ya kufanya maamuzi magumu yaliojaa ushupavu, imani na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake. Maneno machache aliyoyasema alipofika mjini Castel Gandolfo, hadi leo hii yamebakiza chapa katika akili na nyoyo za watu waliokuwepo!
Alisema kwa unyenyekevu mkubwa kwamba, alikua ni hujaji aliyekuwa anasafiri katika awamu yake ya mwisho, ili kukamilisha safari ya maisha yake hapa duniani. Kwa moyo wake wake wote, akili, upendo, sala na tafakari yake ya ndani anapenda kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na binadamu katika ujumla wao. Anatambua kwamba, kulikuwa kuna kundi kubwa la waamini na watu wenye mapenzi mema lililokuwa linamsindikiza kwa sala na sadaka yao. Papa Mstaafu akawaomba kuungana pamoja na Kristo Yesu kwa ajili ya ustawi wa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake!
Tangu wakati huo, tarehe 28 Februari, kila mwaka, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, husali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, ili Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia afya njema ya roho na mwili. Kwa sasa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anajiandaa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 90 tangu alipozaliwa hapo tarehe 16 Aprili 2017. Utakuwa ni muda wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa makuu aliyolitendea Kanisa kwa njia ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika maisha na utume wake kama: Padre, Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni