PAROKO wa Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, Kizota
Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Padri Joby
Tharayil amewataka waamini nchini kusali Rozari Takatifu kwa Imani kuu, jambo ambalo litawasaidia
kuishi maisha ya amani huku shetani
akikosa nafasi kwenye familia zao.
Ameyasema hayo
katika adhimisho la Misa ya kuadhimisha mwezi wa Rozari Takatifu yaliyoanza kwa
maandamano na mafundisho ya jumuiya hadi jumuiya iliyoenda sambamba na uzinduzi
wa ofisi mpya ya Parokia.
Padri Joby amesema
kuwa ni jambo la kumshukuru Mungu kuadhimisha mwezi wa Rozari katika Parokia
yake kwani tangu mafundisho yaanze kutolewa kuhusu umuhimu wa kusali Rozari
waamini wamekuwa na mwitikio mkubwa huku kwa kiasi kikubwa wakitambua umuhimu
wake tofauti na hapo awali.
“Katika Parokia yetu
tuliweka mikakati ya kuwafundisha waamini wetu juu ya umuhimu wa kusali Rozari
kwa Imani japo ilikuwa kazi ngumu kwani wengi wanasali kwa mazoea na wengine
hawajui kabisa, ila tuliendelea kuwafundisha kuanzia watoto mpaka wazee na
kweli tumefanikiwa wanajua kusali na wametambua umuhimu wake, nawaomba tusiwe
wavivu, “ amesema Paroko Joby.
“Wapo waamini ambao
wamekuwa wakisali Rozari Takatifu kwa
mazoea huku wakiwaza mambo yao mengine ya kifamilia na changamoto za
maisha kwa sababu ya kutojua umuhimu
wake jambo ambalo linasababisha kuendelea kuangamizwa na Shetani.
Pale waamini
wanaposali Rozari Takatifu kwa Imani wanajifunika na ulinzi wa Mungu kwenye
maisha yao, shetani hapati nafasi magonjwa na mikosi havitawafika bali
watafanikiwa kwenye shughuli zao,wenye shida zitatatuliwa na kuendelea kutafakari maisha ya baadaye.”
Vile vile Ameongeza
kuwa kwa sasa Dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali, watu wanapenda mambo
ya kidunia zaidi kuliko Mungu na matokeo yake Imani yao kuwa haba na kuanza
kutangatanga kwenye madhehebu mengine hata kwenda kwa waganga wa kienyeji na
hatimaye kuangamia.
Amewataka waamini
kutambua kuwa pale wanapojikita kumuomba Mungu wanatengeneza maisha mazuri ya
mbinguni, hivyo wajiepushe na mambo ya kidunia kwa kutaka kupata vitu ambavyo
havitawafikisha popote.
Katika hatua
nyingine amewashukuru waamini wa parokia hiyo kwa ushirikiano waliouonesha
kukamilisha Ofisi ya Parokia yenye vyumba vitano iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 35
ndani ya miezi mitatu.
“Parokia hii ina
miaka miwili tangu kuanzishwa kwake lakini tumekuwa na mafanikio makubwa
kupitia umoja wa waamini kuanzia watoto hadi wazee ambao wamekuwa wakijitoa kwa moyo wote ukilinganisha kwamba ni familia 586 wanafanya
kazi, kama familia moja nawaomba waendelee na jitihada hizo,” amesema Paroko
Joby.
Hata hivyo amesema wana mpango wa kujenga Kanisa kubwa la kihistoria pamoja na kuanzisha Miradi mbalimbali ikiwemo ya maduka kwani Kanisa lililopo kwa sasa ni dogo kadri parokia inavyozidi kukua.
Chanzo cha habari TEC
Na Doreen Aloyce, Dodoma
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni