Jimbo Katoliki Tunduru Masasi nchini Tanzania linasikitika kumpoteza mpendwa wao Baba Askofu Castory Msemwa aliyefariki tarehe 19 Oktoba 2017, saa 7 mchana nchini Oman. Kwa mujibu wa Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki Tunduru Masasi, Padri Jordan Liviga, anasema, Askofu Msemwa amefariki dunia akiwa mjini Muscat (Oman), wakati wa safari ya kwenda nchini India kupata matibabu ya maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.
Marehemu Msemwa amekuwa na tatizo la kiafya kwa kipindi cha miaka miwili, na amekuwa akipata tiba mbalimbali na kuendelea na utume
kama kawaida. Aliondoka nchini siku ya Jumatano 18 Oktoba kuelekea nchini India kwa matibabu kabla hajafariki dunia. Padri Liviga amebainisha kuwa utaratibu wa kuuleta nchini mwili wa marehemu Askofu Castory Msemwa siku ya Jumapili Dar es Salaam unafanyika. Na hivyo taarifa zaidi za utaratibu wa mazishi zitatolewa baadaye.
Askofu Castory Paul Msemwa amezaliwa mwaka 1955 katika kijiji cha Kitulira, Parokia ya Matola Jimbo Katoliki Njombe. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Motola, baadaye Sekondari katika Seminari Kuu ya Peramiho ambapo pia alisomea Falsafa na Teolojia kati ya mwaka 1981 na 1987. Alipata daraja ya Upadri tarehe 7 Juni 1987. Amekuwa Paroko Msaidizi na kiongozi wa vijana jimboni Njombe. Alikuwa pia mwalimu na amesomea katika Chuo cha Kipapa cha kitasaufi cha Teresiaunum Roma na kuhitimu mwaka 1996. Alipata Daraja la Uaskofu tarehe 30 Januari 2005 na kusimikwa rasmi katika Jimbo Katoliki Tunduru Masasi tarehe 25 Agosti 2005.
Mwenyezi Mungu ampumzishe pema mbinguni, Amina.
Chanzo cha habari ni TEC
Na Bernard James, DSM.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni