0

Ndugu wapendwa, baada ya kutafakarishwa juu ya huruma ya Mungu katika dominika iliyotangulia, leo twamuona Mtume Petro akijibu swali la Yesu, akisema wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.  Na tunamsikia Yesu akimjibu Petro akimwambia wewe utaitwa Petro yaani mwamba. Tunaambiwa kuwa Petro anapewa jina hili si kwa ajili yake mwenyewe bali sababu ya uthabiti wa imani yake. Ungamo la Petro kwamba wewe ni Masiha yaani yule aliyengojewa, mwana wa Daudi, anayetangaza ujio wa ufalme na anayeonesha watu huo ufalme na kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai, yaani Mwana na mwakilishi pekee wa
Mungu na mwenye hiyo roho ya Mungu na aliye katika ushirika na huyo Mungu ni ushuhuda tosha wa imani hai.
Na pia jibu la Yesu laonesha kuwa tamko la Petro latokana na ufunuo na si toka akili ya kawaida ya mwanadamu. Hili ni ungamo la imani na Yesu anamkabidhi mamlaka ya usimamizi wa kanisa.
Imani ya Petro ni zawadi toka kwa Mungu, imani ambayo kwayo, Bwana Yesu analijenga kanisa lake. Hiki kilichotokea kwa Petro kinaweza kutokea pia kwa mkristo ye yote ikiwa ataweka imani yake kwa Kristo. Baba Mtakatifu Francisko akiongea kuhusu hili ungamo la Petro anaweka wazi mbele ya watu swali hili – imani yako inaonekanaje? Au ikoje? Je, ni imara, kama mwamba? Daima Kristo anatafuta imani thabiti katika mioyo yetu, hata kama si kamilifu lakini iliyo kunjufu, ya kweli. Kama akiipata basi hapa atajenga Kanisa lake. Yesu ni jiwe la msingi na Petro ni jengo hai linaloonekana na alama ya umoja. Kila mbatizwa anaitwa kushudia maisha yake kwa ubatizo tuliopokea. Lile swali la Yesu kwa Petro, wewe wasema mimi ni nani linaelekezwa kwetu kila wakati wa maisha yetu. Hatuna budi kutoa jibu sahihi lakini pia hatuna budi kumwomba Mungu daima ili tuweze kupata jibu sahihi, atupatie zawadi ya kujibu kwa moyo mkunjufu. Na hili ndilo ungamo la imani yetu, ndiyo nasadiki yetu.

Sehemu hii ya Injili tunayosoma leo toka Mathayo yaweza kuwa ni kiini cha ujumbe wake wa kuandika hii Injili. Mwinjili Mathayo anaandika Injili yake akionesha mambo makubwa yanayoweza kutendeka tukiwa na imani katika Yesu Kristo.  Hapa tunaona Simoni Petro kwa niaba/jina la wale mitume wengine anakiri imani  “Wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu aliye hai” na Yesu anamjibu, wewe ni mbarikiwa, ni mwamba na juu yako nitalijenga Kanisa. Bila shaka kwake Kristo ni furaha ya pekee kwani kwa jibu hili ina maana kuwa roho mtakatifu anafaya kazi ndani ya mitume. Kwamba wanaweza kujibu au kutoa majibu ambayo yanamfaya Yesu aamini ukomavu wa imani na kwa sasa anaweza kuwakabidhi mitume utume wake. Ili kuanzisha kanisa lake alipenda kuona imani katika wafuasi wake. Ilibidi aulize hilo swali ili kujiridhisha. Yesu anataka kujenga Kanisa lake na ili hili lifanikiwe anatafuta ushuhuda toka kwa wafuasi wake.
Injili ya leo yatoa changamoto kwa kila mkristo. Lile swali la Yesu kwa Petro laelekezwa pia kwetu. Imani yako ikoje? Yesu anapata nini toka kwako/kwetu? Moyo kama mwamba au moyo legelege? Wewe wasema kuwa Yesu ni nani? Lakini hapa lahitajika jibu si tu la maneno bali la ushuhuda. Kadiri ya Mwinjili Mathayo, kanisa ni Kristo – Mt. 18:20 – kwa maana wanapokusanyika pamoja wawili au watatu kwa jina langu, mimi nipo katikati yao. Kanisa linahusianishwa moja kwa moja na ufalme wa Mungu. Matayo anatambua wazi kuwa ufalme haujakamilika katika ukamilifu wake. Uwepo bado wa wadhambi ni dhihirisho hilo. Hata hivyo Yesu alikuja kutangaza ufalme wa Mungu na ujumbe wake. Kwa wale ambao hawakumwona Yesu kama wale wafuasi, basi kanisa latumika kama namna ya kumfahamu huyo Yesu na ujumbe wake. Kazi ya kanisa ni kuendelea kutoa ushuhuda wa uwepo wa huyo Yesu na ufalme wake. Uwepo wa wafuasi ni dhihirisho la uwepo wa huo ufalme.

Neno la Mungu katika somo la pili la leo linatusaidia au linatuongoza kutambua kwa mapana namna ya kuweza kutoa majibu kwa lile swali la Yesu kwa Petro. Mtume Paulo anaongea kuhusu hekima ya Mungu inayopita ufahamu wetu wa kibinadamu. Mtume Paulo anasema kwa hiyo hekima watu wote wanaokolewa. Nasi tunaalikwa kuifahamu hekima hiyo ili tuweze kupata faida za huo ufalme na kwa hiyo hekima tuweze kumkiri Kristo kuwa ni Masiha na Mwana wa Mungu aliye hai. Ni hekima hiyo ya Mungu inayotuwezesha kumkiri Kristo kuwa ni Bwana na Masiha.

Tumsifu Yesu Kristo.
Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

Chapisha Maoni

 
Top