0
Ifuatayo ni barua ya kichungaji kutoka kwa Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza Tanzania anayepembua kwa kina na mapana maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza; Maadhimisho ya Mwaka wa Padre Tanzania pamoja na Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 150 ya Ukristo Tanzania Bara! Anagusia pia mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa ziara za kichungaji zinazofanywa na Askofu Mahalia!
Wapendwa Familia ya Mungu, “Oneni, basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo.” – (1Yn.3:1). Ninawaandikia barua hii ya kichungaji kwa lengo la kuwakumbusha mambo machache yakiwemo haya  yafuatavyo:
  1. MWAKA WA HURUMA YA MUNGU:
Kwa moyo mkunjufu, ninamshukuru Mungu pamoja nanyi kwa fursa adhama tuliyopewa ya kuadhimisha Jubilei ya Huruma ya Mungu. Pia ninawapongeza wote ambao kwa kadiri ya wajibu, nafasi na majukumu yao wamejitosa kuitumia vema fursa hii ya neema na wokovu kwa manufaa yao wenyewe na kwa manufaa ya wengine. Kwa kuzingatia mrejesho na mang’amuzi niliyoyapata kutoka katika parokia mbalimbali za Jimbo letu Kuu, na pia uhitaji uliodokezwa na wadau mbalimbali, nawatangazia kwamba ili azma ya kukidhi kiu na mahitaji ya kiroho ya waamini itekelezwe, kila parokia inaruhusiwa kuendelea na maadhimisho ya Huruma ya Mungu mpaka tutakapotangaza tarehe rasmi ya kuhitimisha kijimbo baadaye mwaka ujao.
  1. JUBILEI YA MIAKA 150 YA UINJILISHAJI TANZANIA BARA:
Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu (Holy Ghost Fathers) walitua Bagamoyo tarehe 3 Aprili 1868. Huo ukawa ni mwanzo wa harakati za uinjilishaji ambao matunda yake ni kuzaliwa kwa kanisa Katoliki katika maeneo ya Afrika ya Mashariki na ya Kati. Tumebakiza miaka miwili ili kanisa Katoliki hapa Tanzania Bara litimize umri wa miaka 150. Hilo ni tukio kubwa la imani na utume wa kanisa. Kitaifa, safari ya kuelekea kwenye maadhimisho ya miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania bara imezinduliwa huko Rubya, Bukoba tarehe 1 Oktoba 2016. Katika Jimbo letu Kuu la Mwanza, mtatangaziwa baadaye kuhusu tarehe ya uzinduzi kijimbo na  ni harakati  na mipango gani ya kuzingatia.
  1. JUBILEI YA MIAKA 100 YA UPADRE NCHINI TANZANIA:
Mapadre wa Kwanza wazalendo wa nchi hii walipewa daraja la upadre huko Rubya, Bukoba mnamo tarehe 15 Agosti 1917. Walikuwa ni: Pd. Angelo Mwilabure (mzaliwa wa Kome), Pd. Celestine Kipanda (mzaliwa wa Kagunguli), Pd. Willibald Mupapi na Pd. Oscar Kyakaraba. Walipopewa daraja, walifungamanishwa (incardination) na Vikariati ya Nyanza Kusini. Baadaye, yalipoundwa majimbo, Pd. Angelo na Pd. Celestine wakawa wa Jimbo la Mwanza na wenzao yaani, Pd. Willibald Mupapi na Pd. Oscar Kyakaraba wakawa wa Jimbo la Bukoba. Pd. Angelo Mwilabure amezikwa Sumve, Pd. Celestine Kipanda amezikwa Kagunguli (Ukerewe, sasa Jimbo Katoliki la Bunda).
Kwa ajili ya kumbukumbu ya kihistoria, ninapenda pia kuwadokezea kwamba , sambamba na mapadre hao wanne, mwaka ule wa 1917 walipadrishwa pia wenzao wawili ambao walitokea Rwanda, nao ni Pd. Donatus Liberaho na Pd. Joseph Bugondo ambao pia walisoma huko Rubya. Kitaifa, maadhimisho ya kuelekea miaka 100 ya uwepo wa mapadri wazalendo yalizinduliwa rasmi huko Rubya, Bukoba tarehe 1 Oktoba 2016, na yatafikia kilele katika maadhimisho yatakayofanyika kitaifa huko Dodoma, mwakani mwezi Agosti.
Ninawaomba mzingatie kwamba katika Jimbo kuu la Mwanza, tutafanya uzinduzi wa Mwaka wa Upadre tarehe 5 Novemba 2016 huko Sumve alikolala Padre Angelo Mwilabure. Ninachukua fursa hii kuagiza kwamba waamini walei kutoka parokia zote, mapadre wote (wanajimbo na watawa), na watawa wa kike na wa kiume, mjipange kushiriki kwa wingi tukio hili la kikanisa. Katika mtiririko wa maadhimisho ya mwaka wa Upadre,  tuzingatie mambo yafuatayo:
  1. Zitolewe sala za shukrani kwa Mungu kwa baraka na zawadi ya mapadre. Pia tuendelee kumwomba Mungu azidi kuwaita vijana wema, waadilifu, wenye afya na akili safi ili waitikie wito wa kuwa makasisi wa Bwana, kwani hakika, mavuno ni mengi ila watendakazi ni wachache!
  2. Mapadre watafakari upya juu ya umaana wa wito, uwakfu na utume wao. Aidha, wajitathmini kuhusu ufanisi, changamoto, faraja na matatizo wanayoyakabili katika safari yao kama mapadre. Nawasihi mapadre wote na kila mmoja binafsi, kujikita katika tafiti moyo nyofu na ya kweli, ili maadhimisho haya yawe ni fursa ya kuamsha upya furaha na ari ya kumfuata, kumtangaza na kumtumikia Kristo, kuhani wetu mkuu, ambaye ametushirikisha ukuhani wake bila mastahili yoyote kwa upande wetu.
  3. Zipangwe fursa za tafakari ya mwezi, mafungo ya pamoja, hija, mikesha, toba na kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kujijenga Kiroho, kijamii, kiutu na kiuchungaji.
  4. Ziandaliwe na kutolewa semina kuhusu kanisa, sakramenti (hasa ya daraja), miito, utume, utandawazi na changamoto nyingine za zama zetu, ili wadau mbalimbali ndani ya kanisa wanufaike.
  5. Mapadre wawe tayari kushiriki katika mikakati ya uinjilishaji maalumu (popular missions) utakaolenga parokia maalum hasa zile za pembezoni na zinazodhihirisha uhitaji wa uinjilishaji mpya na wa kina.
  6. Waamini walei na watawa kwa nafasi zao, watafakari na kutathmini juu ya hali na mwenendo wa utendaji wetu sisi wenye daraja na watushauri kwa upendo, ukweli na haki. Aidha, watafakari juu ya mambo wanayopaswa kuyazingatia wao wenyewe ili kuboresha mahusiano, mshikamano na utengemano na makasisi wao.
  7. Familia yote ya Mungu katika Jimbo kuu la Mwanza, ijipime na kuona ni jinsi gani inavyopaswa na itakavyoweza kuwa mdau hai na halisi katika kutekeleza agizo la Kristo, anayewataka wafuasi wake waeneze Habari Njema kwa mataifa yote. Kwa maneno mengine, tujitathmini na kujipanga kuhusu wito wetu wa kuwa kanisa lenye uelewa, utayari na mwelekeo wa umisionari wa dhati, yaani wa hali na mali.

  1. ZIARA ZA KICHUNGAJI:
Ninapenda kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa maparoko, wasaidizi wao, makatekista na halmashauri ya walei kwa juhudi na uwajibikaji wenu katika maandalizi na utekelezaji wa ziara zangu za kichungaji katika parokia mbalimbali. Pamoja na shukrani hizo, nitambue kwamba kuna tofauti za maandalizi, mipango na utekelezaji kati ya parokia na parokia. Hilo haliwezi kuepukika. Hata hivyo, ninapenda kukumbusha na kuagiza yafuatayo yazingatiwe:
  1. Waamini waandaliwe kiroho na kichungaji ili ziara ya kichungaji ya Askofu ambayo kwa kawaida kutokea mara moja kwa mwaka, iwe na manufaa kwao.
  2. Ratiba izingatie matumizi mazuri na halisi ya muda uliotolewa.
  3. Paroko, bila kungojea kudaiwa, amwandalie askofu mapema mambo yafuatayo:
  4. Ripoti ya kichungaaji, inayobainisha mafanikio, matatizo, matamanio, faraja na karaha (consolations and desolations) na changamoto zinazoikabili parokia na jamii inayoizunguka.
  5. Mpango-kazi wa Kichungaji wa parokia katika mwaka wa kanisa unaoendelea.
  6. Bajeti ya parokia kwa Mwaka unaoendelea.
  7. Vitabu vya Kichungaji (ubatizo, kipaimara, ekaristi, ubatizo katika hatari, ndoa, vifo na mazishi).
  8. Vitabu vya kumbukumbu ya mapato na matumizi ya parokia.
  9. Akaunti za parokia.
  10. Orodha (Inventory) halisi (up to date) ya parokia, ikibainisha mali zinazohamishika na zisizohamishika.
  11.  Journal: kitabu cha kumbukumbu ya matukio muhimu yaliyojiri parokiani.
  12. Mass Intentions Register, ikionyesha: kiasi, mwadhimishi na tarehe ya kuadhimisha nia.
  13. Faili la vikao vya kamati tendaji ya parokia.
  14. Faili la vikao vya Halmashauri ya walei ya parokia.
  15.  Faili la vikao vya baraza la kichungaji la parokia.
  16.  Faili la vikao vya kamati ya mipango na fedha ya parokia.
  17.  Faili la vikao vya baraza la usuluhishi la parokia.
       Waamini waandaliwe vizuri ili washiriki vema, kwa ibada, heshima na uelewa katika madhimisho ya sakramenti mbalimbali kama vile kitubio, ekaristi, kipaimara, mpako wa wagonjwa na ndoa. Ushiriki unaokidhi ni fursa ya neema na utakatifuzo. Kwa hiyo, iepukwe tabia ya kwenda kwa mazoea kwa upande wa waamini; na pia mwelekeo wa kutozingatia kwa upande wa mapadre.
  1. UZINDUZI WA PAROKIA MPYA:
Mpaka sasa, Jimbo kuu la Mwanza linazo parokia 35, mbili kati ya hizo zikiwa ni Kapelania za SAUT na BMC\CUHAS, ambazo kisheria zina hadhi ya parokia. Ninafurahi kuwatangazia kwamba hivi karibuni, tutazindua parokia mpya kwa mpangilio ufuatao:
Tarehe 1 Novemba 2016: Parokia ya Nundu (itakayomegwa kutoka katika parokia ya Nyakato).
Tarehe 21 Desemba 2016: Parokia ya Buhongwa (itakayomegwa kutoka katika parokia ya Mkolani).
Tarehe 31 Desemba 2016: Parokia ya Nyanguge (itakayomegwa kutoka katika parokia ya Bujora).
Kwa mantiki hiyo, Jimbo letu kuu litafunga mwaka huu likiwa na idadi ya parokia 38. Ninawaalika walengwa kujiandaa vizuri: kiroho, kichungaji, kimikakati na kwa hali na mali katika maadhimisho ya uzinduzi. Aidha, naziagiza parokia zote, taasisi na mashirika ya kitawa kushiriki na kuonyesha mshikamano katika uzinduzi wa parokia hizi mpya.
HITIMISHO:
Wapendwa, tunaelekea mwisho wa mwaka wa kanisa. Ninawasihi na kuwaalika mjiandae vema kuanza mwaka mwingine wa kanisa. Kipindi cha Majilio kiandaliwe na kuadhimishwa vizuri ili kichangie ukuaji na ukomavu wa imani inayoakisi utakatifu wa watu wa Mungu. Mungu, Baba Yetu ambaye ni Huruma yenyewe, awabariki na kuwalinda.
Ndimi Mchungaji na Mtumishi wenu,
+Juda Thaddaeus S. Ruwa’ichi, OFMCap
Askofu Mkuu wa Mwanza,

Chapisha Maoni

 
Top