Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania ilikuwa ni nafasi nyingine kwa Jumuiya wanafunzi Wakatoliki Watanzania wanaosoma na kuishi Roma kufanya uchaguzi, ili kuwapata viongozi watakaongoza jahazi kwa kipindi cha mwaka 2016 – 2017. Uchaguzi huu ulisimamiwa na Padre Felix Mushobozi na matokeo yake kutangazwa na Padre Joseph Peter Mosha. Majembe yaliyochaguliwa ni Padre Damian Dotto kutoka Jimbo kuu la Mwanza ambaye kwa mara ya kwanza katika historia ya Umoja wa wanafunzi watanzania wanaosoma Roma amechaguliwa kwa awamu mbili mfululizo.
Viongozi wengine waliochaguliwa ni pamoja na Padre Richard Kashinje kutoka Jimbo Katoliki Shinyanga aliyechaguliwa kuwa Katibu mkuu wa Umoja wa wanafunzi watanzania. Sr. Salome Sheshi kutoka Shirika la Mama Yetu wa Usambara, Jimbo Katoliki Tanga amechaguliwa kutunza “Mkoba wa wa vijisenti vya watanzania” Roma. Mkutubu anaendelea kuwa ni Padre Peter Ndunguru wa Shirika la Kazi za Roho Mtakatifu. Viongozi wapya wametakiwa kuwa kweli ni “majembe ya nguvu” katika kuwahudumia watanzania wenzao wanaoishi ughaibuni, ambko kweli “yataka moyo” kutokana na changamoto mbali mbali zilizoko kwa wakati huu.
Ndugu Salvatory Mbilinyi, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Italia amewapongeza viongozi waliomaliza muda wao na wale waliochaguliwa kushika nyadhifa mbali mbali za uongozi miongoni mwa Wanafunzi Wakatoliki wanaosoma mjini Roma. Amegusia umuhimu wa watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa na Hati za kusafiria yaani “Passport” kwa ajili ya ulinzi na usalama wa maisha yao. Amewakumbusha kwamba, raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoishi nchi za nje wanashauriwa kujiandikisha majina na anuani zao mapema iwezekanavyo katika ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoko karibu na kwa mantiki hii kwa wale wanaoishi Roma, Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.
Kama hakuna ofisi hiyo wajiandikishe katoka ofisi za Ubalozi wa Uingereza. Ofisi hizi lazima ziarifiwe mabadiliko yoyote kama vile anuani au uhamaji kutoka katika nchi hiyo kwenda katika nchi nyingine. Kukosa kujiandikisha kunaweza kuzuia au kuchelewesha msaada na ulinzi ambao raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anastahili kupata ikiwa kutatokea msukosuko au shida yoyote! Sambamba na hili, wanafunzi wanaoishi na kusoma mjini Roma wameshauriwa pia kujiandikisha ubalozini ili kuwa na taarifa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni