0

Madaraka yoyote yakitumika vibaya yanaunda ukosefu wa uaminifu na kuleta  vizingiti, lakini mitume wa Yesu wanaalikwa kuwa makini na wasijiweke juu ya wengine kwa hali yoyote badala yake watoe huduma. Haya ni maonyo yanayojitokeza katika mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye uwanja wa Mtakatifu Petro Jumapili tarehe 5 Novemba 2017 akitafakari Injili ya Siku. Katika Injili hiyo kwa ujumla anawaalika wote kutokuwa na tabia za kiburi, bali kuwa watu wa kawaida na kujikita kwanza kumtafuta na kufuata Yesu.


Injili ya siku ya Jumapili kutoka Matayo (23,1-12), mahali ambapo Yesu anawaonya vikali waandishi na mafarisayo, kuwataka watu wafuate kile ambacho wanasema wao lakini si kutenda wanavofanya, kwa maana wao wanasema lakini hawatendi na kwa njia hiyo Baba Mtakatifu anasema, hiyo ni tabia ya wengi hasa wanaoshikilia  madaraka, na hayo ni madaraka ya raia na hata ya Kanisa, ambayo mra nyingi wanaagiza wengine kutekeleza hata kama ni ya kweli na haki lakini wao hawadiriki kamwe kuyaweka katika matendo binafsi. Hawa ni ndumila kuwili!  Baba Mtakatifu anathibitisha.

Ni tabia mbaya huduma ya madaraka ya namna hii! badala ya kuwa mstari wa mbele na kutoa mfano ulio bora anasema Baba Mtakatifu. Akifafanua zaidi, madaraka yanatokana na kutoa mfano mwema, ili kuwasaidia wengine waweze kutenda jambo la haki na wajibu hata kukabiliana na majaribu ambayo yanajitokeza katika yao ya maisha. Baba Mtakatifu anatoa wito wa kuishi madaraka kama njia kiongozi ya kusaidia kwa maana yakitumiwa vibaya hugeuka kukandamiza, pia hayatoi nafasi ya mtu kukua , badala yake ni kujenga hali ya ukosefu wa uaminifu na vizingiti, hatimaye pia kupelekea ufisadi. Injili ya Yesu inathibitisha baadhi ya tabia hasi za waandishi na wafarisayo kama vile tabia za kufurahia nafasi za kwanza katika masinagogi, na salam katika masoko.
Hivi ni vishawishi vya kiburi ambavyo siyo rahisi kuvishinda, kwa maana ni tabia ya kuishi kifitina tu.
Yesu anawaeleza mitume wake na kuwaalika wasijiite walimu au viongozi kwa maana yupo mwalimu mmoja, ambaye ni mkubwa na ambaye atakuwa mtumishi wao Baba Mtakatifu anasisitiza. “Sisi kama mitume wa Yesu hatupaswi kutafuta cheo, utukufu, madaraka au ukuu wa aina yoyote”, Baba Mtakatifu anasema na kuongeza kutoa mfano binafsi ya kwamba, anashikwa na uchungu kuona mtu ambaye kisaikolojia anaishi au kukimbizana nyuma ya ubatili wa kutafuta utukufu. Badala yake, anasisitiza kuwa, “kama mitume wa Yesu hatuna badi kuacha tabia hizo kwani kati yetu, ni lazima kuwa na tabia rahisi ya kuishi kindugu”.

“Sisi sote ni ndugu, hatuna haja ya kushindana na wengine, hivyo iwapo tumepokea tunu fulani kutoka kwa Mungu Baba wa mbinguni, tunapaswa kuziweka katika huduma ya ndugu zetu, lakini sio kwa ajili ya kujinufaisha binafsi”. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu anatoa wito wa kutofikiria kuwa wewe ni zaidi ya wengine kwasababu anasema,  “unyenyekevu ni msingi kwa ajili maelekezo ya pamoja katika mafundisho ya Yesu, aliyekuja kwa ajili ya kuhudumia na siyo kuhudumiwa”. Anamalizia kuomba kwa  Bikira Maria mnyenyekevu atusaidie kupambana na kiburi na ubatili wa maisha haya.

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican


Chapisha Maoni

 
Top