Mwenyeheri Paulo VI miaka 50 iliyopita alichapisha Waraka wa Kitume “Populorum progression” yaani “Maendeleo ya watu” akiwataka watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kushikamana kwa dhati katika kukuza na kudumisha amani kwani ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu! Ni Waraka unaowahimiza watu wote kujizatiti katika kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu kwa kushirikiana na kushikamana katika upendo wa kidugu! Mwenyeheri Paulo VI alipenda kumwilisha changamoto zilizokuwa zimeibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu: maisha na changamoto za Kanisa katika ulimwengu mamboleo.
Mwenyeheri Paulo VI alitaka kukazia kwa namna ya pekee kabisa: hali ya binadamu, dhamana na wito wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo; umuhimu wa elimu, sera na mikakati ya shughuli za kiuchumi zinazopaswa kusimikwa katika mshikamano unaongozwa na kanuni auni! Waraka huu ni muhtasari wa tafakari aliyoianzisha kunako mwaka 1963 katika masuala uchumi na maendeleo endelevu ya binadamu, hali ya maisha ya kijamii pamoja na kanuni maadili kama kiungo msingi cha maendeleo ya binadamu. Maaskofu, wanataaalimungu pamoja na wanasiasa kadhaa wakachangia mawazo na kazi ikakamilika na kuchapishwa tarehe 26 Machi 1967.
Waraka huu ni tafakari ya ndani kabisa kutoka kwa Mwenyeheri Paulo VI baada ya kutembelea Barani Afrika, Amerika ya Kusini na Asia, akajionea mwenyewe jinsi ambavyo baa la umaskini, ujinga na maradhi yalivyokuwa yanawanyanyasa watu. Ikumbuke kwamba, Mwenyeheri Paulo VI alikuwa ni Papa wa kwanza kuanzisha mchakato wa kutembelea familia ya Mungu nje ya Italia. Waraka wa Kitume juu ya Maendeleo ya watu ni mchango mkubwa wa Mwenyeheri Paulo VI katika ustawi na maendeleo endelevu ya watu kwa kuzingatia historia, tamaduni, hali ya kijamii na kiuchumi.
Hati ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo” linalitaka Kanisa kuonesha umoja na mshikamano na binadamu wote kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kweli liweze kuwa ni chombo cha matumaini kwa watu wa nyakati zote. Binadamu: haki na mahitaji yake msingi; utu na heshima yake ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu. Pili alitaka uwepo mshikamano unaoongozwa na kanuni auni kati ya watu wa mataifa ili kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu kwa kutoa nafasi hata kwa nchi change duniani kuweza kucharuka katika maendeleo.
Kumbe, huu ndio mshikamano wa binadamu katika maendeleo. Yote haya ni sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kutambua na kuenzi haki msingi za binadamu licha ya umaskini wao. Utu na heshima ya binadamu sanjari na umoja, amani na mshikamano kati ya watu ni mambo ambayo hata leo hii yanapaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipochapisha Waraka wake wa Kitume juu ya “Maendeleo ya watu”, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacra Cuore” huko Brescia, Italia kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, wameadhimisha kongamano la kitaifa kuanzisha tarehe 23- 25 Machi 2017 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Elimu na maendeleo kwa ajili ya amani kati ya watu”. Kongamano hili limehudhuriwa na viongozi wakuu kutoka Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu pamoja na wadau mbali mbali wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi na mafao ya wananchi wa DRC.
Katika kongamano hili wajumbe wamekubaliana kimsingi kwamba, Waraka wa Kitume wa Maendeleo ya watu ni chombo cha mshikamano na utawala bora unaozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mshikamano huu unabubujika kwa namna ya pekee kutoka katika tunu msingi za maisha ya kifamilia; mahali ambapo watu wanasaidiana na kutegemezana kidugu, ili kuboresha hali ya maisha ya watu kwa kuondokana na ubinafsi usiokuwa na tija wala mashiko.
Mwenyeheri Paulo VI alikazia haki jamii na haki ya kimataifa ili kujenga na kudumisha mafao ya wengi na utawala bora. Bunadamu na mahitaji yake msingi, haki, amani na utulivu; upendo na mshikamano vikawa ni vikolezo muhimu katika Waraka huu. Amani na usalama vikawa ni jina jingine la maendeleo. Ushirikiano na mshikamano katika kupambana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii sanjari na kukazia usawa, utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwa namna ya pekee kanisa Mafundisho Jamii ya Kanisa katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Utawala bora, uchumi unaojali mahitaji msingi ya binadamu na kwamba, amani ni jina jingine la maendeleo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni