Baba Mtakatifu Francisko kwa barua yake binafsi, “Motu Proprio” “Maiorem hac dilectionem” yaani “Kuhusu sadaka ya maisha” amefungua njia ya kutangazwa wenyeheri na hatimaye, watakatifu waamini ambao hali wakisukumwa na upendo, wamesadaka maisha yao kwa ajili ya jirani zao kwa kukubali na kupokea kifo kabla ya wakati kama njia ya kumfuasa Kristo Yesu kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. (Rej. 1Yoh. 3:16). Sadaka ya maisha inataka kutoa kipaumbele cha pekee kwa ushuhuda wa kikristo unaofumbatwa katika upendo, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake; ushuhuda unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mwamini kama njia ya kutafuta ukamilifu wa maisha na hatimaye, utakatifu. Sadaka ya maisha inajikita kwa namna ya pekee, katika fadhila ya : Imani, Matumaini, Busara pamoja na Nguvu.
Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, anakazia umuhimu wa fadhila ya upendo kwa Mungu na jirani, kama njia ya kumwilisha tunu msingi za kiinjili sanjari na kujikita katika kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya Kristo na Imani ya Kanisa lake. Haya ni mambo msingi ambayo yamekuwa yakitiliwa mkazo na Mababa wa Kanisa tangu nyakati zote. Hapa mashuhuda wa upendo kwa nyakati hizi ni pamoja na Mama Theresa wa Calcutta na Padre Pio wa Pietrelcina pamoja na waamini ambao wameuwawa kutokana na chuki za kiimani.
Kinachotiliwa mkazo hapa anasema Kardinali Amato: ni kifo kinachodumu kwa muda mfupi kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda wa upendo wa kikristo. Lazima kuwepo na mwingiliano kati ya sadaka ya maisha na kifo cha ghafla. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, walau fadhila ya upendo inamwilishwa katika maisha ya kila siku ya mwamini, hadi pale mauti inapomfika na mwishoni, lazima kuwepo na cheche za utakatifu wa maisha mara baada ya kifo cha mwamini huyu kama sharti muhimu la kutangazwa kuwa Mtakatifu. Anasema, Kanisa litaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watumishi wa Mungu kutangazwa kuwa wenyeheri kwa njia ya: kifodini, ushuhuda wa fadhila za kishujaa; ushuhuda wa upendo wa hali ya juu kabisa unaofumbata kifo. Dhana hii ni matunda ya tafakari ya kina iliyotolewa na Papa Mstaafu Benedikto XV aliyekazia ushuhuda wa upendo kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake.
Kama inavyoeleweka na kufafanuliwa na Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa Katoliki kwamba, mwamini anaweza kutangazwa kuwa Mwenyeheri kwa njia ya kifo dini, kielelezo cha pekee katika kumfuasa Kristo, lakini, ikumbukwe kwamba, kielelezo cha juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake ni upendo kwa Mungu na jirani. Kifodini kadiri ya ufahamu wa Kanisa ni kupokea kwa hiyari kifo kama kielelezo cha upendo kwa Kristo! Ni kupokea kifo kutokana na chuki za kiimani, au fadhila nyinginezo za Kikristo. Kifodini ni kielelezo cha unyenyekevu kwa mwamini anayesamehe kama njia ya kumuiga Kristo Yesu, ambaye alipokuwa pale juu Msalabani aliwaombea watesi wake msamaha kutoka kwa Baba yake wa mbinguni! Njia ya Pili inayomwezesha mwamini kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri ni katika mchakato wa kumwilisha fadhila za kishujaa zinazotekelezwa kwa haraka, bila kusita na kwa moyo mkunjufu, kiasi cha kuonekana kuwa ni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si tu juhudi au nguvu za kibinadamu.
Ikumbukwe kwamba, huu ni mwelekeo unaomwezesha mwamini kufikiri na kutenda mintarafu mwanga wa Injili ya Kristo! Fadhila zinazozungumziwa hapa ni zile fadhila tatu za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo bila kusahau fadhila kuu nne yaani: Busara, Haki, Nguvu na Kiasi. Fadhila zote hizi zinafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa, katika Mashauri ya Kiinjili, au Nadhiri kama zinavyojulikana na wengi: Ufukara, Utii, Usafi kamili na Unyenyekevu.
Kardinali Angelo Amato anaendelea kufafanua kwamba, Njia ya Tatu inayomwezesha mwamini kutangazwa kuwa Mwenyeheri, ambayo waamini wengi hawaifahamu sana, lakini imefafanuliwa katika Sheria, Kanuni na Tararibu za Kanisa katika Sheria za Mwaka 1917 inayojulikana kama kutangazwa Mwenyeheri kwa kutumia kanuni ya Ibada ya zamani“Equipollente” ambayo kimsingi inatumika kwa nadra sana katika Kanisa kwa ajili ya kesi maalum “Casus excepti”. Hizi ni njia ambazo Mama Kanisa anazitumia kwa ajili ya kuwatangaza waamini wake kuwa wenyeheri na watakatifu, lakini kadiri ya historia inavyozidi kusonga mbele, njia hizi zinazonekana kana kwamba, zinawatenga baadhi ya waamini ambao wamekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kwa njia ya ushuhuda wa upendo wenye mvuto na mashiko! Yesu mwenyewe anasema, hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. (Rej. Yoh. 15:13). Kardinali Angelo Amato anasema, sasa ni wakati kwa Maaskofu mahalia kuanza kutekeleza barua hii binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Kuhusu sadaka ya maisha” kadiri ya mazingira ya Makanisa yao. Lengo ni kuonesha ushuhuda wa aina mbali mbali za utakatifu unaoyapamba maisha na utume wa Kanisa kwa watu wa Mataifa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chanzo cha habari ni http://sw.radiovaticana.va
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni