0

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 8 Mei 2017 amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Kireno, kilichoko mjini Roma. Amewashukuru kwa kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala zao na amewatakia amani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka kwao wenyewe, familia na mataifa yao! Amegusia hija yake ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, kuanzia tarehe 12- 13 Mei 2017 ili kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, tukio la neema na chachu ya upendo kwa watoto hawa kwa Kristo Yesu.
Bikira Maria, aliwasaidia Watoto wa Fatima kuzama katika: wema na upendo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hii ni changamoto kwa wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Kireno kujitahidi kumfahamu, kumpenda na kujifananisha na Kristo Yesu, kiasi hata cha kujisadaka bila ya kujibakiza! Baba Mtakatifu anapenda kuwaalika Wakleri kujiendeleza zaidi bila kuchoka katika majiundo yao ya: Kikristo, Kipadre, Kichungaji na Kitamaduni, daima wakijitahidi kujiweka wakfu kwa uwepo wa mang’amuzi ya upendo wa Mungu ambaye yuko karibu na daima ni mwaminifu; mang’amuzi waliyopata Wenyeheri Francis na Yacinta Marto pamoja na Mtumishi wa Mungu Lucia dos Santos.
Watoto wa Fatima wawe ni mfano bora wa kujiaminisha kwa kukimbilia tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, anayewanyanyua kwa kuwashika mkono; anawafundisha kukua na kukomaa katika upendo kwa Kristo katika umoja wa kidugu! Baba Mtakatifu anawaalika wanajumuiya hawa kumwangalia na kumwomba Bikira na hatimaye, kumwachia nafasi pia ili aweze kuwaangalia, kwani anawapenda kama Mama ili waweze kujifunza kuwa wanyenyekevu na wajasiri katika kufuasa Neno la Mungu, Kumpokea Mwanaye mpendwa Yesu Kristo; kwa njia ya urafiki, waweze kuwapenda pia jirani zao kadiri ya kipimo cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambao ni mlinzi wa Chuo hiki cha Kipapa. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya: maisha, matumaini na amani!
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wanajumuiya hawa kwa namna ya pekee kumwangalia Bikira Maria aliyepata upendeleo wa pekee wa kuhifadhiwa katika Moyo wa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, Fumbo la maisha ya Bikira Maria linawaunganisha wote, kwani Mwenyezi Mungu, alimwangalia Bikira Maria kwa jicho la upendo, jicho linalomwangalia kila mtu na kumwita kwa majina! Uhusiano mwema na Bikira Maria uwasaidie waamini kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Mama Kanisa, kwani wote ni Mama, kwani lile linaloweza kusemwa kwa Bikira Maria linaweza pia kusemwa kwa Kanisa na moyo wa binadamu, kama anavyofafanua Abate Isaac wa nyota!
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wao ni chemchemi ya uhai na bila kuwa na uhusiano wa kimwana na Bikira Maria, mwamini atajisikia kuwa yatima moyoni mwake! Bikira Maria awe ni kimbilio la Mapadre hasa katika nyakati ngumu za maisha na utume wao, ili waweze kupata ulinzi na tunza ya Mama Bikira Maria, daima wajitahidi kuzituliza nafsi zao na kuzinyamazisha kama mtoto aliyeachishwa kifuani mwa mama yake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jumuiya yao itaendelea kuwa ni shamba la mitume, kituo cha umoja na mshikamano kati ya Makanisa mahalia na Roma; wakiwa wameungana katika upendo na ushuhuda wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia wote baraka zake za kitume. Anawaombea kwa Bikira Maria wa Fatima ili awafunde namna ya kuamini, kuabudu, kutumainia na kupenda kama walivyopenda Wenyeheri Francis na Yacinta Marto pamoja na Mtumishi wa Mungu Lucia dos Santos.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top