Monsinyo Guido Pozzo, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ijulikanayo kama Kanisa la Mungu, “Ecclesia Dei” anasema, tume hii inaendelea kufanya majadiliano ya kina na “Jumuiya ya Udugu wa Mtakatifu Pio X” mintarafu hali ya maisha ya Kanisa kwa nyakati hizi. Ili Jumuiya hii iweze kutambulika rasmi kadiri ya Sheria na miongozo ya Kanisa inapaswa kuwa na umoja kamili na Kanisa zima kama inavyofafanuliwa na kupembuliwa na Sheria za Kanisa na wala si vinginevyo.
Hadi sasa Jumuiya hii haijatambuliwa rasmi kisheria. Lakini juhudi zinaendelea kufanywa ili siku moja, iweze kutambuliwa kisheria, lakini ikumbuke kwamba, umoja na Kanisa ni sababu msingi ya kuweza kwa Jumuiya hii kutambuliwa rasmi na Kanisa. Majadiliano yanayoendeshwa kwa sasa kimsingi yanafumbata: Mafundisho tanzu ya Kanisa; Nidhamu ya Sakramenti, mambo ambayo kimsingi yanagusa: Mafundisho ya Kanisa, Mapokeo na Uelewa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, mambo ambayo yanafahamika sana na Jumuiya ya Udugu wa Mtakatifu Pio X.
Hivi karibuni kiongozi mkuu wa Jumuiya ya Udugu wa Mtakatifu Pio X alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ili kumwelezea hali halisi na msimamo wa Jumuiya yake. Mkutano huu ni sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano na utamaduni wa watu kukutana, ili kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukuza na kudumisha umoja wa Kanisa ndiyo maana Jumuiya ya Udugu wa Mtakatifu Pio X haina budi kutambua kwamba bado kuna matatizo, changamoto na vikwazo vinapopaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu kabla ya Jumuiya hii kutambuliwa rasmi na Kanisa.
Hapa, umuhimu wa pekee kwanza kabisa ni kwa Jumuiya hii kutambua kwamba, wanachama wake ni Wakatoliki wanaopaswa kuwa wazi ili kuweza kukumbatia mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kufikia muafaka. Vinginevyo itakuwa ni vigumu sana kwa Jumuiya hii kutambuliwa kisheria ikiwa kama matatizo na changamoto zilizopo hazijapewa ufumbuzi wa kudumu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni