Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea nchini Colombia kuanzia tarehe 6 – 11 Septemba 2017 kama sehemu ya mchakato wa kuenzi maridhiano, haki na amani, baada ya Colombia kuwa katika mapigano kwa muda mrefu. Hija hii ya kitume nchini humo inaongozwa na kauli mbiu “Demos el primer paso” yaani “Tupige hatua ya kwanza”. Huu ni mwaliko kwa familia ya Mungu nchini Colombia kupiga hatua katika mchakato wa ujenzi wa amani na upatanisho kwa kufuata nyayo za Baba Mtakatifu Francisko ambaye amejipambanua kuwa kweli ni “Mmissionari wa upatanisho”.
Wananchi wa Colombia kwa muda wa miaka 50 wamekuwa wakipigana vita ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo limewagawa na kuwasambaratisha wananchi wa Colombia. Kumbe, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia inapania pamoja na mambo mengine kuimarisha mchakato wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho nchini Colombia. Ili kufanikisha mchakato huu muhimu katika maisha, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kuna haja ya kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kubadilika, tayari kukutana na wengine. Huu ni wakati muafaka kwa Colombia kugundua utambulisho wake kama taifa, ili kuudumisha kwa nguvu zote bila kutoa tena nafasi ya kutoweka kwa amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.
Askofu mkuu Luis Augusto Castro Quiroga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia katika hotuba yake elekezi wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 103 wa Baraza la Maaskofu katoliki Colombia amekazia umuhimu wa familia ya Mungu nchini Colombia kuipatia uzito wa pekee kabisa hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kwa kufumbata ukweli utakaosaidia kukoleza msamaha na upatanisho wa kitaifa.
Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiandaa kikamilifu kumpokea Baba Mtakatifu Francisko; kumsikiliza kwa makini na hatimaye, kumwilisha mafundisho yake katika uhalisia wa maisha ya familia ya Mungu nchini Colombia. Papa Francisko ni kiongozi wa watu, anayependa kujishikamanisha na watu katika shida na mahangaiko yao, ili aweze kuwatangazia Injili ya furaha, matumaini na mapendo. Khalifa wa Mtakatifu Petro anataka kwenda kuwatembelea na kuwaimarisha ndugu zake katika imani; ni mchungaji mwema na kiongozi wa maisha ya kiroho anataka kukazia kweli za Kiinjili, kwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Colombia.
Ari na moyo wa kimissionari ni kati ya changamoto kubwa zinazofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu kwa wakati huu, kwa kuwasukuma Wakristo kutoka kifua mbele, kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu! Anataka kuchochea karama ya shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Colombia. Lengo ni kuwasaidia wananchi wa Colombia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani, jina jipya la maendeleo endelevu! Huu ni muda wa kujenga utamaduni wa kusikilizana kwa makini, kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti msingi. Kuna haja ya kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza katika ukweli, ili hatimaye, waweze kupata ukweli mtimilifu unaofumbatwa katika upatanisho.
Askofu mkuu Luis Augusto Castro Quiroga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia anaitaka familia ya Mungu nchini humo kujipanga vyema katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu; kwa kuwasaidia watu kukipita kipindi hiki cha mpito wa kitamaduni, tayari kushiriki katika uchaguzi mkuu. Ni wakati wa kuondokana na woga na wasi wasi uliotawala akili na nyoyo zao kwa takribani miaka 50 ya vita ya wenyewe kwa wenyewe; sasa umefika wakati wa kuandika ukurasa mpya, unaowasukuma kama taifa kuanza mchakato wa kutembea pamoja katika mawimbi ya msmaha na upatanisho wa kweli; unaotibu na kuganga madonda ya chuki, uhasama na hali ya kutaka kulipizana kisasi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni